Na Mwandishi Wetu
Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Grace Magembe, ametoa ufafanuzi kuhusu picha mjongeo (video) iliyosambaa mitandaoni ikimuonesha muuguzi na askari wakivutana katika hospitali ya Halmashauri ya Kibondo, mkoani Kigoma, akisema chanzo cha sakata hilo zilikuwepo tetesi za muuguzi huyo kuomba rushwa kwa wagonjwa na ndugu, ambapo walieleza ndugu wa mama huyo waliombwa na muuguzi Sh 60,000.
“Kilichooneka ni mtego ambao uongozi wa hospitali uliweka mara baada ya kupata taarifa za uwepo wa taarifa za muuguzi huyo kupokea rushwa huku ikisemekana alikuwa ametanguliziwa shilingi 39,000, hivyo uongozi ukaweka mtego wa kumkamata akipokea kiasi kilichobaki cha shilingi 21,000 hapo ndipo kulipozua taharuki, amesema Dk. Magembe.

Akitoa ufafanuzi huo mbele ya waandishi wa habari leo Septemba 2, 2025 jijini Dodoma, Dk. Magembe video hiyo iliyosambaa ilidaiwa kuwa askari alivamia chumba cha kujifungulia, jambo ambalo sio kweli na ilikuwa na nia ovu ya kuichonganisha Serikali na wananchi.
Amesema, mama huyo alifika hospitalini hapo Agosti 28, 2025 na kupata huduma ya kujifungua kwa njia ya upasuaji siku hiyo hiyo majira ya saa 1:40 usiku ambapo alipumzishwa Agosti 29 na 30, 2025 aliruhusiwa na anaendelea vizuri.
Dk. Magembe amesema video hiyo ilisambaa ikiwa na maelezo kuwa muuguzi huyo alikuwa anamtoa mzazi kondo la nyuma jambo ambalo sio kweli kwani kondo la nyuma hutolewa kipindi cha kujifungua kwa njia ya kawaida au kwa njia ya upasuaji, na tukio hilo halikutokea katika chumba cha kujifungilia au cha upasuaji bali ilikuwa ni wodini.
“Mama anayetolewa kondo kupitia via vya uzazi ni yule aliyejifungua kwa njia ya kawaida, mama huyu alijifungua kwa njia ya upasuaji na hivyo kondo lake lilitolewa akiwa chumba cha upasuaji na sio wodini,” amefafanua.
Kuhusu muuguzi kuonekana kuvaa ‘gloves’, amesema kuwa ni sehemu ya kanuni na utaratibu wa watumishi wa afya wawapo katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku hususan pale mtumishi anapokuwa eneo la kazi, shabaha ikiwa ni kujilinda dhidi ya maradhi au kuambukiza wengine.
Akifafanua kuhusu hatua zilizofikiwa hadi hivi sasa juu ya mtumishi huyo, amesema suala hilo lipo chini ya mamlaka zingine kama ilivyofafanuliwa kwenye taarifa iliyotolewa na mamlaka ya Halmashauri ya Kibondo.