TADB yaendelea kuwa nguzo muhimu katika kufadhili mapinduzi ya kilimo

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendelea kuwa chombo muhimu cha Serikali katika kufadhili maendeleo ya sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, huku akiitaka kuongeza uwezo wake wa kifedha ili kuwafikia wakulima, wafugaji na wavuvi wengi zaidi.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima ‘Nanenane’, Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema TADB imeendelea kutekeleza wajibu wake wa kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wawekezaji mbalimbali, lakini mahitaji ya huduma hizo yanaendelea kuongezeka, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza mtaji wa benki hiyo.

Amesema kuimarishwa kwa benki hiyo kutasaidia kuongeza uwekezaji katika sekta za uzalishaji, kuharakisha mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi, kuongeza tija na uzalishaji, pamoja na kuimarisha uchumi wa taifa.

“Ili kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa mazao na kuhakikisha usalama wa chakula nchini, ni lazima TADB iendelee kuimarishwa kifedha ili iweze kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wakulima na wadau wengine wa sekta ya kilimo,” amesema.

Ameongeza kuwa, Serikali haiwezi kutegemea ruzuku pekee kila mwaka kuendeleza sekta ya kilimo, hivyo taasisi za kifedha kama TADB zina jukumu kubwa la kuhakikisha mitaji inapatikana kwa wakati kwa ajili ya kuchochea uzalishaji.

Aidha, ametaka benki hiyo kuongeza ufadhili wa ununuzi wa mbolea, pembejeo, zana za kisasa za kilimo pamoja na miradi ya kuongeza thamani ya mazao ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.

Pia ameiagiza TADB kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI kuwekeza katika miundombinu ya baada ya mavuno, hususan ujenzi wa maghala ya kuhifadhi mazao.

Amesema uwekezaji huo utaimarisha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na kuwawezesha wakulima kupata mikopo kwa kutumia mazao yao kama dhamana, hatua itakayowaongezea uwezo wa kusubiri bei nzuri ya mazao badala ya kuyauza mara baada ya mavuno.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imeendelea kufadhili miradi ya kimkakati inayochochea ukuaji wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Amesema zaidi ya shilingi bilioni 700 zimetolewa kufadhili miradi ya umwagiliaji nchini, huku benki hiyo pia ikifadhili uzalishaji wa kahawa kupitia vyama vya ushirika vya Kagera na Kigoma pamoja na mradi wa kisasa wa ufugaji na uchakataji wa samaki uliopo Bagamoyo unaotumia teknolojia kutoka Misri.

Nyabundege amesema uwekezaji huo umechangia kuongeza uzalishaji, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje, kuokoa fedha za kigeni, kuongeza ajira na kuimarisha mchango wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

spot_img

Latest articles

BRELA yatumia Nanenane kuhamasisha urasimishaji wa biashara

Na Mwandishi Wetu WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa wito kwa wakulima...

MD TWANGE AWATAKA WANASHERIA WA TANESCO KUENDELEA KUSIMAMIA MAADILI NA TAALUMA

📌 Afungua Jukwaa la Wanasheria wa TANESCO jijini Mwanza 📌 Awasisitiza kutoa ushauri wa kisheria...

MRADI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME WA MSONGO WA KILOVOLTI 400 CHALINZE–DODOMA MBIONI KUKAMILIKA

📌 Wafika asilimia 94 ya utekelezaji wake 📌 Kazi za uvutaji waya kwenye mradi kusababisha...

UMEME JUA KISHAPU AWAMU YA PILI KUIONGEZEA TANZANIA MEGAWATI 100 ZA NISHATI JADIDIFU

📌Waziri Ndejembi ashuhudia utiaji saini, asema ni alama ya miradi ya kielelezo nchini 📌Mradi utakuwa...

More like this

BRELA yatumia Nanenane kuhamasisha urasimishaji wa biashara

Na Mwandishi Wetu WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umetoa wito kwa wakulima...

MD TWANGE AWATAKA WANASHERIA WA TANESCO KUENDELEA KUSIMAMIA MAADILI NA TAALUMA

📌 Afungua Jukwaa la Wanasheria wa TANESCO jijini Mwanza 📌 Awasisitiza kutoa ushauri wa kisheria...

MRADI WA NJIA YA KUSAFIRISHA UMEME WA MSONGO WA KILOVOLTI 400 CHALINZE–DODOMA MBIONI KUKAMILIKA

📌 Wafika asilimia 94 ya utekelezaji wake 📌 Kazi za uvutaji waya kwenye mradi kusababisha...