Na Mwandishi Wetu
MAKAMU wa Rais wa Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi amesema serikali imejizatiti kuhakikisha sekta ya uchukuzi inaimarika ili kuliweka Taifa kwenye nafasi nzuri ya ushindani wa kibiashara, kuongeza mapato ya fedha za kigeni na kukuza mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Jengo la Viongozi Mashuhuri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema pamoja na ujenzi wa jengo hilo, serikali imejipanga kikamilifu kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kisekta kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (2025).
Makamu wa Rais amesisitiza kwamba, serikali itaendelea kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali katika viwanja vya ndege, huduma za usafiri wa barabara, usafiri majini na usafiri kwa njia ya reli.

Halikadhalika amesema, serikali itaendelea na uboreshaji wa huduma za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kwa lengo kuboresha usafiri wa ndani, kuunganisha Tanzania na nchi nyingine, kupunguza gharama za usafirishaji na kuimarisha uchumi wa Tanzania na biashara za kimataifa.
Amesema ili kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji, serikali imedhamiria kuunganisha huduma za Sekta ya Uchukuzi, kama vile uunganishaji wa huduma za viwanja vya ndege, usafiri wa barabara, maji na reli. Mathalan, mradi wa kimkakati unaoendelea wa ujenzi wa barabara za Mwendokasi (BRT) kati ya eneo la Posta na Gongo la Mboto utaunganishwa na kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere ili kurahisisha huduma za usafiri katika jiji la Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa hatua za utekelezaji zinaendelea ili kuhakikisha huduma za reli zinaunganishwa na viwanja vya ndege vya kimataifa, hususan Julius Nyerere, Msalato na Kilimanjaro.


