IJUMAA ya wiki iliyopita yaani Juni 27, 2025 Rais Samia Suluhu Hassan aliweka historia kwa kutoa hotuba yake ya kwanza ya kuvunja Bunge. Alitangaza kuwa Bunge la 12 ambalo lilichaguliwa mwaka 2020 litafika ukomo wake Agosti 3, mwaka huu. Hili ndilo Bunge lililochaguliwa sambamba na kuchaguliwa kwa kipindi cha pili kwa Rais John Magufuli Oktoba mwaka 2020. Safari ya uongozi ya Magufuli iliishia njiani Machi 17, 2021 alipofariki dunia katika hospitali ya Mzena na badala yake Samia wakati huo akiwa Makamu wa Rais akachukuwa nafasi ya urais na kuapishwa Machi 19, 2021.
Kwa hiyo, hotuba ya Ijumaa iliyopita ilikuwa na umuhimu wa kipekee kwa Rais Samia. Walau kuna mambo mawili ya kuifanya hotuba hiyo kuwa na umuhimu wa kipekee. Mosi, ni hotuba yake ya kwanza ya kuvunja Bunge; pili, ni hotuba ya kuhitimisha ngwe ya kwanza ya utawala wake ambao itakapotimu Oktoba mwaka huu, atakuwa amekaa madarakani kwa muda wa miaka minne na miezi kama minane hivi. Tatu, ilikuwa ni hotuba ya kutathmini utawala wake kama Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Binafsi tathmini yangu inaonyesha kwamba aliitendea haki fursa aliyopata ya kuhutubia Bunge. Alitumia muda wa saa tatu kueleza safari ya utendaji na utekelezaji wa majukumu ya utawala wake tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ilikuwa ni hotuba iliyojaa takwimu za sekta mbalimbali za uchumi nchini, huduma za kijamii ambazo zilijaa ulinganisho wa wapi aliikuta nchi na ni wapi ameifikisha.
Nitaje baadhi ya takwimu alizomwaga Rais Samia, ijapokuwa nyingi ya takwimu hizi zilikwisha kutajwa na mawaziri, Rais aliingia kwa kina sana kwenye eneo la mikopo na deni la taifa. Alisema deni la taifa kwa sasa ni Sh trilioni 107.7, kati ya hizo deni la nje ni Sh. trilion 72.94 na la ndani ni Sh. trilioni 34.76. Alichukuwa muda mrefu kufafanua sababu za kuendelea kupaa kwa deni hilo. Moja ni madeni ya mikopo mipya iliyochukuliwa na serikali ya awamu ya sita kugharimia miradi ya maendeleo, lakini pia kutokana na mikopo iliyosainiwa na serikali zilizopita, lakini fedha zake ziliingia wakati wa sasa. Aidha, alisema kuwa kuzidi kuimarika kwa dola ya Marekani dhini ya sarafu ya Shilingi kati ya mwaka 2021 hadi 2025 imesababisha deni la nchi kupaa kwa Sh. trilioni 3.9.
Alitaja kuwa kuiva kwa riba za dhamana za serikali, kurekebisha madeni yaliyokopwa huko nyuma kwenye mifuko ya hifadhi za jamii, kutambua madeni ya wastaafu wa iliyokuwa PSPF kabla ya mwaka 1999 na madeni mengine yalikopwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Ukumbi wa Bunge, yote kwa pamoja vimesababisha kutuna kwa deni la taifa.
Hotuba hiyo iliyogusa maeneo mengi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka chini ya milioni moja mwaka 2021 na sasa zaidi ya watalii milioni tatu, ongezeko la makusanyo ya ndani kutoka Sh. trilioni 1.51 kwa mwezi mwaka 2020/21 hadi kufikia Sh. trilioni 3.09 kwa mwezi mwaka 2025. Pato ghafi la taifa nalo limeongezeka kutoka Sh. trilioni 156.4 mwaka 2021 hadi Sh. trilioni 205.84 mwaka 2024, huku pato la mwananchi likipanda kutoka Sh. 2,327,411 hadi Sh.2,938,634. Mfumuko wa bei nao ukishuka chini ya asilimia tano kwa miaka minne mfululizo, mauzo ya nje yakiongezeka kuingiza dola za Marekani bilioni 8.7 mwaka jana, kutoka Dola za Marekani bilioni 6.39 mwaka 2021.
Aligusia mafanikio katika kuwa na hifadhi ya fedha za kigeni Dola za Marekani bilioni 5.6 zinazoweza kumudu ununuzi wa bidhaa na huduma kwa miezi 4.5; kununua dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kiasi cha tani 4.424 kwa gharama ya Sh. bilioni 702.3. Alitaja mafanikio mengine mengi katika kujenga bandari mpya, ununuzi wa ndege mpya sita za ATCL, kufikisha umeme katika vijiji vyote 12,318 vya Tanzania na sasa juhudi ni kufikisha umeme kwenye vitongoji vyote 64,359 huku tayari umeme ukiwa umefikia vitongoji 33,657 sawa na asilimia 52.3. Alieleza mafanikio kwenye ujenzi wa madaraja makubwa tisa, yakiwamo ya Wami, Tanzanite, Kitengule na John pombe Magufuli aka Kigogo- Busisi na mengine. Ongezeko kubwa la urefu wa barabara za lami na changarawe.
Katika muda wa saa tatu alizosimama Rais Samia alikuwa anatoa takwimu mbalimbali za kila sekta. Kwenye idadi ya ajira, ongezo la bajeti kwenye sekta ya kilimo, kuboresha makazi ya askari wakiwamo wanajeshi, kuunganisha mikoa yote sasa kwenye umeme wa gridi ya taifa, ongezeko la idadi ya majaji wanawake- akieleza kuwa kati ya majaji 68 wa mahakama kuu alioteua 30 ni wanawake na kati ya majaji 15 wa mahakama ya rufani alioteua wanne walikuwa wanawake.
Ni vigumu kueleza hapa takwimu zote za mafanikio ambazo Rais alieleza. Alidurusu kila sekta kwa kina. Aliwasilisha idadi ya majengo mapya, ajira mpya, ongezeko la bajeti na kuboreshwa kwa mitaala ya elimu kwa kina.
Katika kazi yote iliyomchukua Rais muda wote huo, aligusia habari ya watu kupotea pia. Baada ya kusifu kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kuzuia uhalifu kwa kiwango kikubwa, huku alieleza eneo ambalo mafanikio hayajapatikana sana kuwa ni eneo la ajali za barabarani. Ni katika kuzungumzia Jeshi la polisi alisema: “Ninalielekeza Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukomesha matukio ya watu kupotea.”
Maagizo haya ya Rais yaliwafanya wabunge kugonga meza kwa kitambo kidogo kuashiria kuunga mkono maelekezo hayo dhidi ya matukio ya kupotea kwa watu. Matukio ya kupotea kwa watu kimsingi yamechafua taswira ya nchi, ndani na nje. Yameifanya Tanzania kutambuliwa kama nchi ambayo raia wake wanaweza kupotea hivi hivi tu na vyombo vya usalama, kama polisi wasifanye lolote. Matukio haya yamekuwa ni tatizo. Tena tatizo kubwa.
Ukimsikiliza Rais Samia katika hotuba yake na mafanikio ya utawala wake wa miaka minne na ushei aliyoelezea kwa takwimu halisi, naye akisema wazi, mwenye kutaka kutikisa mafaniko ya serikali yake, aje na takwimu za kuthibitisha vinginevyo. Kwa kauli hiyo, Rais alijua wazi kwamba takwimu haziongopi. Alijua wazi, kwamba kila takwimu alizotaja zilionyesha alikotoa nchi na ni wapi ameifikisha. Kwenye kila sekta, kila nyanja. Ni mafanikio juu ya mafanikio.
Katika sura ya mafanikio haya, swali moja linasumbua sana. Ni nani hasa ananufaika na matukio ya kupotea, kutekwa na kuuawa kwa raia? Ni akina nani hasa walioko nyuma ya matukio haya. Hii ni mara ya pili Rais anatoa maelekezo juu ya matukio haya. Alitoa maelekezo ya kufanyika kwa uchunguzi wakati wa mauaji ya kada wa Chadema, Ali Kibao, ambaye alitekwa mchana kweupe kutoka kwenye basi la Tashriff akielekea Tanga. Watekaji wake walidaiwa kuwa na sihala zinazofanana na zile zinazotumiwa na vyombo vya usalama vya nchi yetu. Mzee wa watu alikutwa kesho yake akiwa maiti na mwili wake ukiwa umeharibiwa sana usoni kana kwamba alimwagiwa tindikali.
Ni vigumu kuelezwa ni kwa nini katika mafanikio makubwa kama haya, waovu wa utekaji, upotezaji na mauaji ya watu wanaachwa kufanya matukio haya moja baada ya jingine, huku wakisababisha kuchafuliwa kwa rekodi njema ya mafaniko kama haya aliyoweka wazi Rais? Tutarajie nini baada ya maelekezo haya?