Na Tatu Mohamed
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, ametoa onyo kwa makundi mbalimbali yanayojihusisha na shughuli za ulinzi bila kuwa na utambulisho na mamlaka rasmi, akisisitiza kuwa hakuna mtu au kundi linaloruhusiwa kujichukulia majukumu ya vyombo vya dola.
Katambi ametoa kauli hiyo Septemba 4, 2026 jijini Dar es Salaam ambapo alisema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya watu wanaotumia nguvu kupita kiasi, wakiwemo baadhi ya walinzi binafsi na ‘mabaunsa’.
Amesema baadhi ya makundi hayo yamekuwa yakifanya shughuli za ulinzi bila kufuata taratibu, huku mengine yakitumia silaha, sare au vifaa vinavyoweza kufanana na vile vinavyotumiwa na vyombo vya ulinzi.

“Ni kuelimisha jamii katika kuzuia, kubaini na kutambua uhalifu. Tumekutana na makundi mbalimbali, wakiwemo kampuni za ulinzi binafsi na viongozi wa dini, kwa sababu changamoto nyingi ambazo zimejadiliwa zingeweza kuzaa uhalifu mkubwa kama zisingeshughulikiwa mapema,” amesema Katambi.
Amesema Serikali imekuwa ikiyaona makundi hayo kama wadau wa Jeshi la Polisi katika kulinda raia na mali zao, lakini wajibu huo unatakiwa kutekelezwa kwa mujibu wa sheria na maelekezo ya vyombo vya dola.
Katambi amesema baadhi ya watu wamekuwa wakijipanga na kuunda makundi ya ulinzi bila usajili au utambulisho rasmi, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama wa wananchi.

Amesema Serikali imekutana na baadhi ya makundi hayo na kubaini kuwa baadhi yao hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria, huku wengine wakisema walikuwa na nia njema lakini walitumia njia zisizokuwa halali.
Amesisitiza kuwa hakuna mtu anayeruhusiwa kuunda ‘jeshi’ au kundi linalotekeleza majukumu ya kiusalama bila kutambuliwa na kupewa mamlaka na Serikali.
Katika hatua nyingine, Katambi amezungumzia makundi yaliyokuwa yakihusishwa na Sheikh Mwaipopo, akiwemo ‘Mbwa Mwitu’ na ‘Chui Weusi’, akisema Serikali haiwezi kuruhusu wananchi kujichukulia jukumu la kukabiliana na watu wanaodhaniwa kupanga maandamano au kufanya vitendo vya uhalifu.
Amesema hata kama nia ya kundi hilo ilikuwa kulinda amani, jukumu la kutekeleza sheria na kuhakikisha usalama wa wananchi ni la vyombo vilivyopewa mamlaka na Serikali.
Katambi pia amezungumzia umuhimu wa viongozi wa dini na wananchi kutumia lugha inayojenga umoja na amani, akisisitiza kuwa uhuru wa dini na haki nyingine za kikatiba unatakiwa kutumiwa kwa kuzingatia haki za wengine na maslahi ya Taifa.
Amesema Tanzania imekuwa na historia ya amani na mshikamano bila migogoro mikubwa ya kidini au kikabila, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kulinda hali hiyo.
Aidha, ameitaka mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuwa makini katika kuchapisha maudhui yanayoweza kuchochea chuki, mgawanyiko au kuvuruga umoja na amani ya nchi, akisema wahusika wanaweza kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Kuhusu kampuni binafsi za ulinzi, Katambi amesema Serikali inaendelea kuboresha usimamizi na usajili wa kampuni hizo kutokana na malalamiko mbalimbali yanayohusu mishahara, mikataba, mafunzo na matumizi ya silaha.
Amesema kuna baadhi ya kampuni zimekuwa zikiwapa walinzi silaha bila mafunzo yanayostahili, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wananchi na walinzi wenyewe.
Ametaka kampuni hizo kushirikiana na uongozi wa Jeshi la Polisi katika masuala ya usajili, mafunzo, usimamizi na matumizi sahihi ya silaha.
Katika suala la silaha, Katambi amesema Septemba na Oktoba mwaka huu ni kipindi kilichotengwa kwa ajili ya wananchi kukabidhi silaha haramu au zisizosajiliwa, kwa mujibu wa Tangazo Na. 251 la Agosti 28, 2026.
Amesema wananchi wenye silaha hizo wanapaswa kuzifikisha kwa mamlaka husika kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kupunguza hatari ya matumizi mabaya ya silaha.

Pia amesema Serikali inaendelea na mikakati ya kukabiliana na uhalifu wa mtandaoni na wizi unaofanyika kupitia teknolojia, kwa kushirikisha Jeshi la Polisi, wataalamu wa TEHAMA, kampuni za mawasiliano na wadau wengine.
Amesema baadhi ya hatua tayari zimeanza kutekelezwa, huku akisisitiza kuwa si kila mkakati wa kiusalama unaweza kuwekwa wazi kwa umma.
Kuhusu baadhi ya watu walioitwa na Jeshi la Polisi, Katambi amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua bila ubaguzi, ikiwa ni pamoja na kuwaita watu mbalimbali kwa ajili ya mahojiano pale inapokuwa na sababu za kufanya hivyo.
Ametoa maelekezo kwa Jeshi la Polisi kuhakikisha watu wanaohitajika kwa mahojiano wanapatikana na kufanyiwa taratibu zinazostahili kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza baada ya maelekezo hayo, Sheikh Mwaipopo amefafanua kuhusu makundi ya ‘Mbwa Mwitu’ na ‘Chui Weusi’ yaliyokuwa yakihusishwa naye, akisema hayakuwa jeshi wala hayakuwa na nia ya kuwadhuru wananchi.
“Napenda nitoe ufafanuzi leo, lile halikuwa jeshi wala halikuwa na lengo baya. Tulikuwa na nia ya kujilinda, kuwa na umoja, amani na mshikamano,” amesema Mwaipopo.
Amesema jamii ilitafsiri vibaya uwepo wa makundi hayo, huku akisisitiza kuwa wanachama wake hawakuwa na silaha na walijitahidi kuepuka vitendo ambavyo vingesababisha madhara kwa watu.
Amesema iwapo uwepo wa makundi hayo uliwakwaza au kuwaudhi baadhi ya wananchi, yuko tayari kuomba radhi.

Mwaipopo amempongeza Katambi pamoja na viongozi wa Jeshi la Polisi kwa hatua walizochukua, akisema ameelewa umuhimu wa kuheshimu Serikali na vyombo vilivyopewa mamlaka ya kusimamia usalama.
“Sisi wote tuko hapa, mimi siko juu ya sheria. Kila mmoja anatakiwa kufuata sheria na maelekezo ya Serikali,” amesema.
Amesema kundi hilo liliundwa na wananchi kwa misingi ya uzalendo na si kwa kutumwa na Serikali wala Jeshi la Polisi.
“Serikali haitutumii. Sisi tulifanya kwa ajili ya uzalendo tu,” amesema, akisisitiza kuwa uzalendo haupaswi kutafsiriwa kama kuchochea vurugu au mgawanyiko wa kidini.
Amesema Watanzania wanapaswa kuendelea kuwa kitu kimoja katika masuala ya kitaifa, licha ya tofauti zao za kidini.
Aidha, Mwaipopo amesema wako tayari kushirikiana na Jeshi la Polisi na kufuata taratibu zinazohitajika, ikiwemo mafunzo na matumizi sahihi ya silaha zilizosajiliwa.
Amesema pia kuna umuhimu wa kuwepo kwa sheria na mfumo madhubuti wa kusimamia sekta binafsi ya ulinzi, akisema hatua hiyo itasaidia kuweka wazi majukumu na mipaka ya makundi hayo.
Kwa upande wao, wawakilishi wa kampuni za ulinzi na ‘mabaunsa’ wamekiri kuwepo kwa baadhi ya watu wanaofanya vitendo visivyokubalika, lakini wakasisitiza kuwa si kila anayefanya kazi hiyo ni mhalifu.
Mmoja wa wawakilishi hao amesema baunsa anapaswa kuwa mtu wa amani, uaminifu na anayelinda usalama wa watu pamoja na mali zao, huku akisisitiza umuhimu wa mafunzo na ushirikiano na Jeshi la Polisi.
Amesema changamoto kubwa inatokana na watu wasio na taaluma wanaoingia katika kazi hiyo kupitia madalali au kampuni zisizofuata taratibu, jambo linalochafua taswira ya sekta nzima.


