Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Eatfresh (GBRI Business Solutions) imesema ufadhili wa zaidi ya Sh milioni 700 ulioupata kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) umeiwezesha kupanua ununuzi wa parachichi kutoka kwa wakulima, kuongeza uwezo wa usindikaji wa mafuta ya parachichi na kuimarisha soko la zao hilo nchini.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, Mhasibu wa Eatfresh, Lightness Mariki, amesema kampuni hiyo inanunua parachichi kutoka mikoa mbalimbali inayozalisha zao hilo kwa wingi, ikiwemo Iringa, Njombe, Mbeya, Kigoma na Kagera.
“Kwa mwaka huu tumepata zaidi ya Sh milioni 700 kutoka TADB. Fedha hizi zimetuwezesha kuimarisha mradi wetu wa usindikaji wa mafuta ya parachichi, kuongeza uwezo wa kununua matunda kutoka kwa wakulima na kuboresha shughuli zote za uzalishaji,” amesema.

Amefafanua kuwa, kampuni hiyo inanunua aina mbalimbali za parachichi, hususan aina ya Hass, ambayo ina mahitaji makubwa katika soko la kimataifa kwa matumizi ya chakula na uzalishaji wa mafuta ya parachichi.
Ameeleza kuwa kampuni hununua mazao moja kwa moja kutoka kwa wakulima pamoja na kupitia wasambazaji, huku pia ikipeleka wataalamu mashambani kutoa mafunzo ya uzalishaji bora na namna ya kudhibiti changamoto zinazoweza kuathiri ubora wa matunda.

“Lengo letu ni kuhakikisha wakulima wanazalisha parachichi zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi. Tunawapa mafunzo ya utunzaji wa mashamba na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali ili waongeze tija,” amesema.
Ameongeza kuwa, ushiriki wa kampuni hiyo katika Maonesho ya Nanenane unalenga kuhamasisha Watanzania kuwekeza katika kilimo cha parachichi kutokana na fursa kubwa za soko na thamani ya zao hilo.
Aidha, amewataka wakulima kuchukulia Eatfresh kama soko la uhakika la mazao yao, akieleza kuwa kampuni itaendelea kupanua ununuzi wa parachichi kadri uzalishaji unavyoongezeka.
“Tunawaalika wakulima wote wanaolima parachichi kushirikiana nasi. Tunahitaji mazao yenye ubora na tutaendelea kuwa soko la uhakika kwa wakulima ili waongeze kipato chao na kuchangia ukuaji wa sekta ya kilimo,” amesema.
Ametoa shukrani kwa TADB kwa kuendelea kuiwezesha kampuni kupitia mikopo ya maendeleo, akisema hatua hiyo imeongeza uwezo wa kampuni kuwekeza katika uchakataji wa mazao na kuimarisha mnyororo wa thamani wa parachichi nchini.


