Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) umewataka wawekezaji wa sekta binafsi kutumia fursa zilizopo katika maeneo 38 yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji nchini, ukieleza kuwa miradi hiyo inaweza kuongeza thamani ya mazao, kupunguza upotevu wa bidhaa na kuchochea ukuaji wa shughuli za kilimo na biashara.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Amina Lumuli, amesema maeneo hayo yameandaliwa kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maghala, viwanda, nyumba, majengo ya biashara pamoja na miundombinu ya kilimo na ufugaji.

Amesema marekebisho ya Sheria ya TBA yaliyofanyika Agosti 2023 yameipa taasisi hiyo nafasi pana zaidi ya kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Baada ya marekebisho ya sheria, TBA imepata nafasi kubwa zaidi ya kushirikiana na sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. Tunawaalika wawekezaji kutumia fursa zilizopo katika maeneo yetu kuanzisha miradi yenye tija,” amesema.
Amefafanua kuwa TBA ina ofisi katika mikoa 26 nchini na tayari imefanya upembuzi yakinifu katika maeneo zaidi ya 147 yanayoweza kutumika kwa uwekezaji, huku maeneo 38 yakiwa miongoni mwa maeneo yaliyotangazwa kwa ajili ya kuendelezwa kupitia uwekezaji.

Amebainisha kuwa, moja ya fursa kubwa ni ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhia mazao, ambayo yanaweza kuwasaidia wakulima kupunguza hasara baada ya mavuno na kuhifadhi bidhaa zao katika mazingira yanayolinda ubora.
“TBA ina utaalamu wa kubuni na kujenga miundombinu ya kuhifadhia mazao. Hii itasaidia wakulima kutokulazimika kuuza mazao yao kwa haraka kwa sababu ya kukosa sehemu salama ya kuhifadhia,” amesema.
Aidha, amesema maeneo hayo yanaweza kutumika kujenga miundombinu yenye mifumo ya ubaridi kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa zinazoharibika kwa haraka, zikiwemo samaki, nyama, mboga na matunda.
Ameongeza kuwa, uwekezaji huo unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna, huku ukiongeza muda wa bidhaa kukaa katika hali bora na kuongeza thamani yake kabla ya kufikishwa sokoni.
TBA pia imeeleza kuwa maeneo hayo yana fursa ya kujenga viwanda vya kuchakata mazao, hatua itakayosaidia kuhamisha kilimo kutoka katika utegemezi wa kuuza mazao ghafi kwenda kwenye uzalishaji wa bidhaa zenye thamani zaidi.
Ametoa mfano wa mahindi yanayoweza kuchakatwa kuwa unga na mpunga kuwa mchele, akisema hatua hiyo inaweza kuongeza kipato cha wakulima na kutoa fursa zaidi za ajira katika mnyororo wa thamani wa mazao.
Amesema TBA iko tayari kushirikiana na wawekezaji, wakulima na wafugaji katika kubuni na kutekeleza miradi inayolenga kuongeza thamani ya uzalishaji wa kilimo na ufugaji.
“Tunawahakikishia wawekezaji na Watanzania kwa ujumla kwamba TBA iko tayari kushirikiana nao kutumia maeneo haya kuanzisha miradi yenye tija. Lengo ni kujenga miundombinu itakayochochea uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao na kuchangia maendeleo ya uchumi,” amesema.
Amesisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya kilimo na viwanda vya kuchakata mazao ni muhimu katika kujenga mnyororo wa thamani unaowaunganisha wakulima na masoko, huku ukichochea ajira na kuongeza mchango wa sekta ya kilimo katika uchumi wa taifa.


