Na Tatu Mohamed
TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 10 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Shirika la Usafiri wa Majini la Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini (MOESNA), utakaowakutanisha takribani mawaziri 26 wanaosimamia masuala ya uchukuzi kutoka nchi wanachama, Oktoba 15, 2026, jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano huo unaolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya usafiri wa majini, kukuza biashara baina ya nchi za Afrika na kuongeza ushindani wa bara hilo katika masoko ya kimataifa.

Mkutano huo utafanyika wakati sekta ya usafiri wa majini barani Afrika ikiendelea kuwa na umuhimu katika kurahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria, kuimarisha biashara na kuchochea maendeleo ya uchumi wa nchi zenye mwambao wa bahari na zile zisizo na mwambao huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu maandalizi ya mkutano huo, Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema Tanzania inathamini nafasi yake ya kimkakati katika kuendeleza usafiri wa majini na kuimarisha muunganiko wa kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kusini na Kaskazini.
Kihenzile, aliyekuwa akitoa taarifa kwa niaba ya Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema mkutano huo utajadili mikakati ya kuboresha ushirikiano wa kikanda, kupanua wigo wa usafirishaji wa mizigo na abiria kwa njia ya meli na kuweka mazingira wezeshi ya kukuza biashara na uwekezaji.

Amesema miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni Itifaki ya Kikanda ya Usafirishaji wa Majini kati ya bandari za nchi wanachama na ushirikiano wa kampuni za meli za kikanda, hatua zinazolenga kurahisisha biashara, kuimarisha uratibu wa huduma za usafirishaji na kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo.
“Tanzania ina nafasi muhimu kutokana na jiografia yake katika Bahari ya Hindi na eneo la Maziwa Makuu, huku Bandari ya Dar es Salaam ikiwa lango muhimu la biashara kwa nchi jirani zikiwemo Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Burundi, Malawi na Uganda,” amesema.
Amefafanua kuwa, ushirikiano wa nchi wanachama ni muhimu katika kuhakikisha huduma za usafiri wa majini zinakuwa na ufanisi na kuchangia ukuaji wa biashara ya kikanda na kimataifa, hususan kwa nchi zinazotegemea bandari za mataifa jirani kufikisha bidhaa katika masoko mbalimbali.

Kihenzile amesema mkutano huo pia utajadili mpango wa kuanzisha Chuo Kikuu cha Kikanda cha Masuala ya Bahari (Regional Maritime University), kitakacholenga kuimarisha elimu, mafunzo, utafiti na ubunifu katika sekta ya usafiri wa majini.
Amesema mpango huo unalenga kuongeza idadi ya wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika sekta hiyo, kuboresha ubora wa mafunzo na kuimarisha matumizi ya pamoja ya miundombinu na teknolojia za elimu katika taasisi za nchi wanachama.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa MOESNA, Kassim Mpaata, amesema nchi wanachama zimekubaliana kushirikiana katika kugharamia ujenzi wa chuo hicho, huku Serikali ya Tanzania ikiongoza utekelezaji wa mpango huo.

Mpaata amesema baadhi ya nchi tayari zimeonesha utayari wa kuchangia mradi huo, ambao unalenga kujenga uwezo wa wataalamu watakaohudumia sekta ya usafiri wa majini katika ukanda huo.
Ameongeza kuwa mkutano huo utajadili pia Mpango Mkakati wa MOESNA wa miaka mitano kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 hadi 2030/31, utakaoweka dira ya utekelezaji wa vipaumbele vya shirika katika kuendeleza sekta ya usafiri wa majini.
Mkutano huo unatarajiwa kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama katika usalama wa majini, kuboresha huduma za usafirishaji na kutumia fursa zinazotokana na Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) kukuza biashara na uchumi wa bara hilo.


