Na Mwandishi Wetu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga, limekamata boti aina ya fibre, iliyokuwa ikisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini Kenya kupitia Bahari ya Hindi.
Boti hiyo imekamatwa wakati wa operesheni ya Polisi usiku wa Julai 22,2025 katika eneo la Mawe Mawili, Kijiji cha Kwale, mpakani mwa Wilaya ya Mkinga na Jiji la Tanga.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi, amesema kuwa boti hiyo ilikamatwa na Kikosi cha Polisi Wanamaji, kufuatia taarifa za kiupelelezi na ufuatiliaji wa kina wa mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji haramu.

Kamanda Mchunguzi amesema watuhumiwa wawili waliokuwa kwenye boti walifanikiwa kutoroka baada ya kufika karibu na fukwe, lakini boti pamoja na shehena ya mirungi vilikamatwa.
Jeshi la Polisi mkoani humo limeeleza kuwa litaendelea kuimarisha doria na operesheni maalum hususan katika maeneo ya baharini ambayo yamekuwa yakitumiwa na wahalifu kuvusha bidhaa haramu kutoka nchi jirani.
Aidha, Kamanda Mchunguzi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu katika jamii, hasa vinavyohusiana na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.