Vyama vya siasa vyakumbushwa kutekeleza Sheria ya Gharama za Uchaguzi

Na Tatu Mohamed 

VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kuhakikisha wagombea wao wanazingatia matakwa ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 (Sura ya 278), ili kudhibiti matumizi ya fedha zisizo halali na kulinda usawa wa kidemokrasia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Hayo yameelezwa leo Agosti 18, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Sehemu ya Ruzuku kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, CPA Edmund Mugasha kwenye Mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa.

Amesema Sheria hiyo inaweka sharti la kila chama na kila mgombea kuweka wazi mapato na matumizi ya gharama za uchaguzi, jambo ambalo ni msingi wa uchaguzi huru na wa haki.

“Kila chama na mgombea anatakiwa kutangaza mapato na matumizi ya kampeni. Viongozi mna jukumu la kuhimiza wagombea wenu kutekeleza hili kwa uwazi,” amesema Mugasha, akifafanua kuwa udhibiti wa gharama ni nyenzo muhimu ya kulinda demokrasia.

Awali, akifungua mafunzo hayo Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuhakikisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinafanyika kwa amani na kistaarabu, bila kutumia lugha za matusi, kashfa au vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha mshikamano wa taifa.

Amesema vyama vina wajibu wa kuendeleza misingi ya amani na mshikamano uliorithiwa kutoka kwa waasisi wa taifa.

“Nendeni mkafanye kampeni za kistaarabu mkiwanadi wagombea wenu. Jiepusheni kabisa na lugha za matusi, kashfa, uchochezi au vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga amani na utulivu wa taifa letu,” amesema Jaji Mutungi.

Amesisitiza kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi na kwamba siasa hazipaswi kugeuzwa chanzo cha migawanyiko.

“Uchaguzi si mwisho wa siasa wala maendeleo. Turithishe amani hii kwa kizazi hiki na vizazi vijavyo,” ameongeza.

Aidha, Msajili amewataka viongozi wa kisiasa kutochukulia kwa uzito taarifa za upotoshaji zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii, akieleza kuwa uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa.

“Mtaambiwa uchaguzi haupo, msikate tamaa. Uchaguzi upo, na jambo kubwa zaidi ni kuhakikisha tunaingia kwenye uchaguzi huru na wa haki kwani ninyi ndio wakala wa kwanza wa kuhakikisha hilo linatekelezeka,” amehimiza.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatibu, alikumbusha historia ya changamoto zilizojitokeza mwaka 2010 wakati sheria hiyo ilipoanza kutumika, ambapo baadhi ya wagombea walijaza taarifa za uongo na risiti za kughushi.

“Changamoto hizo zilionekana kwa sababu ya uelewa mdogo, lakini leo tunatarajia kupata elimu ya kutosha ili kuhakikisha kasoro hizo hazijirudii,” amesema Khatibu.

spot_img

Latest articles

DCEA yakamata Lita 66,048 za kemikali bashirifu

NA MWANDISHI WETU MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ((DCEA), imefanikiwa kukamata...

Chevron yaonesha nia ya kuwekeza Tanzania katika sekta ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia

Na Mwandishi Wetu KAMPUNI kubwa ya nishati kutoka Marekani, Chevron Corporation imeeleza utayari wake wa...

Jumba la maajabu laiponza Yanga,  yapigwa faini  milioni 30,  Meneja  matatani

Na Mwandishi Wetu KLABU ya Yanga imetozwa faini ya Sh 30 milioni  kwa kosa la...

Waziri Ndejembi atoa maelekezo mazito utekelezaji wa mradi Malagarasi MW 49.6 KIGOMA

📌Hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mkandarasi kwenye mradi 📌Aagiza ukaguzi maalum wa matumizi ya...

More like this

DCEA yakamata Lita 66,048 za kemikali bashirifu

NA MWANDISHI WETU MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ((DCEA), imefanikiwa kukamata...

Chevron yaonesha nia ya kuwekeza Tanzania katika sekta ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia

Na Mwandishi Wetu KAMPUNI kubwa ya nishati kutoka Marekani, Chevron Corporation imeeleza utayari wake wa...

Jumba la maajabu laiponza Yanga,  yapigwa faini  milioni 30,  Meneja  matatani

Na Mwandishi Wetu KLABU ya Yanga imetozwa faini ya Sh 30 milioni  kwa kosa la...