Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Media Brains ikishirikiana na Shirika la Konrad Adenauer Stiftung (KAS) wameendesha mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Kagera na Geita jinsi ya kumudu uandishi wa kidijitali.
Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na KAS ni muendelezo wa progamu ya kuwajengea uwezo waandishi wa Tanzania katika kumudu uandishi wa habari wa kidijitali, yanazidi kujenga na kupanua wigo wa kuwafikia waandishi walioko pembezoni ili wawe na maarifa ya kumudu kazi zao katika zama hizi za uandishi wa kidijitali.
Wawezeshaji wa mafunzo hayo ambayo tayari yamekwisha kufanyika katika mikoa ya Manyara, Arusha, Singida, Dodoma na Iringa, ni waandishi waandamizi Absalom Kibanda na Jesse Kwayu, wote kutoka Kampuni ya Media Brains.


Akiwanoa waandishi hao mjini Bukoba, Kwayu aliwaambia kwamba miongoni mwa mambo makuu ya msingi kabisa ya kuzingatia katika uandishi wa zama za kidijitali ni kuhakiki kila habari inayofika mikononi mwao.
“Kwa sasa kuna habari nyingi sana zinasambaa katika mitandao ya kijamii. Habari hizi zinasukumwa kwa kasi kubwa. Waandishi nao wanajikuta wakikimbizana na muda ili kuwahi kusambaza habari hizi. Katika uharaka huo, wengi wameangukia katika mtego wa kusambaza taarifa feki na kujikuta katika matatizo makubwa,” alisema Kwayu.


Aliwaambia waandishi hao kwamba pamoja urahisi wa kukusanya habari na kuzisambaza hasa kutokana na msaada wa tekinolojia ya kidijitali inayowezeshwa na mfumo wa internet, waandishi wanapaswa kuwa macho zaidi ili kutokuwa sehemu ya usambazaji wa habari feki na ambazo zinalenga kuhadaa wasomaji na umma kwa ujumla wake. Mazingira haya yanafanya suala la kuhakiki wa kila habari inayosambazwa kuwa la umuhimu wa kipekee.
Naye Kibanda aliwakumbusha waandishi kuwa kwa sasa vyombo rasmi vya habari ni vya kidijitali kwa kuwa zama za wasomaji wengi kupata habari kupitia vyombo kama magazeti na runinga, zinazidi kupitwa na wakati. Aliwaleza kuwa mitandao ya kijamii ndiyo imeshika hatamu kwa sasa kwa sababu ya kuwa na kazi na kuwafikia watu wengi kwa wepesi, haraka na urahisi.
Kibanda aliwambia waandishi hao kuwa Tanzania na duniani kote kwa sasa, watu wanapata habari kwa haraka kutoka kwenye mitandao ya kijamii, ambayo kwa kiasi kikubwa imevunja urasimu wa kusambaza habari ambazo zamani ulihitaji mlolongo mrefu kabla ya kuwafikia wasomaji au wasikilizaji.



Aidha, aliwakumbusha waandishi kwamba mitandao ya kijamii imewezesha mawasiliano ya pande mbili kati ya jamii (wapokea habari) na waandishi wa habari kwani sasa kuna uwezekano wa wasomaji au wasikilizaji kutoa maoni yao juu ya habari zinazosambazwa. Hali hiyo alisema inajenga zaidi ushirika baina ya waandishi na wapokea habari zinazosambazwa.
Mafunzo haya yanawajenga waandishi wa habari kujua jinsi ya kumudu matumizi ya akili unde, ushiriki wa umma katika uandaaji na usambazaji wa habari na jinsi waandishi wanavyoweza kutumia mitandao ya kijamii kujitafutia kipato. Aidha, mafunzo hayo pia yanawajengea waandishi uelewa wa sheria zinazosimamia sekta ya habari nchini pamoja na tekinolojia ya mawasiliano kupitia mifumo ya kidijiti.


