Na Mwandishi Wetu
MHITIMU wa mafunzo ya ufundi stadi kupitia VETA, Ernest Maranya, amebuni mashine inayosaidia kusindika mabaki ya mazao na vyakula kuwa chakula cha mifugo, ubunifu unaolenga kupunguza gharama za ufugaji, kuongeza tija ya uzalishaji na kuchangia utunzaji wa mazingira.
Akizungumza katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’ yanayoendelea jijini Dodoma, Maranya amesema baada ya kuhitimu mafunzo ya VETA mwaka 2017, alianza kujishughulisha na utengenezaji wa mashine mbalimbali katika karakana yake iliyopo Chanika, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.
Amesema amejikita katika kubuni na kutengeneza mashine zinazoongeza thamani ya mazao ya kilimo pamoja na kutoa suluhisho kwa changamoto zinazowakabili wakulima na wafugaji.

“Mashine tunazotengeneza zinasaidia kusindika mazao mbalimbali ya kilimo, lakini pia tumebuni mashine inayoweza kukata na kusaga mabaki ya mazao na vyakula ili kutengeneza chakula cha mifugo chenye ubora,” amesema Maranya.
Ameeleza kuwa mashine hiyo hutumia mabaki ya mazao na taka za vyakula zinazopatikana sokoni, ikiwemo mabaki ya viazi, ndizi, mboga na mazao mengine ambayo mara nyingi hutupwa, na kuyageuza kuwa chakula chenye virutubisho kwa ng’ombe, mbuzi, nguruwe, kuku na mifugo mingine.
Kwa mujibu wa Maranya, matumizi ya mashine hiyo yanapunguza utegemezi wa chakula cha mifugo kinachonunuliwa madukani, ambacho mara nyingi huwa na gharama kubwa kwa wafugaji.

“Wafugaji wengi wanakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za chakula cha mifugo. Kupitia teknolojia hii wanaweza kutumia malighafi zinazopatikana kwa urahisi kutengeneza chakula chenye ubora kwa gharama nafuu, hivyo kuongeza faida katika shughuli zao,” amesema.
Ameongeza kuwa matumizi ya lishe bora kwa mifugo huongeza uzalishaji wa maziwa, nyama na mayai, huku yakiboresha afya ya mifugo na kupunguza athari za baadhi ya magonjwa yanayosababishwa na lishe duni.
Mbali na kuongeza tija kwa wafugaji, amesema mashine hiyo pia inachangia uhifadhi wa mazingira kwa kupunguza taka zinazozalishwa katika masoko na maeneo ya biashara ambazo mara nyingi husababisha uchafuzi wa mazingira endapo hazitatumika ipasavyo.
Maranya amesema mashine hizo zinatengenezwa kulingana na mahitaji ya mteja, ambapo bei zinaanzia takribani Sh600,000 kwa mashine ndogo na kufikia zaidi ya Sh1.5 milioni kwa mashine zenye uwezo mkubwa wa uzalishaji.
Amewahimiza wakulima, wafugaji na wajasiriamali kutembelea banda la VETA katika Maonesho ya Nanenane ili kujionea teknolojia mbalimbali zinazobuniwa na wahitimu wa chuo hicho na kupata elimu kuhusu namna ubunifu wa ndani unavyoweza kuongeza thamani ya mazao, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza kipato.
Amesema matumizi ya teknolojia zinazobuniwa na Watanzania ni sehemu muhimu ya kuharakisha maendeleo ya sekta ya kilimo na mifugo pamoja na kuchochea uchumi wa viwanda nchini.


