Na Jesse Kwayu
KATIKA mfumo wa utawala ambao chimbuko la madaraka ya dola ni wananchi, kama ilivyo Tanzania kwa mujibu wa katiba ibara ya nane, ni jambo la busara kwa kiongozi yeyote kusumbuka kutokana na hisia za wananchi.
Kusumbuka huko kuna maana nyingi. Kwamba kiongozi anakuwa na utambuzi kuwa hakika ‘mabosi’ wake ni wananchi. Kwa maana hiyo, hata kwa nadharia tu, anapaswa kuwaza wananchi wanasema nini kuhusu mwenendo wake, utendaji wake na kwa ujumla utumishi wake.
Anasumbuka kwa sababu anajua chimbuko la madaraka ni wananchi. Ni hao wanaomfuatilia juu ya utumishi wake na kuwajibika kwake. Tawala zote duniani zinazopata ridhaa ya uongozi kupitia sanduku la kura hujisumbua sana na kujua na kutafakari kile kinachosemwa na kutarajiwa na wananchi.
Yawezekana kwa tawala za kimabavu kama za kijeshi au za kifalme kutokusumbuka na hisia za wananchi. Hii ni kwa sababu chimbuko la madaraka yao siyo ridhaa ya umma. Ama ni mabavu au urithi tu ambao hata hivyo historia yake inatokana na mfumo mabavu pia.
Jumamosi iliyopita Watanzania walimuaga na kumzika aliyekuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Tanzania Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo (81), alifariki dunia Februari 19, 2026 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete jijini Dar es Salaam. Misa ya maziko ya Kardinali Pengo ilikuwa ni tukio la kitaifa na kimataifa kwa sababu ya nafasi ya kiongozi huyo wa kiroho.
Kwa maana hiyo, Misa hiyo ilihudhuriwa na watu wa kila aina. Walikuwapo waumini wa Kanisa Katoliki – Makardinali, Maaskofu, Mapadri, Mashemasi, Watawa, Maburuda na viongozi wa ngazi zote za kanisa hilo. Pia waliokuwapo waombolezaji wa madhahebu mengine ya dini ya Kikristo na hata wasiyo Wakristo kama Waislamu. Walikuwapo viongozi wakuu wa serikali waliopo madarakani na waliostaafu. Kwa kifupi tukio la mazishi ya Kardinali Pengo lilikuwa ni tukio kubwa kwa vigezo vyovyote.
Katika misa hiyo, kuna jambo kubwa ambalo siyo la kiluturijia lilitokea. Hili ni lile la utambulisho wa watu mashuhuri waliokuwa wamehudhuria misa hiyo, na mwitiko wa waombolezaji waliokuwa mahali pale. Tukio hili lilitokea wakati Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu (TEC), Dk. Charles Kitima, ambaye alikuwa mshehereshaji alipokuwa akiwatambulisha au kuwatambua viongozi mashuhuri waliohudhuria misa hiyo. Mwitikio wa waombolezaji uliowasilisha ujumbe muhimu dhabiti kuhusu hisia za wananchi kwa viongozi wao wa sasa na waliostaafu.
Kilichotokea katika uwanja wa utawala na sayansi ya siasa, ni kama kura ya maoni (opinion poll). Kila jina la kiongozi aliyehudhuria misa hiyo lilipotajwa, kulikuwa na mambo mawili yaliyotokea, ama kushangiliwa au ukimya kutoka kwa waombolezaji. Kwa waliokuwa wanafuatilia misa hiyo mubashara kupitia vyombo vya habari na hata waliokuwapo eneo la tukio waliona jinsi wananchi walivyoonyesha hisia zao.
Viongozi wote wastaafu waliokuwako mahali pale majina yao yalipotajwa, walishangiliwa na waombolezaji kwa makofi na vigelegele. Hawa ni pamoja Makamu wa Rais Mstaafu Dk. Philip Mpango; Mawaziri Wakuu Wastaafu- Kasim Majaliwa Majaliwa, Jaji Joseph Warioba na Mizengo Pinda pamoja na viongozi wengine. Hawa walishangiliwa kwa makofi na vigelegele kila walipotambulishwa.
Kwa viongozi walioko madarakani, Makamu wa Rais Dk. Emmanuel Nchimbi, kulikuwa na ushangiliaji hafifu, ingawa baadaye alipozungumza Dk. Nchimbi hotuba yake ilionekana kuwagusa vilivyo waombolezaji kiasi cha kuibua mashangilio. Mashangilio hayo, kwa haki yalikuwa ni kukubali na kuitikia kwamba Dk. Nchimbi ni kiongozi anayesikia na kujua hisia za wananchi. Alizungumza kukerwa kwake na chuki na magomvi ya kisiasa baina ya vyama vya siasa, pia akieleza kuwa mashangilio waliyopata viongozi wastaafu katika hadhara ile ilikuwa ni ishara ya wananchi kuwakubali kutokana na utumishi wao mzuri, akiamini na walioko madarakani watajitahidi kufanya vema kama waliostaafu ili nao wapate kushangiliwa vivyo. Ama kwa Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba, naye ni kama mashangilio hayakusikika kabisa.
Punde tu baada ya tukio hilo, mitandao ya kijamii ilichafuka kwa vipande vya taarifa vikielezea uhaba wa mashangilio kwa viongozi walioko madarakani. Kusambaa kwa vipande hivyo vya sehemu ya misa ya mazishi, hatimaye Jumatatu wiki hii kulimuibua Dk. Mwigulu akiwa ziarani mkoani Manyara ambako alijikuta akijibizana na mitandao ya kijamii kwamba: “Wanalinganisha sijui makofi makofi mimi sikilizeni, mimi sijaletwa kwa ajili ya kupendwa. Akinipenda mke wangu inatosha.” Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo bila shaka akijibu wale wote waliokuwa wanajadili tukio la kwenye misa ya mazishi ya Kardinali Pengo. Kwa maneno mengine Dk. Mwigulu alikuwa anaonyesha hisia zake juu ya tukio lile la kukosa makofi na vigelegele.
Hakika Dk. Mwigulu ana haki ya kutoa maoni yake juu chochote kilichotokea. Tena ana haki ya kukasirika au kufurahi jambo lolote likimtokea kama mtu mwingine yoyote. Ni haki yake kutoa hisia zake kama alivyofanya akiwa ziarani Manyara.
Hata hivyo, Dk. Mwigulu pamoja na haki hizo, anasahau jambo moja. Kwamba yeye ni kiongozi wa kisiasa anayetokana na ridhaa ya wananchi kupitia sanduku la kura. Kama kweli sanduku la kura ndilo linampa fursa na haki ya kuwa kiongozi kulingana na ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, basi chochote kinachozungumzwa na wananchi juu ya kiongozi wao siyo jambo la kupuuzwa. Siyo la kupuuzwa kwa sababu wananchi ndiyo ‘mabosi’. Ingelikuwa Dk. Mwigulu ni kiongozi aliyeingia madarakani kwa njia ya mapinduzi kijeshi au kwa mfumo wa kifalme, wala kusingelikuwa na sababu ya watu kujadili ama kushangiliwa kwake au vinginevyo. Kisa, kwa kuwa madaraka yake yasingelitegemea uamuzi wa wananchi.
Yale makofi ambayo Dk. Mwingulu anayakejeli na kuyaita ‘makofi makofi’ ni kielelezo cha kura ya imani, ni kielelezo cha hisia za ndani kabisa za wananchi juu yake kama kiongozi wao. Kwamba wanamuona kama kiongozi wa namna gani? Kwamba wanamkubali kwa kiasi gani? Mtu kupigiwa makofi ni ishara na kielelezo cha kuheshimika, kukubalika na kutambuliwa vema kwa hao wanaopiga makofi. Ni mwitikio kwa watu wanavyokuona. Ni ishara ya kukubaliana nawe ama kwa unayosema, unayotenda, ni kielelezo cha kukuamini.
Kama Dk. Mwigulu Lameck Nchemba hasumbuliwi na makofi ya wananchi, wapiga kura, kama hisia za wananchi kwake, je, huyu ni kiongozi wa sampuli gani? Ni vema Dk. Mwigulu akajua tu makofi yale ni sawa na kura ya imani kwake, ajitafakari. Kujaribu kuonyesha kwamba hasumbuliwi na makofi, au anathibitisha kinyume chake anapoteza fursa ya kurekebisha mambo?


