Na Mwandishi Wetu
Rais Samia Suluhu Hassan, ameliagiza Jeshi la Polisi nchini kuongeza jitihada katika kupambana na matukio ya uhalifu, hususan vitendo vya kupotea kwa watu, pamoja na kutafuta mwarobaini wa ajali za barabarani.
“Pongezi nyingi kwa Jeshi la Polisi kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya, hatuna budi kutambua kwamba uhalifu unaozuiliwa kwa jitihada za Jeshi la polisi ni mkubwa kuliko unaofanyika. Kasi ya kuwabaini na kuwakamata wahalifu na kuwafikisha mahakamani imeongezeka. Jambo ambalo bado hatujafanikiwa vyakutosha ni ajali za barabarani lazima nazo tuendelee kuzitafutia mwarobaini wake. Aidha naliekeza jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kumesha matukio ya watu kupotea,”
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Juni 27, 2025 wakati akilihutubia katika kuhitimisha shughuli za la 12, jijini Dodoma.

Katika hatua nyingine amebainisha kuwa mchakato wa Katiba mpya unatarajia kuanza kipindi kijacho cha miaka mitano kwa sababu ni miongoni mwa ahadi zinazoonekana katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2025/2030.
Ameeleza kuwa asasi za kiraia zimekuwa huru kufanya shughuli zao ikiwemo kukutana na kushauri Serikali na mapendekezo yao mengi yamepokelewa na kufanyiwa kazi.
Kuhusu kuongezeka kwa deni la Taifa, Rais Samia ameeleza kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka ni kutokana na fedha ambazo zilikopwa na awamu zilizopita kupokelewa na awamu hii ya sita, pamoja na kuimarika kwa dola ya Marekani jambo linalochangia kukua kwa deni la nje.

“Hadi kufikia Mei 2025 deni la Serikali lilifikia trilioni 107.7, kati ya deni hilo deni la nje ni shilingi trilioni 72.94 na deni la ndani ni 34.76. Kuongezeka kwa deni la Serikali kumetokana na sababu mbalimbali, mojawapo ni kupokelewa kwa fedha za mikopo mipya na ya zamani ambayo mikataba yake iliingiwa tangu Serikali za awamu za nyuma.
“Ni vyema tukafahamu kuwa mkopo unaweza kusainiwa leo lakini fedha husika zikaanza kupokelewa baada ya maandalizi ya mradi kukamilika na mradi kuanza ili lile deni au mkopo huo uingie kwenye deni la serikali lazima serikali iwe imepokea fedha hizo huduma au vifaa tulivyokubaliana,”

“Katika awamu ya sita pamoja na kusaini mikopo mipya lakini pia tumeendelea kupokea fedha za mikopo ambayo ilisainiwa katika vipindi tofauti na kuongeza kiwango cha deni la Serikali kwa mfano awamu ya sita imepokea kiasi cha shiilingi trilioni 11.3 ikiwa ni mikopo iliyosainiwa na awamu zilizopita.
Rais Samia ameeleza kuwa mwaka huu deni limeongezeka kwa zaidi sh 3.9 trilioni kutokana na ‘exchange rate’.

“Mfano mwezi Machi 2021 kiwango cha kubadilisha shilingi ya kitanzania dhidi ya dola za marekani ilikuwa shilingi 2,298.5 wakati mwezi Machi mwaka huu kiwango hicho kulikuwa 2,650 hivyo endapo deni la Serikali litatajwa kwa shilingi za kitanzania lazima lionekane limeongezeka,”
Akielezea mafanikio katika kipindi cha Serikali ya awamu ya sita, amesema uhuru wa vyombo vya habari na kutoa maoni umeongezeka kutokana na kukua kwa matumizi ya mtandao.