Oktoba 29 siku ya giza, ifungue milango ya haki

OKTOBA 29, 2025 itabakia kuwa siku ya giza na machungu katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni siku ambayo imetufunua wote, imetuacha peupe na kutufungamanisha na mataifa mengine ulimwenguni ambayo yamekuwa yakikumbwa na ghasia, mauaji na matendo mengine ya ukiukaji wa haki za binadamu.

Siku hii ilipaswa kuwa ya kuuthibitishia ulimwengu kwamba taifa letu linaheshimu sheria, kanuni na mifumo ya demokrasia ya vyama vingi. Ilipaswa kuandika ukurasa mwingine mzuri uliopambwa kwa wino wa dhahabu, lakini ukageuka kuwa ukurasa uliojaa giza, uliofunikwa kwa damu ya watoto wa taifa hili waliouawa kwa idadi ambayo hadi sasa hakuna anayetaka kuitaja. Ni siku ya maombolezo na majuto makubwa.

Kwamba kabla ya siku hii na matukio yake kutokea watu wanaoifahamu vema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wasingeliweza kabisa kusadiki simulizi yoyote kwamba Watanzania wangeliweza kujitokeza katika mitaa ya miji mikubwa yote, wakaandamana, wakavamia vituo vya kupiga kura na kuharibu karatasi za kura, maboksi ya kura, mahema ya vituo vya kura, wakapora maduka, wakachoma miundombinu mbalimbali – majengo, vituo vya mabasi, vituo vya mafuta – kwa upande mmoja, na kwa upande mwingine polisi kutumia silaha za moto na kuua raia ovyo.

Siku hii ya giza, siku ya kulaaniwa, imetuacha na majeraha makubwa kama taifa. Imetukumbusha kwamba hata sisi ni sawa na watu wengine ambako majanga haya yanatokea. Ambako raia wanakimbia nchi zao. Ambako wanapigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Kwamba tulikuwa tunaamini tu kwamba tuko tofauti na watu wa mataifa mengine yaliyotumbukia kwenye majanga ya kijamii – kama vita, maandamano na vurugu, lakini hatukujiuliza ni kwa nini kwa miaka yote hii tumekuwa tofauti nao mpaka balaa la Oktoba 29, 2025.

Leo tunapojitafakari kama taifa tunajifunza nini katika hili lililotokea? Tumejiuliza kwa uaminifu kabisa wa mioyo yetu kwamba ni kitu gani hasa kimetufikisha hapa tulipofika? Nani yuko tayari kuukubali ukweli huu mchungu juu ya kiini cha hali hii tunayoipitia kama taifa?

Nani asiyejua kwamba duniani kote uchaguzi katika nchi mbalimbali zimekuwa chanzo kikuu cha mizozo isiyoisha? Nani asiyejua kuwa zipo nchi ziligawanyika huku kila upande ukijitangazia ushindi wa uchaguzi? Kwani sisi ni wepesi wa kusahau kwa kiasi gani hata kushindwa kuona au kukumbuka mambo hayo na kwa njia hiyo, tufanye kila lisilobudi kukwepa njia hiyo ya maangamizi, maafa na machungu yasiyostahili kwa kizazi cha sasa wala kijacho?

Umma umesikia kauli za kutaka kuwapo kwa maridhiano; kauli za kutaka kupoza jazba, machungu na maumivu ambayo taifa limepitia katika siku za giza kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 3, 2025. Umma umesikia ahadi hizi. Ungali ukitafakari. Ungali unajiuliza ni kwa kiasi gani safari hii kauli hizi hazitakuwa ahadi tupu ambazo hazitazaa matunda tarajiwa – kufanyika kwa mabadiliko ya kisheria ya kusaidia kufanyika kwa uchaguzi huru, wa haki na kuaminika?

Ni dhahiri kwa sasa taifa liko katika simanzi. Ni simanzi ya kuvunjika kwa amani. Ni simanzi na kuomboleza mauaji yasiyoelezeka ya vijana wengi waliojitokeza kwenye maandamano, lakini pia waliouawa wakiwa kwenye viunga vya nyumbani kwao na hata watu wazima waliouawa katika kadhia hii kubwa iliyokumba miji mikubwa nchini – Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Moshi, Tunduma, Songea kutaja baadhi tu. Ni simanzi ambayo kwa sasa ni lazima iwe darasa la kujifunza jinsi ya kuenenda. Kujifunza kwamba amani ni kitu tete sana, kinaweza kupotea wakati wowote, kama mazingira ya kuwako kwake hayatapaliliwa na kutunzwa vizuri.

Tunaweza kuendelea kuamini kwamba yaliyotokea nchini yalikuwa ni mambo ya bahati mbaya, na kwamba yanaweza yasitokee tena. Hii ni imani, lakini imani mbaya, imani potofu. Sasa tunatakiwa kama taifa tuanze kutafakari ni wapi tulipojikwaa na ni nini hasa kifanyike ili tusirejee tena huko.

Ukirejesha mawazo nyuma kidogo utagundua kwamba kwa muda mrefu sana kama taifa tumepuuza maumivu ya watu. Tumejiaminisha kwa imani potofu kwamba sisi tulikuwa na kinga ya vurugu za kusababisha kupotea kwa amani. Na ndiyo maana malalamiko ya watu juu ya kuuawa kwa ndugu zao, kupotea kwa ndugu zao, kutekwa na kupotezwa hayakuwahi kuwasumbua wenye mamlaka. Kwa muda mrefu mno, wenye mamlaka waliamini kwamba hakuna kitu cha kuitikisa Tanzania. Imani potofu sana.

Mwalimu Julius Nyerere ambaye sote kama taifa tunakiri kwamba ni Baba wa Taifa hili, katika moja ya hotuba zake nyingi alizopata kuzitoa, mwaka 1987 alisema yafuatayo: “Kila kilichoundwa kisipotunzwa huharibika. Msingi wa amani ni haki, ama haki yenyewe kama ipo au matumaini ya kujenga taifa lenye haki. Panapokuwa hapana haki, wala imani ya matumani ya kupata haki, hapawezi kuwa na amani na utulivu wa kisiasa. Hatima yake patazuka fujo, mapambano na utengano.”

Leo ni takribani miaka 38 tangu Mwalimu alipotoa hotuba hiyo. Ni kama maneno yake yametimia. Kinachoshuhudiwa kwa sasa ni kitu kimoja muhimu, kwa muda mrefu tumeshindwa kulinda na kutunza amani. Tumebaki kuiimba amani kama ni wajibu wa raia tu. Kama ni wajibu wa watawaliwa kukubali kuilinda amani, hata kama wanaona kwamba kuna matukio ya wazi kabisa ya ukiukaji mkubwa wa haki zao. Hakuna taifa liliofaulu kujenga amani huku likikanyaga haki za raia wake. Linaweza kudhibiti amani kwa kitambo kidogo tu. Linaweza kutumia misuli kutisha watu kwa kitambo tu, lakini mwishoni umma utachoka. Ukichoka chochote kinaweza kutokea.

Nani alipata kuwaza kwamba matukio ya Oktoba 29 yangewezekana kutokea hasa ikizingatiwa jinsi vyombo vya ulinzi na usalama vilivyokuwa vinapita katika mitaa ya miji mikuu yote ya mikoa kwa takribani wiki mbili mfululizo kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29? Nani angesadiki kwamba kwa hali ya vyombo vya mabavu ilivyokuwa imetanda kuna mtu angejitokeza mtaani siku ya giza nene- Oktoba 29? Yaliyotokea ni kielelezo cha umma kuchoka na kupoteza uvumilivu.

Kwa kuwa tulipuuza mno juhudi za kulinda amani kupitia njia ya haki, sasa matukio ya Oktoba 29 yanatukumbusha na kutulazimisha kwamba sasa turejee njia kuu. Tuzungumze, tusemezane, tuombane radhi, tukumbatiane, tutambue kwamba hakuna hata raia mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ana haki kuliko mwingine. Kwamba sote tunayo nchi hii moja, na ni wajibu wetu wa kiraia kuilinda, kuipenda na kuitetea nchi, kwa kutenda haki. Ni haki tu bila kubaguana ndiyo itasimamisha taifa letu.

spot_img

Latest articles

Fountain Gate yatoa kocha bora

Na Mwandishi Wetu Kocha wa timu ya Fountain Gate,  Mohamed Laizer amechaguliwa kuwa kocha bora...

Nyota JKT Queens aipigia hesabu Asec Mimosa

Na Winfrida Mtoi Mshambuliaji wa JKT Queens FC, Jamila Rajabu, amesema  amejipanga  kutengeneza  nafasi na...

Zungu achaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Na Mwandishi Wetu MBUNGE mteule wa Jimbo la Ilala Mussa Azzan Zungu ameibuka mshindi...

Heche viongozi wengine Chadema waachiwa na Polisi kwa dhamana

Na Mwandishi Wetu Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Heche na...

More like this

Fountain Gate yatoa kocha bora

Na Mwandishi Wetu Kocha wa timu ya Fountain Gate,  Mohamed Laizer amechaguliwa kuwa kocha bora...

Nyota JKT Queens aipigia hesabu Asec Mimosa

Na Winfrida Mtoi Mshambuliaji wa JKT Queens FC, Jamila Rajabu, amesema  amejipanga  kutengeneza  nafasi na...

Zungu achaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Na Mwandishi Wetu MBUNGE mteule wa Jimbo la Ilala Mussa Azzan Zungu ameibuka mshindi...