Mradi wa Kurasini Logistics Park wakamilika kwa asilimia 90

Na Tatu Mohamed

MRADI wa ujenzi wa Kurasini Logistics Park katika Bandari Kavu ya EPZA, umefikia asilimia 90 ya utekelezaji na unatarajiwa kuanza kutoa huduma Januari 2027, ukiwa na lengo la kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam na kuongeza uwezo wa kuhifadhi na kuhudumia makasha.

Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha miundombinu ya bandari, ambapo utakapokamilika utaongeza uwezo wa kuhifadhi makasha hadi 700,000 kwa mwaka, huku eneo la kwanza (Phase One) likiwa na uwezo wa kuhifadhi makasha 150,000 na eneo la pili likiwa na uwezo wa makasha 550,000.

Akizungumza leo Novemba 12, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema kukamilika kwake kutasaidia kuhamishia baadhi ya shughuli za ukaguzi wa makasha nje ya bandari, hatua itakayopunguza msongamano na kuongeza kasi ya upitishaji wa mizigo.

Amesema shughuli zitakazofanyika katika eneo hilo ni pamoja na uhakiki wa nyaraka (verification), uchunguzi wa makasha kwa kutumia mashine maalumu (scanning) pamoja na ukaguzi wa kimwili, ambazo kwa sasa zinafanyika ndani ya bandari.

Amefafanua kuwa, utaanza kwa makasha ya bidhaa zinazouzwa nje ya nchi (export), kabla ya kuhusisha makasha ya bidhaa zinazoingia nchini (import), hatua itakayosaidia kupunguza msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam.

“=Mradi huu ni sehemu ya manufaa ya uwekezaji unaofanyika bandarini ambapo mwekezaji anayetekeleza mradi huu pia amepewa dhamana ya kuendesha Kituo cha Kuhudumia Makasha namba mbili (Terminal 2),” ameeleza.

Hata hivyo, Profesa Mbarawa ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha barabara maalumu zinazoelekea katika eneo hilo zinakamilishwa kwa haraka ili kuwezesha mradi kuanza kutoa huduma kwa wakati uliopangwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus Abed, amesema bandari hiyo inatarajia kuhudumia zaidi ya makasha milioni 1.5 mwaka huu, ikilinganishwa na makasha milioni 1.3 yaliyohudumiwa mwaka jana.

Amesema ongezeko la shehena limeongeza mahitaji ya maeneo ya kuhifadhi makasha, hivyo kukamilika kwa Kurasini Logistics Park kutasaidia kupokea shehena zaidi na kupunguza msongamano unaosababishwa na shughuli za ukaguzi ndani ya bandari.

“Eneo hili litakuwa na mashine za kutosha za ukaguzi wa makasha (scanners), zitakazosaidia kuongeza kasi ya mtiririko wa shehena,” amesema.

Gallus amesema kwa mujibu wa mpango uliowekwa, eneo hilo litaanza kutumika Januari 2027 kama kituo cha kuhudumia makasha kupitia Bandari Kavu (ICD), kabla ya kuanza kutoa huduma kamili za upanuzi wa bandari (Port Extension) baada ya kuwasili kwa mashine za ukaguzi.

spot_img

Latest articles

Rukwa mbioni kunufaika na umeme wa Gridi ya Taifa baada ya kukamilika kwa Mradi wa TAZA

📌 Utekelezaji Mradi wa TAZA wafikia asilimia 95 📌 Ili kuukamilisha mradi kutakuwa na katizo...

WAZIRI HOMERA AMPONGEZA RAIS SAMIA KUONGOZA KWA VITENDO AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA BARANI AFRIKA

📌Ataja matumizi ya nishati safi kupanda kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia...

HAKIKISHENI MNAMBANA MKANDARASI ILI MRADI WA UMEME SONGEA – MASASI UKAMILIKE KWA WAKATI – MHE. NDEJEMBI

📌Akagua Mradi wa njia ya kusafirisha umeme Msongo wa Kv 220 Songea...

WATALII HIFADHI ZA TAIFA WAFIKIA MILIONI 1.5

Na Tatu Mohamed  IDADI ya watalii waliotembelea hifadhi za taifa nchini imeongezeka kutoka watalii 768,319...

More like this

Rukwa mbioni kunufaika na umeme wa Gridi ya Taifa baada ya kukamilika kwa Mradi wa TAZA

📌 Utekelezaji Mradi wa TAZA wafikia asilimia 95 📌 Ili kuukamilisha mradi kutakuwa na katizo...

WAZIRI HOMERA AMPONGEZA RAIS SAMIA KUONGOZA KWA VITENDO AJENDA YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA BARANI AFRIKA

📌Ataja matumizi ya nishati safi kupanda kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia...

HAKIKISHENI MNAMBANA MKANDARASI ILI MRADI WA UMEME SONGEA – MASASI UKAMILIKE KWA WAKATI – MHE. NDEJEMBI

📌Akagua Mradi wa njia ya kusafirisha umeme Msongo wa Kv 220 Songea...