Na Tatu Mohamed
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee katika kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya matumizi ya dawa bandia na duni, kwa kuwa vinaaminika na wananchi wengi.
Akizungumza Julai 16, 2025, wakati akifungua kikao kazi cha wahariri wa vyombo vya habari kutoka mikoa mbalimbali, kinachofanyika katika hoteli ya JB mjini Tabora, Chacha alibainisha kuwa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari ndiyo silaha muhimu katika kuzuia bidhaa hatarishi kuingia na kusambaa sokoni.
Amesema kazi ya TMDA ni ya msingi kwa usalama wa wananchi, lakini mafanikio yake hayawezi kuwa makubwa iwapo wanahabari hawatashiriki kikamilifu kuibua, kuelimisha na kufuatilia taarifa zinazohusu ubora wa bidhaa za afya.

“Nyinyi ndio jicho na sauti ya jamii. Kupitia kalamu zenu, watu wanaelewa hatari ya dawa bandia na kujua hatua za kuchukua wanapokutana nazo,” alisema Chacha huku akiwataka waendelee kushirikiana na TMDA.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, alisema kikao hicho kinalenga kuwajengea wahariri uelewa mpana kuhusu majukumu ya TMDA, mafanikio yaliyofikiwa na mikakati ya kukabiliana na bidhaa hatarishi.
Alisema mafanikio ya TMDA yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano mzuri na vyombo vya habari, na kwamba sasa huduma nyingi zimetolewa kwa njia ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na usajili wa bidhaa na utoaji wa vibali ndani ya saa 24.

Kikao hicho cha siku mbili kinawakutanisha wahariri na waandishi kutoka mikoa ya Kanda ya Magharibi, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuripoti habari za afya kwa usahihi na weledi, katika kupambana na changamoto ya bidhaa duni na bandia nchini.