MIAKA 10 ya mwanzo ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini, kati ya 1992 hadi 2012, kulikuwa na ‘tusi’ la jumla lililokuwa linaelekezwa kwa vyama vya upinzani. Hili lilikuwa ni kuvibatiza ‘vyama vya msimu’. Vilikuwa vinaitwa vyama vya msimu kwa sababu kuu moja. Kwamba vilikuwa vinaonekana tu wakati wa uchaguzi. Baadhi vilipambana na kufura sura iliyokuwa wamebandikwa. Vikageuka kuwa washindani wa kweli wa chama tawala.
Mwaka huu taifa linakwenda kufanya uchaguzi mkuu wa saba. Kwa vigezo vyovyote vile, kufanyika kwa uchaguzi mkuu mara saba siyo jambo dogo. Iwe huko nyuma ulitawaliwa na rafu, hila au uhalali, ni jambo kubwa hata katika hali yoyote iliyotokea. Uzoefu uliopatikana katika msingi huu umeacha somo kwa vyama vya siasa, wanasiasa na wananchi kwa ujumla wao.
Kama uchaguzi huu ungelikuwa ni kipimo cha kutafakarisha wananchi kuhusu siasa na wanasiasa wetu, basi ungetumika kama kipimo cha kusaidia nchi hii kujenga mustakabali mwema wa taifa kisiasa na kiutawala.
Tangu dirisha la uchukuaji wa fomu za kuwania urais lilipofunguliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Agosti 9, mwaka huu, hadi Jumanne wiki hii ni vyama sita ambavyo wagombea wao wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walikuwa wamefika kuchukuwa fomu za kuwania nafasi hiyo.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na INEC ilisema kuwa vyama 14 kati ya 18 ambavyo vilisaini maadili ya uchaguzi vilikuwa vimewasilisha barua ya kusudio la kuchukua fomu ya urais, na kueleza kuwa orodha hiyo ingeliweza kuongezeka. INEC ilitoa ratiba ikionyesha tarehe na muda wa wagombea wa vyama hivyo kwenda kuchukua fomu.
Vyama ambavyo wagombea wao wamekwisha kuchukua fomu hadi Jumanne ni Chama Cha Mapinduzi (CCM); National Reconstruction Alliance (NRA); Alliance for Africa Farmers Party (AAFP); Chama cha Makini; United Peoples’ Democratic Party (UPDP); na National League for Democracy (NLD).
Kuna uwezekano kwamba orodha hii itaongezeka. Vyama vingi zaidi vitajitokeza kuwania nafasi hizo. Wakati umma ukisubiri kuona mwaka huu ni vyama vingapi vitasimamisha mgombea urais, jambo muhimu la kujiuliza ni kwamba ni kwa kiwango gani baadhi ya vyama vinachukulia suala la uchaguzi kama jambo makini ambalo linabeba hatma ya taifa letu.
Awali nilisema kwamba kuna ‘tusi’ lilikuwa limeelekezwa kwa vyama vya siasa hasa miaka ya mwanzo ya mfumo wa vyama vingi nchini. Hili ni lile la kuviona baadhi ya vyama kama taasisi ambazo zinaonekana kwa msimu tu, aghalabu wakati wa uchaguzi.
Ni kwa maana hii, miaka mitano inaweza kupita bila kusikia baadhi ya vyama vya siasa vikifanya au kusema lolote. Hutasikia vikijijenga – siyo kutafuta wanachama wapya, siyo kufungua matawi, wala siyo kufanya mikutano ya hadhara ya kujitangaza. Kwa kifupi havifanyi chochote. Muhula wa uchaguzi wa miaka mitano unapita ndipo utavisikia tena vyama hivi vikiibuka.
Ninafahamu kwa yakini kabisa kwamba kushiriki katika uchaguzi wa nafasi za kisiasa katika nchi ni haki ya kikatiba ya vyama vya siasa. Kadhalika, ninatambua kuwa kuanzisha chama vile vile ni haki ya kila raia wa Tanzania, kwa maana hiyo hata kama vikiwa mamia kwa mamia, ni haki vikiandikishwa alimradi vinakidhi vigezo vya sheria ya vyama vya siasa.
Pamoja na kutambua haki hii, lipo suala la kujiuliza. Kwamba hivi hawa wanaoanzisha vyama vya siasa, wanapata usajili, wanaendelea kukaa hivyo hivyo, na uongozi ule ule, hawajawahi kushinda nafasi yoyote ya kuchaguliwa, siyo ya mjumbe wa serikali ya mtaa, au mwenyekiti wa serikali ya mtaa au mwenyekiti wa Kijiji, au ya diwani, au ya mbunge, hivi wanapata wapi ujasiri wa kutamani urais?
Yaani chama ambacho hakionekani kokote mtaani, kikifanya chochote, kikihamasisha chochote, kinasukumwa na nini kutamani urais? Yaani urais umefanywa jambo la mzaha sana au siasa ndiyo imegeuzwa mzaha?
Kama taifa tunaweza kudhani kwamba watu wanaofanya masihara na siasa hawana madhara kwa ustawi wa nchi yetu. Ukweli ni kwamba masihara haya ndiyo yamesababisha jamii kuona kuwa siasa ni jambo la utani utani, na kwa maana hiyo hawaichukulii kwa umakini unaotakiwa.
Matokeo ya hali hii ni kuendelea kuruhusu hali ya masihara katika uendeshaji wa siasa zetu. Kwamba matendo haya yanawafanya wananchi kuona kuwa siasa ni mchezo tu wa kuigiza. Ni jambo ambalo siyo la kuchukuliwa kwa umakini mkubwa. Kwamba siasa inaweza kufanywa kwa mizaha mizaha tu. Mizaha kama hii ambayo kwa muda sasa imeachwa mpaka imeota mizizi. Chama kinasajiliwa, kinaachwa tu, hakikui, hakiongezi idadi ya wanachama, hakisaidii wananchi kusukuma chochote katika uwajibikaji na utawala bora. Kipo tu, na msajili wa vyama vya siasa hana shida navyo.
Ninapotafakari yanayoendelea nchini kwetu, kila nikiona wanaojiorodhesha kwenda kuchukua fomu za kuwania urais, ninapata tabu sana kuafiki nafsini mwangu kama kweli malengo ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini ni haya ya sasa ya kuendeleza usanii wa watu wanaotumia vyama vya siasa kama mzaha na siyo njia ya kusaidia kuongeza na kusukuma umakini, uwajibikaji na utawala bora katika nchi.
Bila kutaja baadhi ya majina ya vyama vya siasa, hasa ile orodha ya vyama 19 vilivyosaini maadili ya uchaguzi, unaposikia majina yake ukaona viongozi wake, ukasikia wanachosema na kuahidi eti endapo watachaguliwa watafanya, unaelewa fika kabisa taifa letu limeacha mizaha mibaya kutawala siasa zetu, ndiyo maana wakati mwingine kusukuma ajenda ya uwajibikaji na utawala bora nchini imekuwa ni kazi ngumu mno.
Ninatafuta mtu wa kunisaidia kuwaambia baadhi ya wanasiasa, hasa wale waliobatizwa jina la vyama vya msimu, kuelewa kwamba mizaha yao katika siasa ni maafa kwa ustawi wa taifa letu.