Na Winfrida Mtoi
Watoto 295 wenye umri chini ya miaka 12,wamejitokeza katika mashindano ya mchezo wa kuogelea ya Taifa ambapo Chama cha Mchezo huo Tanzania (TSA), kimesema idadi hiyo ni rekodi mpya kwani haijawahi kutokea.
Mashindano hayo ya siku mbili yameanza leo Juni 14, 2025 na yanamalizika kesho katika Bwawa la Kuogelea la Shule ya Kimataifa ya Tanganyika(IST), Masaki Dar es Salaam, yakishirikisha klabu 18.
Akizungumzia mashindano hayo, Mwenyekiti wa TSA, David Mwasyoge, amesema mwaka huu mwamko umekuwa mkubwa, hasa kutokana na watoto wengi wa kitanzania kujitokeza hali inayoonesha kupiga hatua kwa mchezo huo.

“Mwamko umekuwa mkubwa, wazazi pia wanahamasika na chama kinafanya kazi kubwa kwa kushirikiana na wadau. Ukiangalia miaka 10 hadi 15 iliyopita ilikuwa ukija katika mashindano kama haya asilimia 90 utakuta sio watoto wa kitanzania, lakini leo hii asilimia 100 ni watoto wa kitanzania hayo ni maendeleo makubwa,” amesema.
Ameeleza kuwa lengo ni kupata waogeleaji wengi zaidi na kuwapa wigo mpana makocha kuchagua timu ya Taifa kwa ajili mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Mkurugenzi wa Ufundi wa chama hicho, Amina Mfaume amesema watoto wanafanya vizuri na inaonekana jinsi makocha wanavyofanya kazi kwa sababu muda umekuwa ni mazuri kulingana na rekodi zao.

Amesema licha ya miundombinu kuwa michache wameendelea kufanya vizuri na kufikia malengo waliyojiwekea ya kukuza mchezo huo nchini, wakiangalia zaidi ushiriki wa watoto.
“Lengo letu katika mashindano haya ilikuwa ni watoto 250 lakini waliojitokeza ni 295, kwa hiyo tumepita lengo tunatarajia mwaka ujao tutafikisha 400. Ukiangalia katika mashindano haya mtoto mdogo zaidi aliyeshiriki ana miaka mitano, unaona jinsi gani swimming inakua,’’ amesema Amina.