KATIKA siku za hivi karibuni nimemkumbuka sana Profesa Seithy Chachage (08.01.1955 – 09.07.2006). Huyu alikuwa Mwalimu wa wengi. Alifundisha wengi, mimi ni miongoni mwa watu waliopita kwenye mikono ya Profesa Chachage. Apumzike kwa amani. Fikra zangu kwa Mwalimu huyu nguli wa masuala la sosholojia zimenikumbusha dhana aliyoijenga akiita kwa Kimombo ‘imbecilisation of society’ najaribu kuitafsiri kwa Kiswahili kisicho rasmi kuwani ubwegezaji wa jamii.
Dhana hii ya imbecilisation ni pana, lakini inabeba umuhimu wa kipekee kwa jamii ya watu wanaotaka kusonga mbele. Inabeba uzito wa kipekee kwa watu wanaochukia ulegevu, uovu, kujikomba na zaidi ya yote kuabudu uongo na kujipendekeza. Jamii inayoruhusu kutumbukizwa katika mfumo unaojenga hali ya ubwegezaji, aghalab kujikomboa kutoka katika madhila ya umasikini, wizi wa mali ya umma, rushwa na kila aina ya uovu unaodumaza jamii, inakuwa ni mtihani mgumu ambao hakika haiwezi kufaulu. Si rahisi kufaulu kwa sababu imbecilisation na tafakuri ya kina au fikra tunduizi ni vitu visivyoweza kutangamana. Haviwezi kustawi pamoja asilani.
Profesa Chachage alibainisha sifa kuu za mfumo unaotukuza imbecilisation kuwa ni jamii inayopokea taarifa za vyombo vya habari bila kuwa na uchambuzi wowote wa kina kuhusu taarifa hizo kwa ustawi wake. Kwamba ni watu wanaopokea taarifa bila kuzichambua ili kuzijengea maana katika maisha yao ya kila siku. Jamii ya namna hiyo, aghalab hulishwa taarifa za burudani, propaganda, au taarifa za juu juu ambazo hazina tafakuri ya kina. Nia ikiwa ni kuwafubaza kimaono.
Jamii hiyo pia hujikuta ikitukuza na kujenga mfumo wa elimu unaolenga kukariri na siyo kufungua bongo za wanafunzi ili wajenge uwezo wa kudadisi na kuhoji; kadhalika nyanja za kisiasa hudhibitiwa na kuhodhiwa na mamlaka za dola. Haki ya uhuru wa kisiasa hugeuzwa kuwa kitu cha kuomba ruhusa, kuwekewa mipaka isiyoeleweka kwa ujumla wake, nia kuu ikiwa ni kuvunja uthubutu wowote wa jamii wa kuhoji mamlaka. Katika hali kama hiyo, kukandamiza mijadala au upinzani kunaweza kuzaa jamii inayotii bila kuuliza maswali. Jamii inayoshangilia na kusifu kila kitu hustawi na ukasuku hutamalaki.
Mbinu nyingine ambayo hukuza imbecilisation ni kukuza hoja nyepesi nyepesi, kuondoa watu kwenye mijadala mizito yenye mantiki kwa kuibua vitu vyepesi – vichekesho, burudani (michezo, muziki, sherehe nk) ili kujenga na kuimarisha mfumo unaokuza ulegevu wa kiakili.
Dhana ya Profesa Chachage ilikuwa ni kengele ya kuamsha jamii itambue kuwa kwa kujiruhusu kutofikiri ni kufungua mlango wa jamii kudanganywa kirahisi; kujengwa kwa utamaduni wa kuwako kwa mijadala ya umma ambayo haina kina. Vitu nyeti vyenye maslahi mapana ya jamii kujadiliwa kijuu juu na kubwa ya yote ni wananchi kupoteza kabisa uwezo wa kuwawajibisha viongozi wa umma. Meza kupinduliwa – wananchi kuwaogopa viongozi wao.
Kwa maelezo machache kabisa dhana hii ya imbecilisation inatuelekeza kwenye fikra kwamba mifumo inaweza kuunda mazingira yanayochochea ulegevu wa kiakili, hata kwa watu wenye uwezo mkubwa wa kufikiri wanajiruhusu kugeuka kuwa kasuku.
Tangu Tume ya kuchunguza matukio ya Oktoba 29, 2025 iliyoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande iwasilishe ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Aprili 23, mwaka huu, zipo dalili za dhahiri kabisa kwamba kuna juhudi ya wazi kabisa ya kusukuma jamii katika dhana ya imbecilisation, tena kwa kasi kubwa.
Mathalan, ukifuatilia mijadala ya baadhi ya wanasiasa, ambao kwa hakika sina hakika kama wanajua wanachokijua kuhusu ripoti hii, unapata picha kama kuna kazi wametumwa. Hawa wamepewa kazi ya kupita huko na huko kuisifia ripoti ya Tume kana kwamba imemaliza kila kitu. Wanapita kutaka kuaminisha wananchi kwamba kazi iliyofanywa na Tume imefikisha ukingoni matatizo yote ambayo yalisababisha kadhia na fazaa ambayo taifa hili lilishuhudia kati ya Oktoba 29 hadi Novemba 3, 2025.
Kwa hakika kazi iliyoko mbele baada ya Tume kuwasilisha kazi yake ni nyeti na tete zaidi labda kuliko kabla ya ripoti. Kwa mfano, vidonda vya walioumizwa na matukio haya vitapona vipi? Je, kwa waliopoteza ndugu ni aina gani ya fidia itasaidia kupoza machungu? Pale alipokufa tegemeo la familia, ni fidia gani itatumika kuziba pengo? Au wale waliopoteza mali zao na kubakia katika hali ya ufukara wa kipato, wanarejeshwa vipi? Je, wale walipoteza viungo kuwapa viungo vya bandia itatosha? Je, waliopata madhara ya kisaikolojia kama wale walioona ndugu au wazazi au watoto wakiuawa mbele yao kikatili, hawa watafanywa nini? Na je, mifumo yetu ya uchaguzi, ya ulinzi wa raia na mali zao, unakwenda kutengenezwa vipi? Ni kama ndiyo kwanza tunaamka asubuhi, siku inaanza!
Ninajua kwa hakika Tume imetoa mapendekezo kadhaa katika hayo maswali hapo juu, lakini tatizo kubwa ninaloliona ni utayari wa taifa kuingia katika mjadala wa kweli, wa wazi wa kutafuta maridhiano kama ambavyo imekuwa ikielezwa bila kutumbukia kwenye dhana ya imbecilisation. Ukitafakari bila kina unaweza kudhani ninawahisha gari la kukokotwa na farasi kabla ya farasi. Kwamba nina haraka sana, nisubiri. Lakini wakati watu wakitamani sana subira, kuna vitu vingi ambavyo Tume iliviepuka kabisa kuvisemea.
Kwa mfano, nani asiyekumbuka kwamba amri ya kutokutembea baada ya saa 12 jioni iliyotangazwa na Inspeka Jenerali wa Polisi, Camillus Wambura awali ililenga mkoa wa Dar es Salaam tu? Na je, ni lini ilitangazwa kwamba ilikuwa ni ya nchi nzima? Na ni lini iligeuka kuwa ni ya saa 24 kiasi cha kuathiri kabisa shughuli za raia kiasi cha hata wagonjwa kushindwa kufikia huduma za matibabu?
Tume imejiepusha sana kutaja watu ama kwa nafasi au kwa majina katika janga lote hili. Kikubwa imejigemeza kwenye maelekezo ya adidu rejea, ingawa ilikuwa na adidu za “Uchunguzi wa Vurugu: Kuchunguza matukio yote ya uvunjifu wa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi wa tarehe 29 Oktoba 2025; Kubaini Wahusika: Kufichua wahusika waliohusika na kuratibu vurugu hizo, ikiwa ni pamoja na vifo na uharibifu wa mali. Imekwepa sana njia ya kuwajibisha wahusika. Imependekeza hatua za uchunguzi wa kijinai ufuate.
Wakati umma ukisubiri hatua za uchunguzi wa kijinai uanze, hivi, Tume ililenga kuaminisha Watanzania kuwa hatua ya uchunguzi wa kijinai unafuata wakati wahusika wakuu wa matendo yale ya mauaji ya kikatili ya Oktoba 29 hadi Novemba 3, 2025 bado wako ofisini? Kuna kokote jamii inajiruhusu kuingia katika mjadala huu wa kutaka uwajibikaji? Kuna mahali mijadala hii sasa inafanyika kuhamasisha uwajibikaji? Kwa nini, je, tunasukumwa kwenye ile dhana alieleza Marehemu Profesa Seth Chachage imbecilisation of society – ubwegeshaji wa jamii?


