Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imekamata shehena ya dawa mpya ya kulevya aina ya mitragyna speciosa tani 18.5 iliyokuwa ikiingizwa nchini kama mbolea.
Dawa hizo zimekamatwa zikiwa zimefungwa kwenye mifuko 756 ndani ya kontena kwa ajili ya kufungashwa upya na kutafutiwa soko ndani na nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo Agosti 13, 2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa, katika tukio hilo watuhumiwa saba wamekamatwa, wawili kati yao ni raia Sri – Lanka ambao ni Jagath Prasanna Madduma Wellalage (46) na Santhush Ruminda Hewage (25).
Amewataja watanzania waliokamatwa kuwa ni Riziki Shawej (40), Andrew Nyembe (34), Mariam Mgatila (40), Ramadhan Said (57) na Godwin Maffikiri (40).
“Dawa hizi zilikuwa kwenye kontena lenye ukubwa wa futi 40, zikitokea nchini Sri – lanka. Hii ni mara ya pili kukamatwa kwa aina hii ya dawa mpya ya kulevya, ambapo mwezi Juni mwaka huu, tulikamata mifuko 450 yenye zaidi ya uzito wa tani 11.5 za dawa hiyo mpya ya kulevya aina ya mitragyna speciosa iliyoingizwa nchini kama mbolea ikiwa kwenye kontena lenye ukubwa wa futi 20 ikitokea nchini Sri – Lanka ikiwahusisha watajwa hapo juu. Hivyo, kufanya jumla ya kilogramu 30,082.03 sawa na tani 30 za dawa hizo kukamatwa kwa kipindi kifupi hapa nchini,” ameeleza.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa, Mitragyna Speciosa ni dawa mpya ya kulevya (New psychtropic Substance-NPS) inayotokana na mmea unaofahamika kwa jina la kratom ambao hupatikana zaidi katika nchi za Kusini Mashariki mwa Bara la Asia.
Amesema,dawa hiyo ya kulevya ina madhara sawa na dawa za kulevya jamii ya afyuni (Heroin, Morphine).
“Dawa hii huathiri mfumo wa fahamu pamoja na kusababisha uraibu na vifo vya ghafla. Kutokana na kuongezeka matumizi ya dawa ya mitragym speciosa duniani, pamoja na madhara yanayosababishwa na sumu zilizomo katika dawa hii, nchi nyingi duniani zimezuia uzalishaji, usafirishaji na matumizi yake,”
Vilevile, Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa, ukamataji wa dawa hizo ni ishara ya kuwepo kwa changamoto mpya katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.