Wakatoliki feki wamechafua hali ya hewa, aibu hii anabeba nani?

TAHARUKI kubwa imeibuka nchini. Unaweza kuiona ukichungulia kwenye mitandao ya kijamii. Imesababishwa na akili ndogo sana iliyotunga ‘igizo’ feki la kwenda kuwalalamikia viongozi wawili wa Kanisa Katoliki nchini, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi na Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima, kwenye Ubalozi wa Vatican jijini Dar es Salaam.

Kundi la watu wanaojiita waumini wa Kanisa Katoliki nchini, wakidai wako 120, kutoka mkoa wa Dar es Salaam na mikoa mingine, Jumatatu wiki hii walizuka mbele ya ubalozi huo wakiwa na waraka wao wa kuwalalamikia viongozi hao wawili kwa Mkuu wa Kanisa Papa Leo wa XIV. Baada ya kufika ubalozini, walifanya mkutano na waandishi wa habari kueleza kilio chao.

Wanawatuhumu viongozi hao wawili kwamba wanaingiza siasa katika Kanisa, wanawadharau waumini na kwamba wanataka warejeshwe kwenye mstari. Kwamba wasigeuze madhabau kuwa jukwaa la kisiasa, wasiwadharau na kuwatukana waumini wanaotafuta uwajibikaji kutoka kwao.

‘Igizo’ hili limewaumbua waliolibuni kwa kiwango cha kushangaza. Ni igizo linalofanana kwa karibu sana na jingine ambalo lilipata kuratibiwa na aliyekuwa mwanasiasa machachari Hiza Tambwe, (ilikuwa Aprili 2011) ambaye alikuwa mwanasiasa nguli wa Chama cha Wananchi (CUF) kisha akahama kambi na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupewa kazi katika kitengo cha Uenezi.

Hiza, sasa marehemu, Mungu ampe pumziko la amani, alikusanya watoto wadogo akawajaza kwenye ukumbi wa Karimjee wakati wa mchakato wa katiba mpya, wakati huo Tume ya Katiba ikikusanya maoni ya wananchi kuhusu katiba mpya. Hiza alichukuwa hatua hiyo ili kujaza ukumbi ikiwa ni mbinu ya kuzuia watu wengine wasio wanaCCM kuingia ukumbini. Alifanya hivyo baada ya jana yake, kuona ukumbi ukiwa umejaa watu waliokuwa na msimamo tofauti na wa chama chake. Akibishana na watu hao, aliwaambia kuwa ana uwezo wa kujaza watu wake kwenye ukumbi huo. Na kweli kesho yake aliwajaza watoto. Igizo la kijinga kabisa!

Aliwakusanya watoto hao kutoka maeneo tofauti jijini Dar es Saalam. Waliamshwa alfajiri wakasafirishwa kwa mabasi na kujazwa ukumbini. Ilipofika majira ya saa tano asubuhi, wengi walikuwa wanasinzia na wala hawakujua nini kilikuwa kinaendelea kwenye ukumbi huo. Hiza alifanya hivyo ili kuziba nafasi ya watu wenye hoja kuwa ukumbini kuwasilisha maoni yao kwa Tume. Baadaye watoto hao ambao baadhi waliozungumza na waandishi wa habari walikiri kuwa walikuwa wamekusanywa na kuletwa ukumbini kwa ujira wa Sh. 5,000/=

Sasa igizo la Jumatatu wiki hii ni kama limerudia yale aliyopata kufanya Hiza. Usanii na gilba kubwa.

Katika igizo jipya, waandaaji wamekosea mambo mengi mno. Kwanza wameshindwa kutambua kuwa Kanisa Katoliki lina utamaduni wake ambao unafanana karibu duniani kote. Utamaduni huu ni pamoja na uvaaji, urejeaji wa majina ya viongozi wao, uimbaji, usomaji wa neno, kwa ujumla utaratibu mzima wa kiimani wa Kanisa Katoliki upo wazi kwa waumini wake. Waigizaji walifeli yote haya.

Waigizaji hawa walikosea kiasi cha kujitwika fedheha kubwa kwao na kwa wale waliowatuma. Mosi, uvaaji wa Wakatoliki Feki ulionyesha dhahiri kuwa hawajui maadili ya uvaaji wa waumini wa Kanisa hilo lenye wafuasi wengi zaidi ulimwenguni kote. Mbili, aliyeteuliwa kusoma pingamizi lao kwenda kwa Papa Leo XIV alishindwa hata kutamka jina la kiongozi mkuu wa Kanisa hilo, hakuweza kusoma vitabu vilivyoko kwenye Bibilia aliyokuwa anafanyia rejea. Kwa mfano anataja kitabu cha Wakorintho kwa kujichanganya. Mara anasema Wakorintho wa 11 hadi 12; mara Wakorintho wa 13 mpaka wa 10. Usomaji wa vitabu vya Bibilia wa namna hii unaonyesha dhahiri kuwa msomaji hajui anachokirejea. Bibilia inaorodhesha vitabu vya Wakorintho ambavyo ni Nyaraka za Mtume Paulo kama Wakorintho wa Kwanza (1 Wakorintho) na Wakorintho wa Pili (2 Wakorintho) na milango yake kadhaa.

Kwa maana hiyo, kwa kigezo tu cha kumtambua msomaji kama kweli ni muumini wa Kanisa hilo, alianguka vibaya. Hajui kitabu chake ambacho ni nguzo kuu ya imani yake (Mkristo). Huyu anaonekana kama mtu aliyeokotwa barabarani ili kutumwa kazi hiyo haramu ya kuchafua kanisa na viongozi wake.

Ukiacha suala la kujua kitabu chake cha imani, mzungumzaji huyo pia hana kina chochote cha hicho alichojaribu kuuhadaa umma kwamba anakijua. Kwanza, anaonekana kutokujua alichokuwa anakisoma kilikuwa ni nini hasa. Anasema ‘wanawasilisha pentenstation’ badala ya Petition. Hapa mtu unajiuliza, yaani waandaaji wa pingamizi (petition) hawakuwa na watu wenye uwezo wa kusoma kwa ufasaha, wenye kina cha hicho wanachokilalamikia? Ni anguko la Babiloni.

Yaani hawa watu wamefanikiwa kukusanya watu huko na huko, wamewaandamanisha (bila kuguswa na polisi ambao wametanda kila kona katika jiji la Dar es Salaam kwa sasa) wakafika mpaka Ubalozi wa Vatican, wakapeleka pingamizi lao; wakaandaa ukumbi wa mkutano hotelini, wakalipia, wakajipanga meza kuu kuzungumza, lakini wasemaji wao wepesi mno. Uandaaji huu unaonyesha ni watu wanaojua wanataka kufanya nini. Lakini uwasilisha hoja zao mbele ya waandishi wa habari, umeonyesha kiwango cha juu sana cha utupu (ineptness). Wazungumzaji wawili waliojitokeza mbele ya kamera katika mkutano wa waandishi wa habari, wanaonekana kukosa kabisa kina cha hicho wanachokilalamikia. Hawa ni kama watu waliotumwa kazi.

Sasa turudi kwenye chimbuko hasa la kadhia hii. Kinachosumbua katika kadhia hii ni msimamo wa Kanisa Katoliki nchini juu ya mambo makuu yafuatayo, mosi, kukataa na kulaani kwa nguvu zote kukithiri kwa ukiukaji wa haki za wananchi ambao wamekuwa wakiuawa, kutekwa na kuteswa. Kanisa limesimama imara wakati wote likikemea matukio haya ambayo sasa yameota mizizi nchini. Limetaka uwajibikaji.

Pili, TEC limelaani vikali mauaji baada ya uchaguzi na matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji kufuatia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, likiyataja kuwa ni “mauaji ya kikatili na yasiyo ya kibinadamu” na uovu mkubwa. Wamesisitiza kuwa maandamano ni njia halali ya kueleza malalamiko pale mazungumzo yanaposhindikana, na kwamba nguvu ya dola haipaswi kutumika kuwaadhibu waandamanaji wa amani.

Imetoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi huru kuhusu vurugu na vifo vilivyohusiana na uchaguzi, ukihusisha wadau wa ndani na wa kimataifa, kama vile asasi za kiraia, wataalamu wa haki za binadamu, na taasisi za kidini — si tume ya serikali pekee.

Maaskofu wanataka maafisa wa vyombo vya usalama na wengine waliotenda kinyume cha sheria wawajibishwe, na kwamba majina ya watu walioko kizuizini yatangazwe hadharani. Kuachiwa huru bila masharti wale waliokamatwa bila haki, na kuheshimiwa kwa haki za kikatiba.

TEC imeweka wazi wasiwasi wake kuhusu kudhoofika kwa demokrasia ya kweli katika namna viongozi wanavyopatikana, ikibainisha kuwa chaguzi “zinakosa ushindani wa haki, ukweli, uwazi, uhuru na uhalali” — hoja ambazo zimekuwa zikisisitizwa mara kwa mara tangu mwaka 2016.

Kanisa limekataza mapadre, watawa na wanataaluma (seminaristi) Katoliki kujihusisha na siasa za vyama au kampeni za kisiasa, au kujitambulisha hadharani na chama chochote cha siasa. Badala yake, wanahimizwa kuwaongoza waumini kupiga kura kwa dhamiri iliyoelimika vizuri, inayojengwa juu ya ukweli, haki na mafundisho ya kijamii ya Kanisa.

Msimamo huu wa Kanisa umeudhi wengi akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan ambaye aliituhumu TEC kwa kutoa matamko mengi. Alisema wametoa matamko manane na aliwananga kwamba wanajiona kwamba wao ni dhehebu la dini lenye hadhi kuliko mengine. Yawezekana hasira za mkuu wa nchi dhidi ya TEC huenda zimechangia wapambe kutunga igizo hili ambalo limewafedhehesha wote.

spot_img

Latest articles

Tuna deni la kusimamia miradi na kusikiloza kero za wananchi ili kuleta Maendeleo ya kweli: Salome

Na Mwandishi Wetu NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema viongozi wana deni kubwa...

2025 mwaka wa mageuzi na matokeo katika mashirika ya umma

Na Mwandishi Wetu MWAKA 2025 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Ofisi ya Msajili wa...

Mukwala atua Zanzibar, Simba ikiivaa Azam kesho Mapinduzi Cup

Na Winfrida Mtoi WAKATI Simba kitarajia kukabiliana na Azam FC kesho katika mchezo wa nusu...

Serikali yawekeza zaidi ya Sh. Bilioni 280 kuimarisha upatikanaji umeme Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano...

More like this

Tuna deni la kusimamia miradi na kusikiloza kero za wananchi ili kuleta Maendeleo ya kweli: Salome

Na Mwandishi Wetu NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema viongozi wana deni kubwa...

2025 mwaka wa mageuzi na matokeo katika mashirika ya umma

Na Mwandishi Wetu MWAKA 2025 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwa Ofisi ya Msajili wa...

Mukwala atua Zanzibar, Simba ikiivaa Azam kesho Mapinduzi Cup

Na Winfrida Mtoi WAKATI Simba kitarajia kukabiliana na Azam FC kesho katika mchezo wa nusu...