Na Mwandishi Wetu
BENKI ya CRDB, imemkabidhi Deo Ferdinand Mlawa na wenzake watano zawadi wazojishindia katika droo kubwa ya kampeni kubwa inayohamasisha matumizi ya huduma za benki kupitia simu ya mkononi kwa mwaka 2025.
Mlawa wa Mikocheni jijini Dar es Salaam alitangazwa mshindi wa jumla wa kampeni ya Benki ni Simbanking ya Benki ya CRDB Desemba 17 mwezi huu na Desemba 30, 2025 akakabidhiwa gari jipya aina ya Toyota Harrier Anaconda.
“Najisikia furaha sana. Hii ni zawadi ya kufungia mwaka 2025 na kuuanza mwaka mpya 2026 kwa staili yake. Naishukuru sana Benki ya CRDB kwa zawadi hii kubwa. Niwakumbushe Watanzania wenzangu kuendelea kutumia huduma za Simbanking kwani huwezijua lini utatangazwa mshindi,” amesema Mlawa.

Licha ya Mlawa mwingine aliyekabidhiwa zawadi ni Desderius Magombola kutoka Meru mkoani Arusha aliyejishindia gari aina ya Toyota IST New Model.
Kutokana na dharura aliyokuwa nayo iliyomzuia kusafiri, zawadi yake ilipokelewa na Isis Nyanda katika hafla fupi iliyofanyika Dar Village jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi zawadi hizo, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul amesema magari hayo yote mawili yamekatiwa bima kubwa kutoka CRDB Insurance Compani ambayo ni kampuni tanzu ya Benki ya CRDB pamoja na kujazwa mafuta ‘full tank’ tayari kwa kuingia barabarani.

“Siku zote Benki ya CRDB tunatekeleza ahadi yetu. Leo ni siku ya aina yake kukabidhi Toyota Harrier Anaconda kaka yangu Deo Ferdinand Mlawa kwa bahati hii aliyoipata kutokana na matumizi makubwa ya huduma zetu za Simbanking. Zawadi zetu zilikuwa wazi kwa kila mteja wetu,” amesema Bonaventura.

Kwa mwaka 2025 Benki ya CRDB imetoa zawadi ya magari manne aina ya Toyota IST New Model kwa washindi waliokuwa wanapatikana katika kila robo mwaka.
Kwenye droo ya mwisho ambayo ndio kubwa zaidi, gari la tano limetolewa kwa mshindi wa jumla pamoja na wanafunzi wawili wa chuo kikuu kupata ufadhili wa kulipiwa ada na wengine wawili kujishindia simu ya kisasa aina ya iPhone 17 Promax.
Wanafunzi waliopata ufadhili wa kulipiwa ada ni Happiness Justine Chacha anayesoma Chuo cha Usafiri wa Majini (DMI) na John Simon Soka kutoka Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) jijini Dar es Salaam huku Maimartha Haji Seleman wa Keko jijini Dar es Salaam na Felix Geofrey Sembwana naye wa jijini Dar es Salaam wakishinda iPhone 17 Promax.

Akizungumzia zawadi aliyoipata, Happiness amesema: “Napata mkopo wa Bodi (ya Mikopo ya Elimu ya Juu) lakini ufadhili huu wa Benki ya CRDB umeniongezea hamasa ya kusoma kwa bidii zaidi. Naziomba taasisinyingine nazo ziwe zinatoa zawadi kama hizi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu wanapotangaza matumizi ya bidhaa au huduma zao.”
Kufungwa kwa kampeni hii iliyodumu kwa mwaka mzima, Bonaventura amesema kunafungua milango ya maandalizi ya msimu mpya mwaka 2026 hivyo kuwataka wateja wa Benki ya CRDB kuendelea kutumia huduma za Simbanking kwani katika msimu huu mpya kutakuwa na zawadi nyingi tofauti zitakazotolewa kwa wateja watakaoshinda.

“Kwa wale ambao si wateja wetu ni wakati wao sasa kujiunga nasi kwani ukishakuwa na akaunti tu na ukatumia huduma za Simbanking kupitia simu yako ya mkononi iwe ya kisasa au kiswaswadu, unajiweka kwenye nafasi ya kuibuka mshindi,” amesema Bonaventura.


