Aibu: Ukaburu waibuka Baraza la Wawakilishi

MSIMU wa siasa za masimango na kubaguana umerejea tena na kushika kasi. Safari hii vyombo vya juu kabisa vya uwakilishi wa wananchi vimekuwa ndiyo jukwaa mahususi kwa ajili ya kusukuma siasa za kuonyeshana jinsi ambavyo ni vigumu kwa Watanzania kupikika chungu kimoja. Siasa za msimu huu zinasukumwa kuonyesha kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania japo kuwa ni nchi moja, bado watu wake hawana uhuru, haki na fursa za kupata huduma na haki mbalimbali sawasawa kila mahali katika mipaka ya nchi hii.

Ngoma ya safari hii inapigwa kwa madaha yote. Imejielekeza katika mambo mawili. Huduma za afya na fursa za ajira. Ndani ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar viongozi wawili wenye wadhifa wa uwaziri, bila kumung’unya maneno, Naibu Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh alieleza isivyo halali wala kufaa kwa watu kutoka Tanzania Bara kupata fursa za ajira akieleza hizi ni za Wazanzibari, ana mkakati wa kuzipoka.

Naye Dk. Saada Mkuya anayekaimu nafasi ya Waziri wa Afya, alieleza isivyowezekana kwa watu kutoka Tanzania Bara kunufaika na Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar (ZHSF).

Wataalam wa mawasiliano wanafahamu kwamba katika mazungumzo tani (tone) hubeba maana halisi ya kusudio la ujumbe kuliko hata maana halisi ya maneno yenyewe. Tani huonyesha hisia za mzungumzaji zilizojificha ndani kabisa ambazo hazitamkiki kwa maneno. Namna ya kujieleza na mtazamo wa mzungumzaji huakisi dhahiri malengo yaliyojificha ndani yake.

Kwa kifupi, hisia zilizoonyeshwa na mawaziri hao wawili, pia wakiwa wameingia katika mjadala huu baada ya kuibuliwa kwa hoja hizo na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuwasilisha ujumbe muhimu juu ya mtazamo wa baadhi ya viongozi kuhusu Muungano wa Tanzania ambao ulizaliwa Aprili 26, 1964 yaani miaka 62 iliyopita.

Kauli za kuuchoka Muungano siyo mpya. Zimekuwako miaka mingi, aghalab wahusika wakuu wa kauli hizi ni watu wenye nafasi katika safu za uongozi. Wamekuwako baadhi ya wabunge kutoka Tanzania Bara ambao nao wameonyesha hisia zao za kuuchoka Muungano. Hawa wamekuwa wakitoa kauli ama za kuubeza Muungano wenyewe au hata kubeza watu kutoka Zanzibar.

Vivyo hivyo, kutoka upande wa Zanzibar (wahafidhina wengi wakikataa kutaja kuwa Zanzibar ni Tanzania Visiwani), nako kumekuwa na kauli tata. Zikiitaja Tanzania Bara kama mkoloni aliyeikalia Zanzibar kwa mabavu. Wakiamua nani awe kiongozi wao hata kama umma unataka kinyume chake.

Kwa bahati njema, kila kauli hizi zilipotolewa waliibuka watu wenye hekima na busara katika safu za uongozi wa kisiasa na serikalini na kusafisha kiwingu kilichochafuka. Miongoni mwa kumbukumbu kubwa ya kihistoria ni ile ya kundi la Wabunge wa G55 wakitaka kuanzishwa kwa serikali ya Tanganyika ndani ya mfumo wa Muungano. Pamoja na wabunge hao kufanikiwa kulishawishi Bunge mwaka 1993 mpaka kupata azimio la Bunge la kuitaka serikali kuanzisha mchakato wa kuundwa kwa serikali ya Tanganyika, hoja yao ilikuja kuuawa. Pengine ni nguvu, ushawishi, na uhodari wa Mwalimu Nyerere ndivyo vilizima azimio hilo kupitia mchakato wa Chama Cha Mapinduzi ambao mwishowe ulilifanya Bunge lenyewe kutengua azimio lake.

Mara nyingi kauli za kupalilia hisia za Kitanganyika au za Kizanzibari zimekuwa zikitumiwa kama gia ya kutafuta uhalali wa kisiasa. Wapo wanaodhani kwamba juhudi hizi zitasaidia kutatua matatizo ya kweli na ya msingi ya wananchi, wakati ukweli halisi ni kinyume chake.

Kauli hizi zinafanana moja kwa moja na kauli ambazo kwa kitambo sasa raia wa nchi ya Afrika Kusini wamekuwa wakizitoa dhidi ya wageni kutoka mataifa ya Afrika. Kwamba kule Afrika Kusini hali ya kuzorota kwa uchumi, kuadimika kwa fursa za ajira na kipato kidogo kwa wananchi wa kawaida, kunafungamanishwa na uwepo kwa wageni kutoka mataifa ya Afrika. Siyo mataifa mengine. Siyo Asia wala Ulaya. Hapana. Kutoka Afrika hata kama baadhi ya hao Waafrika wameanzisha biashara halali zikakua na kuajiri mamia ya raia wazawa wa Afrika Kusini.

Ni tani (tone) ile ile ya Afrika Kusini ndiyo mawaziri hawa wawili ndani ya Bazara la Wawakilishi wameiwasilisha. Kwamba matatizo ya Wazanzibari ya huduma duni/finyu za afya na ukosefu wa ajira, yamesababishwa na watu kutoka Bara. Dawa ni nini kuwafukuza! Kuwanyang’anya hizo ajira. Kuwazuia huduma za afya!

Viongozi hawa wameonyesha kiwango cha chini kabisa cha tafakari. Wameshindwa kutambua kuwa tatizo kubwa linalokabili taifa hili, bila kujali ni Watanganyika au Wazanzibari ni uchumi mdogo. Ni huduma za afya isiyotosheleza mahitaji na kwa ubora unaokidhi haja; aidha ni fursa chache za ajira ambazo asilani hazifanani na wimbi kubwa la nguvu kazi inayohaha usiku na mchana kusaka fursa hizo. Iwe ni Tanzania Bara au Zanzibar. Ukosefu wa ajira nchini kwa miongo kadhaa sasa kunatajwa kuwa ni miongoni mwa bomu kubwa linalotishia amani nchini. Ukosefu wa ajira ni bomu linalosubiri kulipuka wakati wowote.

Mawaziri hawa wawili kama ilivyo kwa wawakilishi walioibua hoja hii tenge, wanajua nini kinapaswa kufanywa. Kama ajira hakuna au hazitoshi Zanzibar, dawa si kuwinda Wabara, bali kukuza ajira. Kukuza uwekezaji, kuvutia mitaji kutoka nje, kuondoa kodi kero ili iwe rahisi watu kuanzisha biashara zitakazoongeza fursa za ajira.

Kama bajeti ya bima ya afya ni finyu, dawa ni kukuza uchumi, ili kila mtu afikiwe na huduma hiyo. Kuwafukuza Wabara au kuwakatalia huduma, hakusaidii kutatua tatizo la bajeti finyu ya afya.

Ni hakika, ubaguzi hauna mipaka, na hauna desturi ya kufika mwisho. Watu hubaguana kwa hisia tu kuwa huyu siyo wa kwetu, lakini ukweli wa mambo ni huu, kila mtu ni wa kipekee, hafanani na mwingine. Hatufanani rangi, hatufanani kwa wajihi, hatufanani kwa kila kitu. Ila sote tu binadamu, ubinadamu wetu ndio unatuweka pamoja kama viumbe wenye kujua jema na baya.

Tabia ya kutafuta uhalali wa kisiasa kwa kisingizio cha kutetea watu kwa kuangalia asili yao, au ukanda au eneo ni tabia ya kujivika kilemba cha ubaguzi. Tabia hii haiwezi kuvusha jamii, achilia mbali taifa. Ni kwa mustakabali huu, wote wanaohubiri ubara na uvisiwani wajue tu kuwa wao ni makaburu tu wa zama za sasa. Mwisho wao ni kuvuruga jamii. Ubora wa kiongozi hupimwa jinsi anavyofanikisha kutatua matatizo ya jamii – ajira, afya, elimu, barabara nk.  huku akidumisha ustawi wa taifa na siyo kulivunjavunja kwa matarajio ya umaarufu wa kitambo kidogo tu. Tuache ukaburu hautaleta ajira wala huduma bora za afya.

spot_img

Latest articles

WANANCHI MSIHOFU KUTUMIA NISHATI YA UMEME KATIKA VYOMBO VYA USAFIRI -MD TWANGE

📌Asema TANESCO inajenga vituo vya kuchajia vyombo hivyo nchi nzima 📌Aeleza mpango wa kusambaza majiko...

BODI YA DAWASA YAINGIA MTAANI KUKAGUA UPATIKANAJI WA MAJI

Na Mwandishi Wetu BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira...

ELIMU YA VIPIMO YAWAVUTIA WANANCHI, WAAHIDI KUWA MABALOZI WA KUJITOLEA

Na Mwandishi Wetu Dodoma – “Sasa najua ni nini ninapaswa kuangalia ninapojaza mafuta, kununua...

More like this

WANANCHI MSIHOFU KUTUMIA NISHATI YA UMEME KATIKA VYOMBO VYA USAFIRI -MD TWANGE

📌Asema TANESCO inajenga vituo vya kuchajia vyombo hivyo nchi nzima 📌Aeleza mpango wa kusambaza majiko...

BODI YA DAWASA YAINGIA MTAANI KUKAGUA UPATIKANAJI WA MAJI

Na Mwandishi Wetu BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira...