Ziara ya Rais Samia Uturuki yafungua milango ya uwekezaji, biashara

Na Tatu Mohamed

ZIARA ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Uturuki na ushiriki wake katika Mkutano wa 31 wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), imefungua fursa mbalimbali za uwekezaji, biashara na ufadhili wa miradi ya maendeleo, huku Tanzania ikipata ahadi za kuimarisha sekta za kilimo, maji, nishati na mazingira.

Kupitia mazungumzo na viongozi wa mataifa mbalimbali, taasisi za fedha na washirika wa maendeleo, Tanzania imepata fursa ya kuwasilisha mahitaji yake ya maendeleo, kutafuta mitaji na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 15, 2026 kuhusu matokeo ya ziara hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, amesema ziara hiyo imekuwa na manufaa katika kufungua fursa za maendeleo, uwekezaji, biashara na uhifadhi wa mazingira.

Amesema katika mkutano huo Rais Samia alisisitiza umuhimu wa haki ya tabianchi, akieleza kuwa Afrika inachangia kwa kiwango kidogo katika uzalishaji wa hewa ukaa duniani, lakini inaendelea kukabiliwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi.

Machumu amesema Tanzania ina fursa kubwa katika biashara ya hewa ukaa, misitu, rasilimali za asili na nishati safi, hivyo uwekezaji katika maeneo hayo unapaswa kuzingatia maslahi ya jamii na kufanyika katika masoko yenye uwazi na haki.

Amesema kitovu cha mafunzo kuhusu mabadiliko ya tabianchi kinatarajiwa kujengwa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha ujuzi na uwezo wa vijana kukabiliana na changamoto za tabianchi barani Afrika.

Ameongeza kuwa Tanzania imepata fursa za uwekezaji katika biashara ya hewa ukaa kupitia taasisi za ndani, ikiwamo Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), ambavyo vimekutana na taasisi na kampuni kubwa za kimataifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Richard Muyungi, amesema mazungumzo yaliyofanyika wakati wa ziara hiyo yamefungua njia ya kupata ufadhili wa miradi ya maji na uwekezaji katika sekta ya kilimo.

Amesema Mfuko wa Kimataifa wa Tabianchi (GCF) umekubali kutoa fedha zilizobaki ili kukamilisha mradi wa maji katika maeneo ya Ziwa Victoria na Simiyu, unaokadiriwa kugharimu Dola za Marekani milioni 120.

Dkt. Muyungi amesema Tanzania pia imepata fursa ya uwekezaji wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 150 katika sekta ya kilimo, ikihusisha maeneo ya uzalishaji, usambazaji, viwanda, misitu na biashara ya hewa ukaa.

“Uwekezaji huo unalenga kuongeza uzalishaji, kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao na kufungua fursa za biashara kwa wakulima na wafanyabiashara nchini,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema Serikali imepata fursa ya kuimarisha ushirikiano na taasisi za kimataifa katika sekta ya nishati na mazingira, ikiwamo uwekezaji wa ziada katika miradi ya dola milioni 150 kwa ajili ya kuimarisha sekta ya kilimo na kukuza biashara ya hewa ukaa.

Akizungumzia ushirikiano katika Nishati, Waziri wa Nishati, Juma Homera, amesema Tanzania imepata fursa ya kushirikiana na nchi na taasisi mbalimbali katika kuimarisha matumizi ya nishati safi, hususan katika shule, vituo vya afya na maeneo ya uzalishaji.

Amesema Saudi Arabia ni miongoni mwa washirika wanaoshirikiana na Tanzania kuendeleza matumizi ya nishati safi, ikiwamo gesi asilia (LNG), ili kupunguza utegemezi wa nishati zinazochafua mazingira.

Aidha, amesema Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeidhinisha ufadhili wa majiko ya umeme kwa kaya 70,000, huku ufadhili wa majiko mengine 70,000 ukitarajiwa kutolewa hivi karibuni.

“Shirika la Kimataifa la Nishati Jadidifu (IRENA) pia linashirikiana na Tanzania kufadhili miradi ya kusambaza majiko, kuendeleza matumizi ya gesi asilia na kuongeza uwezo wa wataalamu katika teknolojia ya nishati jadidifu.

“Vilevile, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linashirikiana na Tanzania kuhamasisha matumizi ya teknolojia za nishati safi katika shule na vituo vya afya, ili kupunguza gharama za uendeshaji, kulinda afya na kuhifadhi mazingira,” amesema.

Amefafanua kuwa, mahitaji ya fedha kwa ajili ya kutekeleza hatua zilizoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC) ni Dola za Marekani milioni 19.3, ambapo tayari zimepatikana Dola milioni 7.3 na kiasi kinachohitajika kutafutwa ni Dola milioni 12.

Amesema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya uwekezaji katika nishati jadidifu na kuhamasisha matumizi ya magari yanayotumia umeme na gesi, yakiwamo CNG, LNG na LPG, ili kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Amesisitiza kuwa uwekezaji katika nishati unalenga kukuza uchumi, kupanua mtandao wa nishati na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe, amesema Rais Samia alitumia mkutano huo kutetea maslahi ya nchi zinazoendelea, hususan katika upatikanaji wa fedha za tabianchi, teknolojia na kujengewa uwezo.

Katika eneo la ufadhili wa tabianchi, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Serikali inaendelea kuratibu juhudi za kupata fedha kupitia mifuko ya kimataifa na taasisi za fedha, huku ikihamasisha matumizi ya mifumo ya ufadhili wa kijani, ikiwamo hati fungani za kijani.

Aliongeza kuwa Serikali inaangalia namna ya kutoa unafuu wa kodi kwa baadhi ya magari yanayotumia umeme na gesi ili kuhamasisha matumizi yake na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Kwa ujumla, matokeo ya ziara hiyo yanaonesha maeneo mbalimbali ambayo Tanzania inalenga kuyatumia kuimarisha uchumi, kuongeza uwekezaji, kupanua masoko ya bidhaa zake na kupata rasilimali za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

spot_img

Latest articles

WAZIRI HOMERA ASHIRIKI MIJADALA YA KIMATAIFA YA NISHATI COP31, AKUTANA NA WADAU WA MAENDELEO

📌azungumza na SEforALL na UpEnergy kujadili fursa za kuimarisha matumizi ha nishati safi ya...

Rukwa mbioni kunufaika na umeme wa Gridi ya Taifa baada ya kukamilika kwa Mradi wa TAZA

📌 Utekelezaji Mradi wa TAZA wafikia asilimia 95 📌 Ili kuukamilisha mradi kutakuwa na katizo...

Mradi wa Kurasini Logistics Park wakamilika kwa asilimia 90

Na Tatu Mohamed MRADI wa ujenzi wa Kurasini Logistics Park katika Bandari Kavu ya EPZA,...

KATIBU MKUU WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA ASISITIZA ULINZI WA BIASHARA ZA WAZAWA.

Na Mwandishi Wetu KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mhe.Balozi Waziri Rajab...

More like this

WAZIRI HOMERA ASHIRIKI MIJADALA YA KIMATAIFA YA NISHATI COP31, AKUTANA NA WADAU WA MAENDELEO

📌azungumza na SEforALL na UpEnergy kujadili fursa za kuimarisha matumizi ha nishati safi ya...

Rukwa mbioni kunufaika na umeme wa Gridi ya Taifa baada ya kukamilika kwa Mradi wa TAZA

📌 Utekelezaji Mradi wa TAZA wafikia asilimia 95 📌 Ili kuukamilisha mradi kutakuwa na katizo...

Mradi wa Kurasini Logistics Park wakamilika kwa asilimia 90

Na Tatu Mohamed MRADI wa ujenzi wa Kurasini Logistics Park katika Bandari Kavu ya EPZA,...