JUMATANO ya Agosti 6, 2025 Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alitangaza kifo cha aliyekuwa mtangulizi wake kwenye kiti hicho, Job Yustino Ndugai, ambaye pia alikuwa mbunge wa Kongwa kwa miaka 25 mfululizo tangu mwaka 2000 kwa tikiti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Tangu kutangazwa kwa kifo cha kiongozi huyu aliyeongoza moja kati ya mihimili mitatu ya madaraka ya dola tangu mwaka 2015 hadi Januari 2022, kumekuwa na mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii. Mijadala hii imeonyesha mitazamo kinzani juu ya maombolezo ya kiongozi huyu.
Binafsi nimesikiliza na kusoma maoni ya watu wengi yakiwakilisha hisia zao kama tanzia kwa Marehemu Ndugai. Makundi haya yamegawanyika katika sehemu mbili, wapo wanaompopoa mawe marehemu na wapo wanaoomboleza kwa huzuni na kumlilia. Binafsi nimejitafakari sana kama ninaweza kuandika tanzia ya Ndugai bila kujeruhi au kuudhi watu au kuwa miongozi mwa makundi mawili yanayokinzana.
Kwanza nami niungane na wote kutoa salama zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa Marehemu Ndugai. Ninajua Ndugai alikuwa na familia kama mume, baba, babu au hata kaka, analiliwa na ndugu zake. Ni dhahiri ndugu hawa wamepoteza mwanafamilia muhimu katika maisha yao. Ni utu na ubinadamu kuwahurumia wafiwa wote. Hivyo nawapa mkono wa pole, na kuomba Mola ampumzishe Marehemu mahali pema peponi.
Ninaandika tanzia hii nikiwa nimepata somo gumu sana juu ya maisha yetu wanadamu. Somo hili linatokana na ujumbe katika mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha Ndugai. Katika zama tunazoishi sasa, hakuna mwenye hatimiliki na taarifa. Kila mtu anao uwezo wa kusambaza taarifa kwa yeyote. Maendeleo ya tekinolojia ya habari na mawasiliano yakisukumwa sana na mawasiliano ya kidijitali, yamemfanya kila aliyeunganishwa kwenye mfumo huo, kuwa na fursa ya kusambaza chochote alicho nacho.
Ni katika kusoma, kutazama na kutafakari baadhi ya yaliyowasilishwa kwenye mitandao ya kijamii, nimejikuta nikiwaza mara mbilimbili kama ninastahili kweli kuandika tanzia hii au la. Pamoja na kujihoji sana, nimesukumwa kuandika ili nami niwe sehemu ya Watanzania waliosema kitu baada ya kifo cha Ndugai.
Katika maandiko ambayo nimeyapitia yakiwa ni ujumbe kwa ajili ya msiba wa Ndugai ni pamoja na wa Profesa Anna Tibaijuka almaarufu kama Mama T, ujumbe wa Askofu Benson Bagonza na ujumbe wa Majid Mjengwa. Nimeamua kutaja hawa watatu kwa sababu kuu moja, wote wameonyesha kuguswa kwanza na kifo cha Ndugai, lakini zaidi juu ya hisia na ujumbe wa watu mbalimbali juu ya matendo ya marehemu wakati wa uhai wake.
Kwa mfano, Mama T ameonyesha dhahiri kwamba mashaka mengi ambayo alikutana nayo Ndugai akiwa Spika na ambayo ndiyo yamekuwa mzizi wa baadhi ya watu kumshambulia badala ya kumlilia, yalisukumwa kwake. Alikuwa anatekeleza maagizo. Mama T anasema haya kama ushuhuda binafsi unaotokana na mazungumzo yake na Marehemu Ndugai.
Ama kwa Mjengwa, ameonyesha kushtushwa na mwelekeo mpya wa utu kutoweka katika kuomboleza miongoni mwa jamii ya Kitanzania. Aidha Mjengwa anaonyesha picha ya Ndugai kama kiongozi na mtu rahimu.
Pengine ujumbe wa Askofu Bagonza kuhusu kifo cha Ndugai ndiwo umenitafakarisha zaidi. Askofu anajenga hoja kwa nini watu wanaomboleza kifo cha Ndugai kwa staili hiyo. Anasema kuna uchuro katika taifa. Anajenga hoja akisema kuwa kuna kitu kisicho cha kawaida katika taifa letu akirejea mambo kadhaa. Moja, anaeleza kuwa akifa mwanasiasa kutoka chama tawala, watu wanashangilia na kukejeli; akifa kiongozi wa kitaifa au jamaa yake, watu wanashangilia; watumishi wa serikali kutoka idara fulani fulani zinazogusa masuala ya haki za watu, wakipata janga lolote, watu wanashangilia; watu wasio serikalini au kwenye siasa, lakini wana ukaribu na wanasiasa na viongozi wa serikali, wakipata majanga au misiba, watu wanashangilia; na viongozi wa dini, wa ukweli na wa uwongo (Mungu ajua), wakiwatabiria mabaya wanasiasa, wanaaminika. Lakini wakiwatabiria mazuri, wanatukanwa. Kwamba ni kama Mungu amemilikishwa kwa watu wenye chuki dhidi ya viongozi.
Tafakari ya Askofu Bagonza inafafanua kuwa hali hii inasababishwa na mifumo ya utoaji haki katika taifa kufunikwa na giza linalokatisha tamaa wanyonge; watu masikini na wanyonge kujaa hasira inayogeuka kuwa ukatili; kwamba sasa taifa limejijenga katika matabaka ya watawala na watawaliwa. Makundi haya yanakinzana. Moja lina uhakika wa kuishi na kutawala, jingine halina uhakika wa kuishi.
Binafsi mapema mwaka 2016 nikiwa na wenzangu tulipata fursa ya kuonana na Ndugai mjini Dodoma. Wakati huo, wanahabari wakifanya juhudi ya kuwasilisha mawazo yao juu ya muswada wa sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016. Ninakumbuka miongoni mwa mambo ambayo Ndugai alisema kwa moyo mzito kabisa, ni uamuzi wa kuzuia vikao vya Bunge kutangazwa moja kwa moja kwenye runinga.
Ndugai alisema wazi kwa lugha ya Kiingereza “This is going to be a very unpopular parliament.”
Tukiwa na wenzangu, tuliona jinsi uamuzi wa kuzuia ‘Bunge live” haukuwa uamuzi wa moja kwa moja wa Bunge kama muhimili unaojitegemea, bali yalikuwa ni maelekezo kutoka mahali fulani. Kwa maana hiyo, alichosema Mama T kwa kiasi, nami nilikisikia kutoka kinywani mwa Ndugai, mwaka 2016.
Tafakari hii inanisukuma kumzungumzia Ndugai kama mtu aliyebadilishwa kutoka alivyokuwa kabla ya kuwa Spika wa Bunge la 20, kuvaa alichovaa na hadi anabadilika kutoka kile alichosema Mjengwa kuwa mtu rahimu hadi wa aina ya hisia ambazo zimepamba kwenye mitandao ya kijamii. Akihusishwa zaidi na uvunjaji wa haki za wabunge wengine, kukiuka taratibu za Bunge, lugha za kibabe na kudhalilisha wengine hata kufikia hatua ya kujitangaza kwamba hakuna ‘mtu wa kumfanya lolote’ na ‘mtu yeyote asicheze naye.’
Kadhalika, hisia za watu juu ya kifo cha Ndugai zinaamsha tafakari muhimu juu ya mwenendo wetu kama taifa. Kwamba, kama haikuwa kawaida Watanzania kushangilia kifo au magumu yanayowakuta wenzao, sasa hivi ni nini hasa kimetokea kiasi cha kuanza kubadilika kwa hulka ya Kitanzania kuwa watu wa kushangilia mashaka ya wengine?
Wakati tukitafakari hali hii yafaa pia kujiuliza maswali ya msingi juu ya kile ambacho tunakiita Utanzania. Kwamba kwa hulka na hata kihistoria Watanzania ni watu waungwana, wanaosumbuliwa na shida za watu wengine; wanaolia na waliao pia kucheka na wachekao. Kama sasa hulka hii inatoweka kwa kasi hivi, ni muda wa kujiuliza ni nini hasa kimetokea? Nani huyo anayeshambulia hulka ya utu, huruma na upendo wa Watanzania kwa wenzao? Kwa nini inatokea sasa?
Yawezakana kabisa haya yaliyojitokeza kuhusu kifo cha Ndugai, ikawa ni wito kwa taifa hili kujitafakari kama kulikuwa na tunu – utu, undugu, huruma na maelewano, ni nini hasa kinazimomonyoa? Kuna mahali tulijikwaa, tuamke.


