Na Mwandishi Wetu
KOCHA Mkuu wa Yanga, Pedro Concalves amesema falsafa yake katika mechi ya kesho Novemba 22,2025 dhidi ya AS FAR Rabat ni kutawala mchezo, huku akifahamu wapinzani wake wamejipanga sana eneo la kiungo.
Yanga inatarajia kukutana na FAR Rabat ya Morocco ikiwa ni mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika utakaopigwa kwenye dimba la New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, Pedro amesema kila mtu anawasema kuwa wamepangwa kundi la kifo kwa sababu ya timu kubwa nne. “Lakini kama unataka kuwa bingwa lazima ushindane na mabingwa,”
“Falsafa yangu ni kuutawala mchezo kwa gharama yoyote ile. Nahitaji wachezaji wangu wajitume sana. Malengo yangu makubwa ni timu kucheza vizuri. Matokeo ya mchezo wa kesho naamini yatatokana na namna ambavyo tutacheza vizuri. Mimi naamini matokeo mazuri yanatokana na namna ambavyo tutaongeza utulivu na umakini,” amesema kocha huyo Rais wa Ureno.

Ameeleza kuwa bado wapo kwenye mchakato bora wa kufika wanapohitaji na dhamira ya Wanayanga ni siku moja kuona timu hiyo ikibeba taji la Afrika.
Aidha Kocha huyo amesema anachohitaji katika mchezo huo ni hamasa ya mashabiki na anatarajia hilo kutoka kwa Wanayanga hasa waliopo visiwani Zanzibar ili kuwaongezea nguvu zaidi katika kuonesha mchezo bora.
Naye Nahodha Msaidizi wa Yanga Dickson Job, amesema wachezaji wamejipanga kukabiliana na kila mpinzani na wanatarajia kuiona timu ikianza vema hatua ya makundi.
“Tupo tayari kukabiliana na kila mpinzani ambaye anakuja mbele yetu. Tuna imani na matarajio makubwa kuhakikisha kuwa tunapata alama tatu muhimu kesho. Tumekuwa na mechi kadhaa za Kimataifa ambazo tumecheza katika Uwanja huu wa Amaan,” amesema Job.
Kwa upande wake Kocha wa AS FAR Rabat Alexandre Santos, amesema ni lazima kuwa makini katika mchezo huo kutokana na kukabiliana na timu yenye wachezaji wenye kiu ya mafanikio.


