Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imewataka wakulima, wafugaji na wavuvi kutumia maarifa, taarifa sahihi na teknolojia za kisasa kuongeza tija katika uzalishaji na thamani ya mazao yao, ili kunufaika na fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema matumizi ya teknolojia na maarifa ya kisasa ni muhimu katika kuboresha ubora wa mazao na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinafikia viwango vinavyohitajika katika masoko ya kimataifa.
Akizungumza katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau mbalimbali, Londo amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira yatakayowawezesha wazalishaji kuongeza thamani ya mazao kupitia usindikaji na matumizi ya teknolojia.

Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza kipato cha wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na kuchochea ukuaji wa viwanda na uchumi wa taifa.
“Matumizi ya taarifa sahihi na maarifa ndiyo msingi wa kuongeza tija katika uzalishaji na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema Londo.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uzalishaji kwa kuimarisha miundombinu ya barabara kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kuhakikisha pembejeo zinapatikana kwa wakati na kuendelea kutoa ruzuku kwa lengo la kupunguza gharama za uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo kwa Utaratibu wa Koroba nchini, Geoffrey Kilenga, amesema matumizi ya teknolojia yanaweza kuwa kichocheo muhimu katika kuwawezesha wazalishaji wa Tanzania kunufaika na masoko makubwa ya kikanda na kimataifa.
Amesema Tanzania ina fursa ya kuuza mazao katika masoko ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Ulaya, Asia na Marekani, lakini fursa hizo zinahitaji bidhaa zinazokidhi viwango vya ubora na usalama vinavyotakiwa.
Kilenga amesema moja ya teknolojia zilizooneshwa katika mkutano huo ni kifaa cha AflaBox, kinachoweza kusaidia kubaini kwa haraka uwepo wa sumukuvu (aflatoxin) katika nafaka bila kulazimika kupeleka sampuli maabara.
“Teknolojia kama AflaBox inamwezesha mkulima, msindikaji au mnunuzi kujua ubora wa zao kabla ya kulifikisha sokoni. Hii ni muhimu katika kulinda afya za walaji na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa,” amesema.
Amesema matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kupunguza changamoto zinazowakabili wazalishaji katika kuthibitisha ubora wa mazao, huku yakisaidia kuongeza uaminifu wa wanunuzi na masoko.
Kilenga amewataka wananchi kuhakikisha wanapata mazao kutoka kwa wazalishaji wanaozingatia viwango vya ubora, huku akiwashauri wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo kuendelea kutumia ushauri wa wataalamu katika uzalishaji na uhifadhi wa mazao.
Amesema matumizi ya sayansi na teknolojia katika mnyororo mzima wa uzalishaji ni muhimu katika kuhakikisha Tanzania inazalisha chakula salama, kuongeza thamani ya mazao na kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika masoko ya ndani na nje ya nchi.


