Na Mwandishi Wetu
Baada ya timu ya JKT Queens kutoa sare mbili mfululizo Ligi ya Mabingwa Wanawake Afrika (CAFWCL), bado ina matumaini ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo, ambapo mchezo ujao itakutana na TP Mazembe Novemba 15,2025.
Katika michuano hiyo inayoendelea nchini Misri, JKT Queens jana ilitoka sare ya 1-1 na Asec Mimosa ya Ivory Coast, mchezo wa kwanza ilitoa suluhu kwanza dhidi ya Gaborone United ya Botswana.
Ili kusonga mbele hatua ya nusu fainali, wawakilishi hao wa Tanzania wanahitaji ushindi mbele ya TP Mazembe ukiwa ni mchezo wao wa mwisho wa kundi B.
Kocha wa timu hiyo, Kessy Abdallah, amewaomba mashabiki wawe na amani kwani, kuelekea mchezo wa mwisho wanaandaa mpango mkakati kuhakikisha timu inakwenda hatua ya nusu fainali.
Naye mlinzi wa kati wa JKT Queens, Ester Maseke, amesema licha ya timu yake kutoka sare dhidi ya Asec Mimosa ya Ivory Coast na kufikisha alama mbili katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake, bado wanaamini wana nafasi ya kufanya vizuri na kufuzu hatua ya nusu fainali.
Maseke amesema kikosi cha JKT Queens kimeonyesha uwezo mzuri katika michezo iliyopita na kwamba matokeo ya sare hayamaanishi mwisho wa safari yao kwenye mashindano hayo.
Ameongeza kuwa tuzo ya mchezaji Bora wa mechi aliyopata katika mchezo dhidi ya Asec Mimosa ni matokeo ya ushirikiano mkubwa kati yake na wachezaji wenzake.


