Na Winfrida Mtoi
CHUO cha Maendeleo ya Michezo Malya kinaendesha mafunzo maalum kwa wakufunzi wa gym na makocha wa viungo ili kuwaongezea ujuzi na kufahamu mbinu mbalimbali zitakazowasaidia kufanya kazi yao kwa weledi.
Mafunzo hayo yaliyoanza Novemba 24,2025 yanayoendelea katika ukumbi wa Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es Salaam, yanahusisha washiriki 30 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania.
Akizungumzia lengo la kutoa mafunzo hayo, Makamu wa Mwenyekiti wa Chuo hicho, Salumu Mtumbuka amesema ni kutokana na kukua kwa michezo na maeneo ya gym ndiyo watu wengi wanapenda kwenda kufanya mazoezi.

“Tumeona tutoe mafunzo haya kwa makocha wa viungo wa michezo yote na wataalamu wa gmy ambao wanafundisha watu kufanya mazoezi, hii itasaidia kutoa elimu yao kitaalamu zaidi.
“Tutaendelea kutoa mafunzo ya michezo kwa lengo ya kupata wataalum ambao wataleta maendeleo katika Taifa letu, pia nina imani elimu hii ambayo washiriki wanapatiwa itaongeza nguvu katika mazoezi yao, “ameeleza.
Kwa upande wake mshiriki wa mafunzo hayo, Peter Pingo amesema elimu aliyoipata itamuongezea ubora katika kazi yake ya kufundisha mazoezi gym.
“Naishukuru Serikali chini ya Chuo ya Malya ambao wametoa kozi hii ambayo itatuongezea weledi na ufanisi wa kazi yetu, nina imani nitakuwa bora zaidi katika kuhakikisha watu wanapata mazoezi yenye viwango vizuri, ” ameeleza.


