Na Tatu Mohamed
VYOMBO vya habari nchini vimetakiwa kuwa makini katika kuripoti taarifa zinazohusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa kuhakikisha zinazingatia ukweli, wakati na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ili kulinda amani na mshikamano wa kitaifa.
Wito huo umetolewa leo, Agosti 1, 2025, na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegelege, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Tume na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

“Vyombo vya habari ni daraja kati ya Tume na wananchi. Mnapaswa kutoa taarifa zilizo sahihi, zisizopotosha na kwa lugha ya kujenga ili kuimarisha mshikamano wa kitaifa wakati wa uchaguzi,” amesema Jaji Mwambegelege.
Amebainisha kuwa Tume imeandaa mafunzo maalum kwa wahariri na waandishi wa habari yatakayofanyika Agosti 4, 2025, kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili kuripoti kwa weledi na kuzuia upotoshaji.

Amehimiza wanahabari kuhimiza uvumilivu wa kisiasa kwa wananchi na kuepuka lugha zinazoweza kuchochea vurugu wakati wa kampeni.
Amesema Tume imehusisha vyombo vya habari katika hatua mbalimbali za maandalizi ya uchaguzi ili kuongeza uwazi na kujenga uaminifu kwa wananchi.

Amebainisha kuwa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesajili jumla ya taasisi na asasi 164 kwa ajili ya kutoa elimu ya mpiga kura, na nyingine 88 kwa ajili ya uangalizi wa uchaguzi.
“Tushirikiane kuhamasisha wananchi, kuimarisha amani na kulinda mshikamano wa kitaifa,” amesema Jaji Mwambegelege.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa TAMWA na Mhariri kutoka Clouds Media Group, Joyce Shebe, amesema wanahabari wana wajibu wa kuelimisha jamii kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati ili kusaidia wananchi kufanya maamuzi bora.
“Elimu sahihi inasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi. Uwepo wetu hapa na Tume ni ishara kwamba tunajiandaa kuwaelimisha Watanzania kwa usahihi,” amesema Shebe.
Naye Mhariri wa Gazeti la Nipashe, Salome Kitomari, amesema mkutano huo umewapa wanahabari nyenzo muhimu kama sheria na miongozo ya uchaguzi, hatua itakayowawezesha kupeleka taarifa zilizo sahihi kwa umma.

Kwa upande wake, Kiondo Mshana kutoka Gazeti la Uhuru, amesema mafunzo kwa wanahabari yanapaswa kuwa ya mara kwa mara, siyo tu wakati wa uchaguzi, ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa kina kuhusu maadili ya uchaguzi.
