Ukatili huu wa Polisi unawapa faraja gani?

UKATILI uliofanywa na baadhi ya askari polisi dhidi ya raia waliokuwa wanakwenda kusikiliza kesi ya jinai inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Jumatatu ya wiki hii Septemba 15, 2025 jijini Dar es Salaam, unatukumbusha kutupia tena macho ripoti ya Tume ya Haki Jinai ambayo iliundwa kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini. Tume hii iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na kisha kuizindua Januari 31, 2023. Tume hii iliyoongozwa na Mwenyekiti Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, Makamu Mwenyekiti Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue na wajumbe tisa pamoja na Sekretarieti yake, ilifanya kazi kwa takribani miezi saba na kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Julai 2023.

Itakumbukwa kwamba madhumuni ya Tume hiyo yalikuwa ni kumsaidia Rais kupata ushauri na mapendekezo juu ya namna bora ya kuboresha mfumo na utendaji kazi wa taasisi zinazohusika na haki jinai. Kuundwa kwa Tume hii ilikuwa ni njia ya kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu utendaji katika taasisi za haki jinai na mfumo wa utoaji haki nchini kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na haki za raia. Katika mapendekezo yake, Tume ilibaini kuwapo kwa matatizo na changamoto nyingi katika mnyororo wa haki jinai, tangu kwenye kuzuia uhalifu; kubaini uhalifu unapotendeka na taarifa kutolewa Polisi; uchunguzi na namna ukamataji wa watuhumiwa unavyofanyika; mashtaka yanapoandaliwa; mashauri yanapoendeshwa na hukumu kutolewa

mahakamani; waliohukumiwa wanapokwenda kufungwa magerezani; na maisha ya wafungwa waliomaliza vifungo vyao wanaporejea uraiani. Ni hakika, Tume hii ilifanya kazi kubwa na ya kutukuka.

Katika vyombo vilivyoguswa kwa undani na Tume hii ni pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania. Tume ilisema dhahiri kwamba: “Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko mbalimbali kutoka kwa wananchi kuhusu vitendo vinavyochafua taswira ya Jeshi la Polisi. Malalamiko hayo dhidi ya Jeshi la Polisi yanahusu kushindwa kuzuia uhalifu, matumizi ya nguvu kupita kiasi, kubambikia kesi, vitendo vya rushwa, mali za watuhumiwa kupotea vituoni na kuchelewa kufika kwenye maeneo ya matukio. Hali hiyo inasababisha wananchi kupoteza imani kwa Jeshi la Polisi na kutokutoa ushirikiano unaotakiwa.”

Ili kukabiliana na changamoto hizo, Tume ilipendekeza mambo kadhaa kuhusu Jeshi la Polisi, mosi, Jeshi la Polisi lifanyiwe tathmini ya kina itakayoliwezesha kufanyiwa maboresho makubwa na kuundwa upya ili kuondoa kasoro za kiutendaji zilizopo; pili, Jeshi la Polisi libadilishwe kisheria, kimuundo na kifikra na kuwa Polisi Tanzania (National Police Service) ili kutoa taswira kuwa Jeshi la

Polisi ni chombo cha kuwahudumia wananchi; na tatu, kubadilisha mitaala ya mafunzo na mtazamo wa askari wa Jeshi la Polisi ili kutoka katika dhana ya ujeshi (police force) kwenda dhana ya kuhudumia wananchi (police service). Haya ni baadhi tu ya mapendekezo yaliyotolewa na Tume ili kuboresha Jeshi la Polisi kuwa chombo cha kuhudumia wananchi.

Kama nilivyoeleza hapo juu, ukatili ulioshuhudiwa Jumatatu wiki hii ukifanywa na askari polisi dhidi ya raia waliokuwa wanakwenda kusikiliza kesi ya Lissu Mahakama Kuu Dar es Salaam, umeshitua wengi. Hii si mara ya kwanza askari hao kuwapiga raia mithili ya wafugaji waswagavyo wanyama. Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zinaonyesha ukatili usiomithilika, ukitendwa mchana kweupe. Watu wanapigwa kana kwamba ni wahalifu waliojihami kukabiliana na askari hao. Wapo waliojeruhiwa mgongoni, miguuni na sehemu nyingine za mwili. Kwa kifupi, damu imemwagika tena. Yaani askari wanampiga mtu ambaye hata hajiwezi kaanguka chini, au wamekwisha kumdhibiti. Ukatili wa kinyama kabisa.

Matukio haya yanatokea miaka miwili na ushei baada ya mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kupokelewa na Rais. Mapendekezo ambayo kimsingi yalipaswa kuwa dira na mwelekeo mpya wa kulisuka Jeshi la Polisi. Miaka miwili siyo muda mfupi. Kwa mwenye nia ya kubadili hali ya mambo, dalili za mabadiliko zingeanza kuonekana. Kinachofanywa na askari hawa, kama kilivyoshuhudiwa Jumatatu wiki hii, ni kielelezo kwamba bado kama taifa tuna safari ndefu sana ya kulifanyia mageuzi yenye tija Jeshi la Polisi, ili liwe na utu katika utendaji wake kwa maana hiyo kuzingatia dhima hasa ya kuanzishwa kwake- ulinzi wa uhai na mali za raia.

Ukijiuliza kwa mfano, Polisi wanaweza kujitetea kwa kitu gani kwamba raia kwenda kusikiliza kesi mahakamani ni kosa la jinai. Na kama ni kosa la jinai, adhabu yake ni kupigwa mithili ya mnyama anayeswagwa? Kwa nini kuna juhudi kubwa ya kutaka kuzuia raia kufika mahakamani kusikiliza kesi ya Lissu? Kuna shida gani hata kama watajaa mahakamani kama mafuriko? Uendeshaji wa kesi hii unafanyika katika mahakama ya wazi. Ni eneo ambalo raia wanaruhusiwa kufika. Polisi wanawazuia raia kufika mahakamani kusikiliza kesi ili iweje?

Wapo wanaodhani kwamba haya ni mambo mepesi. Kwamba askari polisi anaweza tu kunyanyua fimbo akamtwanga raia kama mtu anayeua nyoka, kisha akampiga mateke akiwa tayari ameanguka chini. Unyama huu unaweza kuufananisha na ule waliokuwa wanafanyiwa raia weusi wa Afrika Kusini zama za utawala wa ubaguzi wa rangi wa Makaburu.

Yapo maswali mengi yamekuwa yanaulizwa juu ya mwenendo wa baadhi ya askari polisi. Wapo baadhi ya askari polisi matendo yao dhidi ya raia ni uhalifu wa kiwango cha juu. Kumtwanga marungu, mateke raia mwenye chupa ya maji ya kunywa mkononi, ni kielelezo cha juu kabisa cha ukatili, unyama na uhalifu dhidi ya utu. Askari mwenye kiapo cha kulinda raia na mali zao, anapata wapi nguvu na msukumo wa kuona damu ya raia asiye na hatia ikimwagika? Anapata faida gani akishamvunja raia mguu, au mkono, au kumsababishia majeraha mengine mwilini? Huu ni upolisi wa nini? Kuumiza raia au kulinda raia?

Kumekuwa na vilio vya muda mrefu sasa dhidi ya polisi juu ya tabia hii ya matumizi ya nguvu iliyopitiliza dhidi ya raia. Kwa bahati mbaya, wenye dhima ya kusaidia kusukuma mabadiliko ya kifikra na kimwenendo kama Tume ya Haki Jinai ilivyoshauri, ni kama wanaamini zaidi katika matendo ya kikatili dhidi ya raia. Ukitafakari kwa kina sana unashindwa kuona askari anayejeruhi raia, anapata faraja gani, au anapata faida gani au anakuwa amejiimarisha kivipi kiweledi?

Kwa hali ya mambo inavyokwenda kama Jeshi la Polisi halitaundwa upya, kuna kila uwezekano chombo hiki muhimu kwa ajili ya ulinzi wa uhai na mali za raia, kidogo kidogo kinaelekea kutumbukiza taifa katika chuki kubwa. Matendo ya kupigapiga ovyo raia, kuwajeruhi, kuwabambika kesi yanatoa ujumbe mmoja kwa raia, kwamba polisi siyo kwa ajili yao bali dhidi yao. Matendo haya yanapanda mbegu ya uhasama na chuki. Huu siyo mwelekeo unaotubashiria mustakabali mwema kama taifa. Yu wapi wa kuwaambia askari hawa sasa ukatili wao watosha?

spot_img

Latest articles

Mwendokasi: Adha kwa abiria, gubu la madereva

Na Mwandishi Wetu Inakaribia miaka 10 tangu usafiri wa mabasi ya haraka maarufu kama Mwendokasi...

Vijana wahimizwa kuendelea kulinda amani

Na Tatu Mohamed VIJANA nchini wametakiwa kuhakikisha wanalinda na kuendeleza amani iliyopo kwa kuwa wao...

Serikali ya Austria kufadhili miradi ya umeme Tanzania

Na Mwandishi Wetu SERIKALI ya Austria kupitia Benki ya UniCredit imeahidi kuipatia fedha...

NIDA yawasajili watu wenye mahitaji maalum Temeke

Na Tatu Mohamed KATIKA kuadhimisha Siku ya Utambulisho Duniani, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA)...

More like this

Mwendokasi: Adha kwa abiria, gubu la madereva

Na Mwandishi Wetu Inakaribia miaka 10 tangu usafiri wa mabasi ya haraka maarufu kama Mwendokasi...

Vijana wahimizwa kuendelea kulinda amani

Na Tatu Mohamed VIJANA nchini wametakiwa kuhakikisha wanalinda na kuendeleza amani iliyopo kwa kuwa wao...

Serikali ya Austria kufadhili miradi ya umeme Tanzania

Na Mwandishi Wetu SERIKALI ya Austria kupitia Benki ya UniCredit imeahidi kuipatia fedha...