Na Tatu Mohamed, Dodoma
SHIRIKA la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) limewahimiza Watanzania kuachana na matumizi ya kuni na mkaa wa miti na badala yake kutumia mkaa unaotengenezwa kutokana na mabaki ya mazao mashambani, ili kulinda mazingira na kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Mhandisi Paul Josephat Kimati, kutoka TIRDO, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya Wakulima na Wafugaji kitaifa(Nanenane) yanayoendelea mkoani humo.
Mhandisi Kimati amesema kuwa TIRDO imefanya utafiti wa kina kufuatia Agenda ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu nishati safi ya kupikia, na kwamba mkaa unaotokana na mabaki ya mazao ni njia mojawapo ya kutimiza dhamira hiyo.

“Tumetafiti kwenye mabaki ya mazao mashambani, ikiwemo vifuu vya nazi, vifuu vya chikichi, maranda ya mbao, mabaki ya mpunga na magunzi ya mahindi. Vyote hivi vikitumika vizuri vinaweza kutoa mkaa wa ubora na gharama nafuu,” amesema Mhandisi Kimati.
Aidha, amesema mkaa huo si tu kwamba ni rafiki kwa mazingira, bali pia ni nafuu na unaweza kuzalishwa kwa kutumia teknolojia rahisi inayopatikana hapa nchini.
Ameongeza kuwa TIRDO ipo tayari kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali wanaopenda kujifunza kuhusu teknolojia hiyo, na kuwakaribisha katika ofisi zao kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo.

“Tunawaalika wafanyabiashara, wakulima na wadau wengine kutembelea banda letu hapa Nanenane ili wajifunze na kuona kwa macho yao teknolojia tunazotumia katika kuzalisha mkaa huu mbadala,” amesema.
Hatua hii ya TIRDO inakuja wakati ambapo nchi inaendelea kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala, kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti hovyo kwa ajili ya kuni na mkaa wa mawe.