Kabla ya kumsukuma Nchimbi, tukumbuke ya Kikwete vs Lowassa

KWENYE mitandao ya kijamii bado hakujatulia. Watunga riwaya na wabuni matusi dhidi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, bado wanasaga meno. Wana hasira kubwa. Wamefura.

Hawa walianza kidogo kidogo vita dhidi yake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bungeni, mitaani na kidogo ndani ya serikali. Kwa hasira kubwa, waendesha mapambano hawa nimewafananisha na simulizi ya waumini wa dini ya Kikristo kama inavyoelezwa katika kitabu chao cha imani, Bibilia. Kwamba kule Uyahudini Mwanamke mmoja (Herodia) alikitaka kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye sinia, kwa sababu hakutaka maonyo yake dhidi ya mwenendo wake usiofaa. Kwamba Mwanamke huyo angali akiwa ni mke wa mtu haikuwa sahihi kuishi na Mfalme Herode.

Siku ya siku ikafika Mwanamke huyo akapata upenyo, kupitia kwa binti yake ambaye Mfalme Herode alimtaka achague zawadi baada ya kumfurahisha mbele ya waliokuwa karamuni naye. Binti akaenda kwa mamaye kuuliza achague zawadi gani. Mama akajua saa imefika, ya kumwondoa mbaya wake aliyekuwa anamzuia kuishi na Mfalme.

Mwanamke huyo alimweleza binti yake aende kwa Mfame Herode kuomba kichwa cha Yohana Mbatizaji kwenye kombe. Mfalme alihuzunika juu ya ombi hilo, lakini kwa viapo vyake na kulinda heshima mbele ya wafalme wengine, aliagiza kichwa cha Yohana Mbatizaji kikatwe na binti akapewa kama zawadi katika kombe naye akakipeleka kwa mamaye.

Kwa kadri siku zinavyosonga ndivyo wenye hasira dhidi ya Makamu wa Rais wanavyojidhihirisha. Wanatunga mashitaka mengi ya kuumbaumba dhidi yake. Katika ufinyangaji wa mashitaka haya mbinu nyingi zinatumika ili kujenga taswira mbaya ya Makamu wa Rais.  Kwamba ni kiongozi aliyepoteza sifa ya kukalia kiti cha Makamu wa Rais. Kwamba anajitenga na serikali, kwamba anahujumu serikali anayopaswa kumsaidia Rais kuisimamia ili isonge mbele. Mambo ni mengi katika madai haya.

Mitandaoni, kwenye vikao rasmi, ajenda inasukumwa. Kwa ushawishi mkubwa pengine wenye uwezeshwaji mkubwa wa fedha, kampeni inapigwa kwamba Makamu wa Rais amepoteza sifa ya kuwa kiongozi, hivyo wanataka kichwa chake. Kichwa kikatwe kama cha Yohana Mbatizaji.

Hali hii kwa wengine wanaweza kuchukulia poa. Kwamba ni ugomvi tu wa hovyo. Kwamba ni upepo tu utapita. Yawezekana kweli ni mambo mepesi. Hata hivyo, tujiulize ni kwa jinsi gani kiongozi mkuu namba mbili baada ya Rais wa Jamhuri wa Muungano kichwa chake kinatafutwa kwa mbinu hizi chafu? Hawa wanaotafuta shingo ya Makamu wa Rais wanataka kupata nini?

Nitafafanua kidogo. Hawa wanaotafuta kichwa cha Makamu wa Rais ni watu wenye hasira kali. Hawataki maonyo, hawataki kusikia sauti na wito wa neno HAKI. Hawataki kusikia maridhiano, hawataki kusikia Katiba Mpya, hawataki kusikia kauli zozote za kutaka kila Mtanzania atafute kupatana na mwenzake, kila mwenye dukuduku asikilizwe, kwamba Watanzania hawana sababu ya kuiparaganyisha nchi yao. Kwamba kila mtu awajibike kuheshimu Katiba kufuata sheria na kanuni za kuendesha nchi. Kwamba tuache ubabe katika nchi! Haya ndiyo Makamu wa Rais amekuwa akihamasisha kila apatapo fursa ya kuhutubia.

Lugha hizi kwa wakumbatia uhafidhina; watu wanaoamini katika ubabe na kuumiza wengine – hasa kumwaga damu, ni matusi kwao. Ni sawa na kauli ya Yohana Mbatizaji dhidi ya Herode na Herodia kwamba mahusiano yao hayakuwa sahihi, ilikuwa ni kufuru kupora mke wa mtu, pia kufuru mke wa mtu kuishi na mwanamume mwingine. Hasira iliwaka dhidi ya Yohana kwa kuwaonya dhidi ya uovu wao.

Vivyo hivyo, ndivyo Makamu wa Rais anawekwa kwenye kilengeo. Kisa, anataka mwelekeo mwema, maelewano, ushirika, hatua za maana kujenga Tanzania ya HAKI, amani na upendo. Amekufuru. Ni lazima watafute kichwa chake.

Mwaka 2005 Rais Jakaya Kikwete alishinda urais kwa kishindo. Akaunda baraza la mawaziri, atamteua Edward Lowassa kuwa Waziri Mkuu wake. Wapo watu walinuna. Kwa nini Lowassa awe Waziri Mkuu. Kwa nini aonekane anafanya kazi kwa kasi kubwa? Kwa nini ni yeye tu kila mahali, kwa nini, kwa nini na kwa nini Lowassa. Zengwe likasukwa. Kwamba Lowassa anamhujumu Rais, kwamba anatamba sana, kwamba nyuma ya pazia anautaka urais, anataka kumpindua bosi wake, Rais Kikwete.

Zengwe likapikwa, likaiva, kisha likaanza kupakuliwa, mwisho wa yote hata Mkuu akaona yawezekana ni kweli. Kilichotokea baada ya hapo ni Lowassa kujiuzulu nafasi ya Waziri Mkuu. Alifikia uamuzi huo kwa kile kilichodaiwa ni kashfa ya Richmond ambayo kimsingi haikuwapo.  Leo dunia inajua kwamba kilichowatenganisha Lowassa na Rais Kikwete ni zengwe lililopikwa mpaka likaiva na kupakuliwa. Gharama ya zengwe lile limegharimu taifa hili mambo mengi.

Zengwe lile ndilo baadaye lilikuja kuwa zimwi. Ndilo chimbuko la kuzorota kwa hali ya demokrasia tunayoshuhudia nchini leo. Ndilo chimbuko la kuwa na aina ya uchaguzi mkuu tulioona mwaka 2020 na mwaka 2025. Ni chimbuko la tabu yote ya kisiasa tunayopitia leo kama taifa.

Sijui kama zengwe dhidi ya Makamu wa Rais litafika wapi. Sijui ni kwa kiwango gani wasuka zengwe wa safari hii wataendelea kutumbukiza nchi hii katika shida za kisiasa. Ila kama taifa tunapaswa kukumbuka kuwa utaratibu wa kulea watu wenye historia ya kutesa, kuumiza na kupora, watu wasioamini katika utawala wa sheria, watu wasioamini katika maridhiano, ni wa hatari dhidi ya ustawi wa taifa letu.

Leo Tanzania inasotwa kidole kwa yaliyotokea Oktoba 29,2025. Tumeaibika kama taifa, mbele ya waungwana wote duniani, mbele ya jumuiya ya kimataifa. Katikati ya hali hii ngumu, wanaibuka watu wanaoanzisha zengwe lisilotabirika mwisho wake ni upi.

Tujifunze kwa machungu ya zengwe la Herodia dhidi ya Yohana Mbatizaji; tuombe Mungu tusimpate Herode wetu leo atakayepokea na kukubali zengwe hili, kesho ya taifa hili itakuwa mbaya kuliko leo. Tukumbuke kuwa bado zimwi la maafa ya Oktoba 29, 2025, limetuganda, tusitafute jingine.

spot_img

Latest articles

Ni Yanga tena ubingwa Ngao ya Jamii

Na Mwandishi Wetu Nyota mpya  wa Yanga, Albert Kangwanda amewapa raha mashabiki wa timu hiyo...

ZOEZI LA UVUTAJI NYAYA AWAMU YA PILI ENEO LA KIKOMBO NA MKONZE KATIKA MRADI WA CHALINZE–DODOMA KUANZA KESHO

📌TANESCO yasema baadhi ya Mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya...

SOKO BUBU LA MADINI LAGUNDULIWA JIJINI DAR ES SALAAM

▪️Watuhumiwa 14 wakamatwa na tuhuma za utoroshaji madini ▪️Waigeuza nyumba ya kupanga kama soko ▪️Waziri Mavunde...

Msajili wa Hazina ateta na Rais wa Benki ya Biashara na Maendeleo

Na Mwandishi Wetu MSAJILI wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais...

More like this

Ni Yanga tena ubingwa Ngao ya Jamii

Na Mwandishi Wetu Nyota mpya  wa Yanga, Albert Kangwanda amewapa raha mashabiki wa timu hiyo...

ZOEZI LA UVUTAJI NYAYA AWAMU YA PILI ENEO LA KIKOMBO NA MKONZE KATIKA MRADI WA CHALINZE–DODOMA KUANZA KESHO

📌TANESCO yasema baadhi ya Mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya...

SOKO BUBU LA MADINI LAGUNDULIWA JIJINI DAR ES SALAAM

▪️Watuhumiwa 14 wakamatwa na tuhuma za utoroshaji madini ▪️Waigeuza nyumba ya kupanga kama soko ▪️Waziri Mavunde...