Polepole achana na gia ya wamachinga, ni donda ndugu

HIVI karibuni Humphrey Polepole, mwanasiasa machachari na aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Malawi na baadaye Cuba na nchi kadhaa za Caribbean, alirusha makombora mazito. Amegusa watu kadhaa. Sina shauku ya kumgusa yeyote kati ya hao ambao Polepole amewashambulia, akawabagaza, akawadhalilisha na kuwaita majina aliyowaita. Sina sababu. Kikubwa, wapo na wanaweza kujitetea wenyewe. Na baadhi wamejitetea kwa takwimu na vielelezo vya uhakika.

Katika safu hii, nilipata kuandika “Kwa nini ninatamani Polepole anyamaze milele.”  Katika makala ile, ambayo ilitoka katika safu hii Julai 31, 2025, nilimkumbusha Polepole ambaye analia leo kwamba chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimejaa wahuni, kuwa yeye ni sehemu ya hiki anachotaka kuaminisha umma kwamba anapingana nacho.

Nilimtaka Polepole ajitokeze kwanza hadharani, awaombe radhi Watanzania kwa kuwa sehemu ya uchafuzi wa uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020. Aidha, nilimkumbusha Polepole kwamba kile walichokianzisha cha kumomonyoa demokrasia kwa ule uhuni wa ‘kuunga juhudi’ kati ya 2016 – 2020- huku mabilioni ya fedha za walipa kodi yakitumika kuwarubuni wanasiasa wa upinzani kujiunga na chama tawala, wakiwamo wabunge, madiwani, na wajumbe wa serikali za mitaa, ndiyo hasa msingi wa kilio chake leo.

Kuna watu wengi nimezungumza nao, na wanaamini kwamba Polepole anafanya kazi njema na ya kusaidia kukomboa taifa hili. Sitaki kuingia kwenye mjadala huo, kwa sababu hicho anacholilia au kulaani au kupinga ni kilio cha kutaka kurejea kwa yale yaliyojiri kati ya 2016 na 2020, lakini pia ni kilio cha kutaka kundi lao litawale dola. Kwa maneno mengine, Polepole analilia kurejea kwa kundi lao dhidi ya kundi lingine ambalo anaamini sasa ndilo limetamalaki.

Kwa leo ninaomba kujielekeza kwenye moja ya hoja yangu ambayo kwa muda imekuwa inaniuma kila nipitapo kwenye miji ya nchi hii. Hoja ya kutamalaki kwa ‘uholela, vurugu, uchafu na kelele zisizoelezeka’ katika miji mingi ya nchi hii. Wiki iliyopita niliandika katika safu hii kwamba Ninatamani Tume ya Charles Keenja irudi Dar es Salaam. Kwa waliokuwapo 1996 watakumbuka kuundwa kwa Tume ya Jiji la Dar es Salaam maalumu kama Tume ya Keenja kuongoza Jiji la Dar es Salaam baada ya kushindwa kabisa kwa halmashauri ya Jiji hilo kutimiza wajibu wake. Kikubwa kushindwa kusafisha jiji. Milima ya taka kuzagaa kila pahali, vibanda vya wafanyabiashara ndogo ndogo vichafu kutapakaa kila pahala, uchuuzi wa kila aina kila pahala. Vyote hivi vilikuwa ni uholela usiomithilika uliokuwa taswira ya Jiji la Dar es Salaam.

Juzi Polepole katika hoja zake ameshangaa kwamba mwaka 2021 serikali ya awamu ya sita iliamua kuwafurusha wamachinga mijini, wakati serikali ya awamu ya tano ya JPM ilikuwa imepiga marufuku wamachinga kusumbuliwa!

Yaani kama kuna shida kubwa inayokabili maisha ya wakazi wa miji yote ya Tanzania kwa sasa, ni uholela wa wamachinga. Nitangaze mapema kabisa, sina nongwa na wamachinga. Ninatambua wanatafuta mkate wao wa kila siku. Wapo ndugu na hata wanangu katika umachinga. Lakini, sikubaliani na uholela wao usiokuwa na mipaka. Hapana!

Tatizo ambalo ninaliona sasa ambalo labda Polepole anayehoji sababu ya wamachinga kutakiwa kujipanga, angetusaidia kueleza ni kwamba kwa kiwango gani ule utaratibu wa kuwapa vitambulisho wamachinga, ulisaidia kuwapanga, kupanga miji yetu, kuzuia ‘uholela’ wa kufanya biashara kokote – barabarani sehemu ya kupita magari, ya waenda kwa miguu, juu ya mitaro ya maji, mbele ya maduka ya watu na hata kwenye malango ya makazi ya watu?

Wamachinga kwa jinsi wanavyofanya shughuli zao sasa katika miji mikubwa, hakika hili ni bomu. Hakuna utaratibu wowote, hakuna udhibiti wowote, hakuna uzingatiaji wa tahadhari yoyote ya usalama, na kwa ujumla ni upenyo mkubwa wa kukwepa ulipaji wa kodi halali kwa serikali.

Ukipitapita katika mitaa mingi ya miji yetu, utashuhudia mtu anayejiita mmachinga akiwa amepanga bidhaa ambazo zinajaa duka, tena duka kubwa ambalo lingestahili kulipa kodi halali serikalini. Hawa ndiyo wamachinga wamezagaa kila kona. Kwamba pamoja na juhudi za awali za serikali ya awamu ya sita za kutaka kuwapanga, kwa sasa hivi ni kama serikali imezidiwa mbinu na maarifa ya kuratibu shughuli za wamachinga.

Nilisema wiki iliyopita, na leo ninasema tena hakika hatuwezi kuona manufaa ya uboreshaji wa miundombinu kama barabara na madaraja katika miji yetu, kama hatuwezi kudhibiti uholela wa kuacha kila mwenye gunia lake alitandike kokote na kupanga hapo bidhaa zozote, kisa anatafuta kipato. Ni lazima tukubali na kuelewa kwamba binadamu kwa kawaida anaishi kwa kanuni, taratibu na sheria. Katika uzingatiaji wa vitu hivyo, hatuwezi kudhani kwamba kuacha tu kila mahali pawe ni gulio, pawe ni vibanda vya wamachinga, pawe ni uchuuzi holela, eti ni mbinu ya kuwasaidia wamachinga.

Sitaki kuamini kwamba serikali imeshindwa kuwapanga wamachinga. Eti imeshindwa kuwapatia mahali pa kufanyia shughuli zao na kwa uhakika na katika kusimamia sheria na taratibu watakiwe kufanya shughuli zao huko. Utaratibu wa kudhani kwamba kuwaacha wamachinga watapakae kila kona ni kubembeleza kura, ni kujidanganya, kimsingi ni kuzuia kasi ya maendeleo, hakika ni kufungua mkondo wa kusaidia kukwepa kulipa kodi halali kwa serikali.

Ninamuomba Polepole akumbuke kwamba kilele cha vurugu za wamachinga ambazo sasa hivi Watanzania wanapambana nazo, ni vile vitambulisho walivyovishabikia sana. Kila kimoja kikiuzwa kwa Sh. 20,000/- Umma utakumbuka kwamba awali, serikali ya awamu ya tano ilitoa vitambulisho 670,000 na katika awamu ya pili vilitolewa vitambulisho 1,100,000 kwa wakuu wote wa mikoa ambao walikuwa na jukumu la kuhakikisha vinawafikia wamachinga.

Katika kugawa vitambulisho hivyo, hakukuwa na utaratibu wowote wa maana wa kuhakikisha wamachinga hao wana maeneo mahususi ya kuendesha biashara zao. Nia ilikuwa ni kuuza vitambulisho tu. Uholela huu mpaka sasa hivi unatungarimu kama taifa.

Kwa mfano, sasa hivi ukiinga ndani ya Stendi Kuu ya Mabasi ya Magufuli pale Mbezi Mwisho, hakika unaweza kupata mshituko mkubwa. Stendi ile ambayo ilijengwa kwa gharama kubwa ya Sh. bilioni 71, ilipaswa kuwa kioo cha nchi. Ni stendi ya kimataifa. Ndiyo stendi kubwa kuliko zote nchini. Lakini, kwa sasa hivi mle ndani ni umachinga na uholela wa hatari umejaa. Kila mahali ni uchuuzi usiokuwa na mpangilio wowote wa maana. Hali ya mle ndani inashangaza mno. Huu ni mfano mwingine wa kuonyesha kwamba taifa linajenga miundombinu muhimu kwa gharama kubwa, lakini mwisho wa siku inaachwa tu kuendeshwa kiholela mno.

Tunapozungumza mambo haya mtu anaweza kudhani kwamba ni mambo madogo. Kikubwa ambacho baadhi ya watu hawaoni, akiwamo Polepole, ni kutaka kuona ubora wa maisha kwa Watanzania ukiongezeka, kwamba miundombinu hii inayojengwa inaongeza vipi ubora wa maisha ya watu wetu ni jambo la msingi sana. Sasa ukimsikia Polepole akitaka umachinga utamalaki kila mahali nashindwa kujua anataka kutuongezea ubora gani wa maisha au ni uwajibikaji gani anataka kuchochea? Polepole achana na gia ya wamachinga, hili ni donda ndugu.

spot_img

Latest articles

Shughuli ya Wanamsimbazi imenoga kwa Mkapa

Na Winfrida Mtoi MASHABIKI wa timu ya Simba wamejitokeza kwa wingi kuhakikisha wanashuhudia kilele cha...

Mhandisi Mramba na JICA wajadili utekelezaji wa Miradi ya Nishati

Na Mwandishi Wetu KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amekutana na...

Ujenzi wa Kampasi ya UDOM Njombe waanza kwa kasi

Na Mwandishi Wetu UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ukiongozwa na Makamu Mkuu wa...

Serikali yasitisha mchakato uchaguzi TOC

Na Mwandishi Wetu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imesitisha mchakato wa uchaguzi wa...

More like this

Shughuli ya Wanamsimbazi imenoga kwa Mkapa

Na Winfrida Mtoi MASHABIKI wa timu ya Simba wamejitokeza kwa wingi kuhakikisha wanashuhudia kilele cha...

Mhandisi Mramba na JICA wajadili utekelezaji wa Miradi ya Nishati

Na Mwandishi Wetu KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amekutana na...

Ujenzi wa Kampasi ya UDOM Njombe waanza kwa kasi

Na Mwandishi Wetu UONGOZI wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ukiongozwa na Makamu Mkuu wa...