Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo la Peramiho, Jenista Joakim Mhagama (58) amefariki dunia leo Disemba 11, 2025 jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Spika wa Bunge Mussa Azan Zungu katika kikao cha Bunge, imethibitisha kuondokewa na mbunge huyo aliyehudumu kwa zaidi ya miaka 20.
“Kwa masikitiko makubwa, naomba kutangaza kifo cha Mbunge wa Peramiho Mheshimiwa Jenista Mhagama kilichotokea leo 11 Desemba, 2025 jijini Dodoma. Natoa pole kwa waheshimiwa Wabunge wote, familia ya marehemu, ndugu, jamaa na wananchi wa Jimbo la Peramiho. Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu,” ameeleza Spika Zungu kupitia taarifa hiyo.
Mhagama alizaliwa Juni 23, 1967, na safari yake ya uongozi ilianza kupitia elimu ambapo alimaliza masomo ya sekondari katika Shule ya Wasichana Peramiho mwaka 1985.
Baadaye alipata Stashahada ya Ualimu katika Chuo cha Ualimu Korogwe mwaka 1989 na kufanya kazi ya ualimu kwa miaka sita kuanzia 1991 hadi 1997, akifundisha katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Songea na baadaye katika VETA Songea hadi mwaka 2000.
Mhagama hata baada ya kuingia kwenye siasa, aliendeleza elimu yake na mwaka 2004 alipata Diploma ya Kimataifa ya Uongozi na Utawala kutoka Cambridge International College.Safari yake ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilianza mwaka 1987, kupitia jumuiya za vijana na wanawake.
Mwaka 2000, aliteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kwa mara ya kwanza. Miaka mitano baadaye, alifanikiwa kushinda kwenye kura za maoni za CCM dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Simon Mbilinyi, na kupata nafasi ya kugombea Jimbo la Peramiho. Aliendelea kushinda Jimbo la Peramiho katika chaguzi zilizofuata, ikiwemo uchaguzi wa mwaka 2015 ambapo alipata kura 32,057 dhidi ya 11,462 za mpinzani wake.
Mhagama aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuanzia Januari 2014 hadi Januari 2015, kisha akateuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Uratibu na Bunge. Katika serikali ya Rais John Magufuli, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu kuanzia Desemba 2015 hadi Januari 2022.
Mwaka 2022 alihamishiwa Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora na mwaka 2023 alirudi Ofisi ya Waziri Mkuu kusimamia Sera na Bunge.
Nafasi yake ya mwisho serikalini ilikuwa Waziri wa Afya, wadhifa aliokabidhiwa Agosti 2024.


