Na Mwandishi Wetu
WAKAZI wa Mtaa wa Luhanga, Kata ya Kisukuru, Wilaya ya Ilala, wamepokea mabomba kutoka kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa ajili ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa maji utakaowanufaisha wananchi takribani 6,500 wa eneo hilo.
Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuboresha upatikanaji wa huduma ya majisafi na kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji inayochangiwa na ongezeko la idadi ya wakazi na mahitaji ya huduma hiyo.

Akizungumza baada ya kupokelewa kwa mabomba hayo, Semeni Adam, mkazi wa Mtaa wa Luhanga, ameipongeza DAWASA kwa kufikisha miundombinu hiyo, akisema hatua hiyo ni ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi unaotarajiwa kuboresha upatikanaji wa maji katika eneo hilo.
“Awali mtaa wetu huduma ya maji ilikuwa ya uhakika, lakini baada ya ongezeko la wakazi, huduma imekuwa ya changamoto kutokana na kuongezeka kwa matumizi,” amesema Semeni.
Kwa upande wake, Meneja wa DAWASA Mkoa wa Kihuduma Tabata, Gilbert Massawe, amesema Mamlaka imejipanga kuboresha na kubadilisha miundombinu ya maji katika Mtaa wa Luhanga ili iendane na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wananchi.

Ameeleza kuwa mabomba yenye kipenyo cha inchi nane na inchi sita tayari yamefikishwa katika eneo hilo kwa ajili ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi unaohusisha kipande cha mtandao wa maji chenye urefu wa zaidi ya kilomita 3.2.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Luhanga, Kata ya Kisukuru, Lukresia Msuya, ameishukuru Serikali kupitia DAWASA kwa hatua za haraka zilizochukuliwa katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa majisafi katika eneo hilo.

“Nitoe wito kwa wananchi wa Luhanga kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa mradi huu. Awali Serikali ilidhamiria kuchimba visima kusaidia upatikanaji wa maji, lakini kutokana na mazingira ya maeneo kutokuwa rafiki, imeamua kuja na mradi mbadala. Hivyo, wananchi tutunze mradi huu,” amesema Msuya.


