Na Mwandishi Wetu
Timu ya Taifa ya wanawake ya mchezo wa kriketi ya Tanzania inatarajiwa kushiriki mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia yatakayofanyika nchini Namibia kuanzia Agosti 30 hadi 5 Septemba 2025.
Mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha nchi nane kutoka Kanda ya Afrika ambazo ni Nigeria, Namibia, Kenya, Rwanda, Tanzania, Botswana na Uganda, ambazo zitachuana kuwania nafasi ya hatua za juu.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Kriketi Tanzania (TCA), kikosi cha Tanzania kimejiandaa vyema na kipo tayari kwa ushindani mkubwa ili kuhakikisha kinapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika hatua zinazofuata za michuano ya dunia.

Wachezaji wa kikosi hicho wametoa wito kwa watanzania kuwapa sapoti ya hali na mali, wakibainisha kuwa uwepo wa mashabiki na hamasa kutoka nyumbani utawapa nguvu zaidi ya kupambana uwanjani.
Mashindano hayo yanachukuliwa kuwa hatua muhimu katika kuendeleza mchezo wa kriketi barani Afrika na kutoa nafasi kwa wachezaji chipukizi kuonyesha vipaji vyao, huku Tanzania ikitarajia kutumia mashindano haya kuinua hadhi ya mchezo huo nchini.