Na Mwandishi Wetu
MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Raymond Mndolwa, ametoa pole kwa waandishi wa habari waliopata ajali ya gari mkoani Iringa walipokuwa wakirejea nyumbani wakitokea kuripoti Maadhimisho ya Miaka 49 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mndolwa, akiwa ameambatana na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa NIRC, Mariam Mziwanda, alifika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa na kuwatembelea waandishi hao wa habari, ambapo aliwajulia hali na kuwapa pole kwa niaba ya taasisi hiyo.

Ajali hiyo ilitokea jana, Februari 5, 2026, katika Kata ya Idodi, Wilaya ya Iringa Vijijini.
Gari lililohusika katika ajali hiyo lilikuwa limewabeba Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Iringa, Joseph Nzala Lyata, pamoja na waandishi wa habari akiwemo Frank Leonard, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa na mwandishi wa magazeti ya Habari Leo na Daily News.

Waandishi wengine waliopata ajali hiyo ni pamoja na Zuhura Zukheriwa wa Abood TV, Denis Mlowe wa blogu ya Fullshangwe, Clemence Sanga wa Channel Ten pamoja na Herieth Mola wa Mkombozi Online TV.



