Maaskofu, Masheikh nyanda za juu wahimiza uchaguzi wa amani

Na Mwandishi Wetu, Mbeya

VIONGOZI wa dini kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wamewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, huku wakisisitiza umuhimu wa kudumisha amani kabla, wakati na baada ya Uchaguzi huo.

Viongozi hao kutoka mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa wametoa kauli hiyo leo Oktoba 23, 2023 katika Kongamano la Amani na Uchaguzi lililofanyika jijini Mbeya.

Mwishoni mwa kongamano hilo lililoongozwa na kauli mbiu ‘Kupiga kura ni haki yetu na kulinda amani ni wajibu wetu’, viongozi wa Dini wamesoma maazimio, yanayosisitiza ulinzi wa amani ya nchi na kuhimiza wananchi kushiriki katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akisoma tamko rasmi la viongozi wa dini wa Nyanda za Juu Kusini, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la TAG ICC Mbeya, Askofu Profesa Donald Mwanjoka, amesema moja ya maazimio ni kuwataka wananchi wote waliopata nafasi ya kujiandikisha kujitokeza siku ya uchaguzi, kufanya maamuzi ya busara na kuchagua viongozi waadilifu watakaotumikia kwa uaminifu.

“Tunawakumbusha wananchi wote kwamba kushiriki katika Uchaguzi ni haki ya kikatiba na wajibu wa kizalendo. Amani ni msingi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kiroho, hivyo tofauti za kisiasa hazipaswi kuwa chanzo cha chuki, maandamano au vurugu,” amesema Prof. Mwanjoka, kwa niaba ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) na Kamati za Amani za mikoa hiyo.

Viongozi hao pia walitoa wito kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, haki na wa kuaminika, huku vyombo vya ulinzi na usalama vikisisitizwa kuzingatia utu, sheria na haki za binadamu wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Sheikh wa Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa huo, Sheikh Msafiri Njalambaha, amesema amani ni msingi wa maisha ya ibada na ustawi wa taifa.

“Hakuna Uchaguzi, maendeleo, wala ibada bila amani. Kura ni haki yetu, amani ni wajibu wetu,” amesema.

Askofu Oscar Ongele ambaye ni Mwenyekiti wa JMAT Mkoa wa Mbeya, amewasihi viongozi wa dini kutumia nyumba za ibada kuhamasisha waumini waliojiandikisha kwenda kupiga kura kwa amani.

“Tujitokeze kwa wingi, tuwahimize waumini wetu washiriki bila hofu, kwa sababu vyombo vya ulinzi na usalama vipo kulinda amani yetu,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Iringa, Dk. Joseph Mgumi, amesema hakuna maendeleo bila uongozi na hakuna uongozi bila Uchaguzi, hivyo ni muhimu kila Mtanzania kushiriki.

“Tupige kura kwa wingi ili tupate viongozi watakaotuletea maendeleo,” amesema.Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa wa Songwe, Sheikh Alhaj Batuza, amesisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa kila jambo.

“Wazee wetu walihangaika kuupata uhuru. Leo sisi tunapaswa kuilinda amani kwa vitendo, si kwa maneno,” amesema.

Aidha, Askofu Mstaafu Ambele Mwaipopo wa KKKT Dayosisi ya Ziwa Tanganyika (Rukwa) amewakumbusha wananchi kuwa ni wajibu wa kila mmoja kulinda amani aliyopewa na Mungu.

“Asicheze mtu na amani ya taifa letu; kila mmoja awe mlinzi wa amani,” amesema.Sheikh wa Wilaya ya Njombe (mkoani Njombe), Shabani Dinga amewahamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kwa amani, huku akisisitiza umuhimu wa uvumilivu na ukomavu wa kisiasa.

Naye Askofu Jacob Kahemele wa Kanisa la Anglikana Mbeya amesema tofauti za kisiasa hazipaswi kugawa watu.

“Uchaguzi ni mchakato wa kawaida wa kidemokrasia. Tuwe na hekima, tuvumiliane, tushiriki kwa amani,” amesema.

Kwa upande wake, Askofu Erica Mwakyokile wa Kanisa la Pentecost Shilo Mkoa wa Mbeya, amewahamasisha Watanzania kuendelea na maombi katika nyumba za ibada hadi Uchaguzi utakapopita.

“Kila mtu yuko hapa kwa sababu ya amani, tuendelee kuomba ili Tanzania iendelee kuwa nchi ya utulivu,” alisema.Viongozi hao kwa pamoja walihitimisha kwa kuwataka Watanzania kutambua kuwa kura moja inaweza kuandika historia mpya ya taifa, hivyo wajitokeze kupiga kura kwa amani, umoja na uzalendo, wakiweka mbele maslahi ya nchi kuliko ya mtu binafsi.

spot_img

Latest articles

Mradi wa Taza kufungua Soko jipya la biashara ya umeme Afrika

Na Mwandishi Wetu, Mbeya IMEELEZWA kuwa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya...

SGR yapata ajali, TRC yataja chanzo

Na Mwandishi Wetu Treni ya Mwendokasi (SGR) imeacha njia yake na kupata ajali katika eneo...

Yajayo baada ya uchaguzi mkuu yahitaji hekima kubwa

JUMATANO ijayo, OKTOBA 29, 2025, taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linakwenda kuongeza...

More like this

Mradi wa Taza kufungua Soko jipya la biashara ya umeme Afrika

Na Mwandishi Wetu, Mbeya IMEELEZWA kuwa mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya...

SGR yapata ajali, TRC yataja chanzo

Na Mwandishi Wetu Treni ya Mwendokasi (SGR) imeacha njia yake na kupata ajali katika eneo...