Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimemtangaza Salum Mwalimu kuwa mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Uamuzi huo umetangazwa leo Agosti 7, 2025 na Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma, Benson Kigaila kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Amesema jina la Mwalimu lilipendekezwa na Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho yenye jukumu la kuleta mapendekezo ya jina la mgombea urais Tanzania na Zanzibar katika kikao kilichofanyika jana.

Baada ya kutangazwa mgombea urais chama hicho, Mwalimu amemteua Devotha Minja kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi mkuu.
Salum Mwalimu na Devotha ni wanasiasa waliojiunga na chama hicho mwaka huu wakitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambako waliwahi kuwa katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Katika hatua nyingine Chaumma kimeidhinisha rasmi ilani yake ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.