TAIFA lipo katika kampeni za uchaguzi mkuu ambao ni mahususi kusaka madaraka ya dola. Wapo wanaosaka nafasi ya kiti cha rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wapo wanaotafuta nafasi katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na wapo wanaotafuta viti katika mabaraza ya madiwani. Pamoja na ukweli kwamba hamasa ya uchaguzi mwaka huu haiko juu sana kama ilivyopata kuwa katika chaguzi nyingine sita zilizopita, haibadilishi ukweli kwamba baada ya Oktoba 29, mwaka huu, tutakuwa na muhula mpya wa serikali. Kwa maana hiyo tutakuwa na Rais na Baraza jipya la mawaziri, Bunge jipya na mabaraza ya madiwani mapya nchini kote.
Uchaguzi unafanyika kwa sababu ni takwa la kikatiba. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ibara ya 8 (a) inaeleza chimbuko la madaraka ya serikali kwa kueleza kwamba: “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa katiba hii”; sehemu ya (b) inasema: “lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;”
Kwa msingi huu, uchaguzi ni njia ya kikatiba na kisheria ya kupata madaraka ya dola kwa ajili ya kutumikia watu. Ukitafakari nguvu kubwa inayotumika kutafuta madaraka hayo unapata uelewa wa umuhimu wa madaraka hayo ya dola. Ukitafakari nafasi ya urais unaona kwa wazi kabisa ni nafasi kubwa yenye madaraka makubwa, lakini wakati wote katika kukalia madaraka hayo ni vema ikaeleweka kwamba chimbuko la madaraka hayo ni wananchi. Vivyo hivyo kwa wabunge na madiwani.
Ninatamani kuzungumza kwa kiasi nafasi ya madiwani katika mlolongo huo wa madaraka ya dola. Sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 ndiyo inaweka utaratibu wa kuwapata viongozi hao. Madiwani ni sehemu muhimu ya kuundwa kwa serikali za mitaa. Hawa ndiyo wanaounda mabaraza ya madiwani katika halmashauri zote nchini. Halmashauri zipo za aina nne, halmashauri za wilaya; halmashauri za miji; halmashauri za manispaa na halmashauri za majiji.
Katika mfumo wa utawala wa serikali nchini, madaraka ya serikali huanzia kwenye ngazi ya mtaa ambako kuna serikali ya mtaa, au kijiji. Viongozi wote hawa, yaani wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji na wajumbe wao, huchaguliwa na wananchi moja kwa moja. Kwa rejea ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya 8 (a) na (b) wenye mamlaka ni wananchi na wanachagua wanaokalia viti vya mamlaka ya dola – rais, wabunge na madiwani ili waletewe ustawi. Kazi kuu ya serikali iwe ya mtaa, ya Kijiji, halmashauri, bunge mpaka kwa rais ni kuwaletea wananchi ustawi.
Ukitazama kazi ambayo imefanywa na serikali katika wajibu wa kuwaletea wananchi maendeleo, utaona mambo mengi makubwa yaliyofanyika. Kwa mfano, zimejengwa barabara nyingi katika miji yote ya Tanzania, yamejengwa madaraja makubwa, mifumo ya mitandao ya maji safi na taka nayo imejengwa. Zimejengwa shule, zahanati, vituo vya afya na huduma nyingine za kijamii kwa kiwango cha juu na kwa gharama kubwa pia. Shughuli hizi za ujenzi wa miundombinu ndiyo hasa njia ya kuwapelekea ustawi wananchi. Ndiyo jukumu la serikali, na ni hakika ndiyo matumizi sahihi ya kodi za wananchi.
Katika juhudi hizi, kuna kitu ambacho kwa uhakika halmashauri nyingi, hasa zile za miji mikubwa kama za majiji, manispaa zimekwama kabisa kufanya. Hii ni kuweka miji hiyo katika hali ya usafi. Ukitembelea miji yote mikubwa ya Tanzania, kama Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Arusha, Moshi, Dodoma na kwingineko kwingi tu, kuna uholela wa kutisha katika kufanya biashara.
Kwa mfano, kila mahali sasa hivi yameibuka masoko yasiyo rasmi, vibanda na shughuli za wamachinga zimezagaa kila kona. Katika miji yetu, kuna sehemu huwezi siyo tu kupita kwa gari, bali hata kwa miguu ni lazima ujipange sawa sawa ili kupita. Mitaa ya Kariakoo katika jiji la Dar es Salaam, hakika huwezi kupenya kwa gari katika maeneo mengi.
Kuna vurugu na uvamizi wa barabara zilizojengwa kwa gharama kubwa. Wavamizi wakuu ni wamachinga, madereva wa bodaboda na bajaj, pamoja na vijiwe vya mama na baba lishe. Kwa kifupi ni hivi, hizi zinazoitwa serikali za mitaa ni kama zimejivua wajibu wao muhimu wa kusimamia mpangilio wa kisheria unaokubalika wa watu kufanya shughuli zao mijini. Kila mahali sasa ni soko, kila mahali sasa ni mikokoteni na vibanda vya kudumu vya wamachinga.
Hali hii ya uholela usiodhibitiwa unazaa tatizo jingine kubwa la kiafya. Kwamba sasa ukusanyaji na uzoaji wa taka katika maeneo hayo yaliyovamiwa umekuwa ni mgumu. Mitaro ya maji machafu sasa imegeuzwa kuwa sehemu ya kutupa taka ngumu, hasa mifuko ya plastiki. Hata zile juhudi za kukomesha mifuko ya plastiki sasa zimekuwa ni bure. Kila mahali sasa mifuko ya plastiki imetapakaa, imerejea kama zamani. Hakuna hatua zozote zinachukuliwa. Ukifanya ulinganisho baina ya Tanzania Bara na Zanzibar katika udhibiti wa mifuko ya plastiki, utaona jinsi Zanzibar wamepiga hatua. Tanzania Bara ni kama hakuna tena udhibiti.
Kuyumba au kushindwa kwa halmashauri kufanya majukumu yake, ndiko mwaka 1996 kulisababisha aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, katika serikali ya Rais Benjamin Mkapa, kuvunja lililokuwa Jiji la Dar es Salaam. Kwa maana hiyo baraza lote la madiwani lilivunjwa na badala yake iliundwa Tume ya Jiji la Dar es Salaam, iliyoongozwa na mwenyekiti wake, Charles Keenja.
Tume ya Keenja iliyodumu kwa zaidi ya miaka minne ilijipatia umaarufu mkubwa. Ilisafisha jiji la Dar es Salaam lililokuwa limeshindikana. Ilifanikiwa kuondoa vibanda vya wafanyabiashara ndogondogo vilivyokuwa vimetapakaa kila mahali, vingine karibu kabisa na ikulu. Tume hii ilifanikiwa kukarabati hata majengo ya jiji yaliyokuwa yemechakaa kiasi cha kuhatarisha maisha ya watumishi wa umma waliokuwa wanayatumia.
Moto wa Tume ya jiji uliacha swali moja muhimu na zito mpaka leo, kwamba, je, ni bora kuwa na madiwani katika kusimamia shughuli zote za utawala katika halmashauri za taifa hili, au bora kuwa na tume kama ya Keenja iliyofanya kazi ya kupigiwa mfano? Swali hili mpaka leo hii linasumbua akili za wengi. Kwamba kwa nini tuna miji michafu na mabaraza ya madiwani yapo? Kwa nini hatuwezi kuwapanga wamachinga hata pale serikali ilipojenga masoko ambayo yangeliweza kutumika na kuacha barabara zitumike kwa madhumuni ya kujengwa kwake? Kwa nini kila uchao uzembe wa kushindwa kusimamia mpangilio mzuri wa kukaa mjini unagharimu wakazi wa mijini muda na fedha nyingi kusafiri kutoka kituo kimoja kwenda kingine?
Ni kwa jinsi hii pamoja na ukweli kwamba uchaguzi wa madiwani ni moja ya matakwa ya kikatiba kwa Tanzania, kila nikilala na kutafakari, ninatamani sana kuona Tume kama ya Keenja ikitusaidia kusimamia miji yetu. Ninatamani kuona watu wanaothubutu kuwaambia wamachinga kwamba hapa hamuwezi kufanya uchuuzi wenu, nendeni pale tulipowatengea nafasi; natamani kuona watu wanawajibika ili ustawi utokee katika miji yetu na siyo kuchelea kukosa kura kwa kuwa eti watakuwa wamewakasirisha wamachinga kwa kuwaambia kwamba uholela wao hauleti tija bali hasara kwa taifa. Ninaitamani Tume ya Charles Keenja irudi tena Dar es Salaam.