Na Tatu Mohamed
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Athumani Kilundumya, ameipongeza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kuimarisha ushirikiano na sekta ya kilimo katika kuleta mapinduzi ya kidijitali, hatua inayochochea maendeleo katika sekta hiyo muhimu.
Akizungumza leo alipotembelea banda la e-GA kwenye Maonesho ya Kilimo na Mifugo (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Kilundumya ameeleza kuridhishwa kwake na jitihada za e-GA katika kujenga mifumo ya TEHAMA kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali chini ya sekta ya kilimo.
“Natambua jitihada za e-GA, ikiwemo ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa Mbolea kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA). Mfumo huu umeboresha usajili na utoaji wa leseni kwa wauzaji na wasambazaji wa mbolea, pamoja na kutambua maghala na kudhibiti soko la bidhaa hiyo muhimu,” amesema Kilundumya.
Ameongeza kuwa, kupitia mfumo huo, Serikali ina uwezo wa kudhibiti bei ya mbolea kwa kuzingatia ruzuku inayotolewa, hatua inayowawezesha wakulima kupata pembejeo kwa gharama nafuu na kuongeza tija shambani.

Aidha, ametaja taasisi nyingine zilizonufaika na ushirikiano na e-GA kuwa ni Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika, iliyoshirikiana katika ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika, na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa ujenzi wa Mfumo wa Usimamizi wa Shughuli za Umwagiliaji.
“Nimefahamu pia juu ya Mfumo wa eKilimo ambao unarahisisha utendaji kazi serikalini. Natamani kuona mfumo huu ukisaidia kupata taarifa hata za wakulima wadogo walioko vijijini. Imani yangu ni kuwa e-GA itaweza kulifanyia kazi hili tukileta mahitaji rasmi,” ameongeza Kilundumya.
Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Subira Kaswaga, amemshukuru Naibu Katibu Mkuu kwa kutembelea banda lao na kuahidi kuwa e-GA itaendelea kushirikiana na sekta ya kilimo katika kubuni na kuendeleza mifumo bunifu ya TEHAMA.

“e-GA imeendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo ili kuhakikisha mapinduzi ya kidijitali yanafika kwa wananchi wa mijini na vijijini kwa usawa,” amesema Kaswaga.
Maonesho ya Kilimo na Mifugo ya Nanenane kwa mwaka 2025 yanaendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, yakiwa na kaulimbiu isemayo ‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’.