CRDB YAZINDUA UGHAIBUNI LOAN KUSAIDIA WATANZANIA WALIOPATA AJIRA NJE YA NCHI

Na Mwandishi Wetu

BENKI ya CRDB imezindua rasmi huduma ya mkopo ya Ughaibuni yenye lengo la kuwawezesha Watanzania waliopata ajira nje ya nchi kugharamia maandalizi muhimu ya safari na hatimaye kufikia ajira walizopata.

Huduma hiyo imezinduliwa Leo Agosti 27, 2026 jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano kati ya CRDB, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) pamoja na mawakala binafsi wa ajira, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuondoa changamoto ya ukosefu wa fedha inayowafanya baadhi ya vijana kushindwa kuanza kazi licha ya kuwa tayari wamepata ajira.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, amesema serikali imebaini kuwa baadhi ya Watanzania wanaopata ajira nje ya nchi hushindwa kusafiri kutokana na kushindwa kumudu gharama za awali ikiwemo hati za kusafiria, vipimo vya afya, vibali na tiketi.

Amesema hali hiyo imeifanya serikali kushirikiana na CRDB na mawakala binafsi wa ajira kuanzisha huduma hiyo ili kuhakikisha changamoto ya kifedha haiwi sababu ya kijana kupoteza ajira aliyopata.

“Ughaibuni Loan si ruzuku wala msaada wa bure. Ni fursa ya kifedha iliyobuniwa mahsusi kuwawezesha Watanzania wenye ajira zilizothibitishwa kukamilisha maandalizi yao na kwenda kufanya kazi nje ya nchi,” amesema Munisi.

Ameongeza kuwa, serikali imeendelea kufungua masoko ya ajira nje ya nchi kupitia ushirikiano na mataifa mbalimbali, huku ikisisitiza ajira hizo ziwe salama, halali na zenye staha.

Kwa mujibu wa Munisi, tangu serikali irejeshe rasmi utaratibu wa kuwaunganisha Watanzania na fursa za ajira nje ya nchi mwaka 2022, jumla ya Watanzania 14,600 walikuwa wamepata ajira katika nchi mbalimbali hadi Juni 2026.

Amesema ajira hizo zinahusisha kada mbalimbali ikiwemo uuguzi, mifugo, uhandisi, ujenzi, uchimbaji madini, umeme, useremala, upishi, huduma za hoteli, udereva na kazi za majumbani.

Amebainisha kuwa, serikali pia imeendelea kufanya makubaliano na nchi mbalimbali kwa ajili ya kufungua masoko mapya ya ajira, huku ikiendelea na mazungumzo na mataifa mengine yenye mahitaji ya nguvu kazi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa CRDB, Pendason Philemon, amesema benki hiyo imetenga Sh bilioni 250 kwa kipindi cha miaka mitano kwa ajili ya kuwawezesha Watanzania wenye ajira nje ya nchi kukamilisha gharama za maandalizi ya safari.

Amesema mikopo hiyo itakuwa kati ya Sh 500,000 hadi Sh milioni 20, kulingana na mahitaji ya mwombaji, aina ya kazi na uwezo wa kurejesha mkopo.

“Mkopo huu unaweza kutumika kugharamia mahitaji mbalimbali ya awali kama hati ya kusafiria, visa, vipimo vya afya, tiketi, mafunzo ya lugha na utamaduni pamoja na mahitaji muhimu kabla ya kuanza kupokea mshahara,” amesema.

Amefafanua mwombaji anatakiwa kuwa na barua ya ajira, maelezo ya mahitaji ya safari, kitambulisho kinachotambulika pamoja na barua ya utambulisho kutoka kwa wakala wa ajira aliyesajiliwa.

“Mnufaika anatakiwa kuwa na akaunti ya CRDB itakayotumika kupokea fedha za mkopo pamoja na mshahara atakaolipwa na mwajiri wake akiwa nje ya nchi,” amesema.

Ameongeza kuwa, mkopo huo utalipwa ndani ya muda usiozidi miezi 24, huku mnufaika akipewa kipindi cha neema cha miezi miwili kabla ya kuanza marejesho.

Amesema CRDB imebuni huduma hiyo baada ya kubaini kuwa gharama za maandalizi ya safari, ambazo zinaweza kufikia kati ya Sh milioni tano na Sh milioni 20 kulingana na nchi na aina ya ajira, zimekuwa kikwazo kwa baadhi ya vijana.

Naye Mwakilishi wa wanufaika wa ajira za nje, Dickson Mbaga, ameishukuru serikali na CRDB kwa kuanzisha huduma hiyo, akisema imewasaidia vijana waliopata ajira kukabiliana na gharama za safari na visa ambazo hapo awali zilikuwa kikwazo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Wateja Binafsi wa CRDB, Stephan Adili, amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na serikali katika kubuni bidhaa za kifedha zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania, hususan vijana.

Amesema CRDB imekuwa ikiongoza katika kutoa huduma kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi na itaendelea kutumia uzoefu huo kuhakikisha fursa za ajira za kimataifa zinaambatana na huduma zinazowawezesha vijana kuzifikia.

spot_img

Latest articles

Ofisi ya Msajili wa Hazina kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma za China

Na Mwandishi Wetu OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) iko katika hatua za mwisho za...

Makamu wa Rais atangaza kujiuzulu

Makamu wa Rais wa Tanzania, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ametangaza kujiuzulu wadhifa wake kuanzia...

RAIS SAMIA AAGIZA WAKUU WA MIKOA KUJIANDAA NA UDHIBITI WA ATHARI ZA ELNINO

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,...

Rais Samia azindua Kituo cha kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,...

More like this

Ofisi ya Msajili wa Hazina kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma za China

Na Mwandishi Wetu OFISI ya Msajili wa Hazina (OTR) iko katika hatua za mwisho za...

Makamu wa Rais atangaza kujiuzulu

Makamu wa Rais wa Tanzania, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ametangaza kujiuzulu wadhifa wake kuanzia...

RAIS SAMIA AAGIZA WAKUU WA MIKOA KUJIANDAA NA UDHIBITI WA ATHARI ZA ELNINO

Na Mwandishi Wetu RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,...