CCM yatangaza kufufua mchakato wa Katiba mpya

*Askofu Gwajima apigwa kitu kizito

Na Mwandishi Wetu

WAKATI joto la uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 likizidi kupanda, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimezindua ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2025-2030 ambayo sasa inatamka wazi kwamba inakwenda kuhuisha mchakato wa katiba mpya.

Mchakato wa Katiba mpya ambao ulianza mwaka 2014 chini ya utawala wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, ulikwama kabla ya kumalizika huku awamu ya utawala huo ikifikia mwisho. Ilitarajiwa kwamba awamu ya tano iliyoingia madarakani mwaka 2015 chini ya utawala wa Rais John Magufuli, ungeukamilisha.

Hata hivyo, Rais Magufuli siyo tu kwamba hakutaka kabisa kukamilishwa kwa mchakato huo, bali pia alisema wazi kwamba hakuna kokote katika kampeni zake za uchaguzi wa mwaka 2015 aliahidi katiba mpya. Badala yake, aliendesha uatwala wake kwa staili iliyopendelea zaidi kujirundikia madaraka na kuweka vigingi vingi dhidi ya utawala wa kidemokrasia ya vyama vingi.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan.
Askofu Josephat Gwajima, Mbunge wa Jimbo la Kawe.

Kwa hali hiyo, mchakato huo ulikwama kwa zaidi ya miaka 10, juhudi mbalimbali za kuunasua hata alipoingia madarakani kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha Rais Magufuli, bado haupata mafanikio yoyote.

Ingawa Bunge la Katiba lilifikia hatua ya kupatikana kwa Katiba Pendekezwa, wajumbe wa vyama vya upinzani walisusia hatua ya kupigwa kura wakilalamika kuwa Rasimu ya Katiba Pendekezwa ya Tume ya Katiba ilioongozwa na Jaji Joseph Warioba, ilichakachuliwa na wajumbe wa CCM. Ususiaji huo ndio ulizaa kile kilichokuwa kuja kuwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ukiviunganisha vyama vya upinzani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambao Edward Lowassa aligombea urais chini yake na kuibua upinzani mkubwa dhidi ya mgombea wa CCM.

Ingawa mchakato wa Katiba wa mwaka 2014 ambao ulianzishwa na Rais Jakaya Kikwete haukuwa umetajwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010 – 2015, utashi binafsi wa Rais huyo ambaye pia alikuwa ni mwenyekiti wa chama tawala, ulipokewa kwa tahadhari kubwa.

Hata hivyo, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa alikuwa ameahidi kwamba kama angeshinda uchaguzi, ndani ya kipindi cha kifupi angeiwezesha Tanzania kupata katiba mpya. Hatua ya Rais Kikwete ‘kupoka’ sera hiyo, ilikuja kuonekana kama ilikuwa na nia ya kupoteza fursa ya taifa kupata katiba mpya, kwa kuwa moto wa kutaka katiba mpya ulikuwa umekolea, lakini mchakato aliouanzisha ulipoteza fursa hiyo kwa miaka zaidi ya 11.

Katika hatua za awali za kukusanya maoni ya wananchi juu ya katiba wanayoitaka, zikianza kujitokeza dalili kwamba wapo watu waliotamani kuendelea na Katiba ya Mwaka 1977 ambayo ndiyo inayotawala hadi sasa. Wengi walikuwa wanatuhumu mapendekezo ya Tume ya Katiba na kudai kuwa ilikuwa na nia ya kuvunja Muungano kwa kuwa ilikuwa inapandekeza muundo wa serikali tatu.

Katika ilani hii mpya, ambayo ndiyo inakwenda kutafuta ridhaa ya wananchi kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu, CCM inasema kwamba sasa inakwenda kuhuisha mchakato wa Katiba Mpya.

Mchakato wa Katiba Mpya umekumbwa na changamoto nyingi, miongoni mwake ni kauli kutoka kwa viongozi wenye dhamana serikalini, kwamba hatua muhimu kabisa ya kabla ya kuhuishwa kwa mchakato kwake ni kutolewa kwanza kwa elimu ya Katiba, ambayo ilikadiriwa kwamba ingelichukuwa muda wa miaka mitatu.

Pamoja na ahadi hiyo kwamba ingelitolewa elimu ya Katiba kwanza, sasa ni zaidi ya miaka mitatu imepita, mchakato wa elimu hiyo haujaanza.

Ilani hii pia imetangaza kuwekwa kwa mfumo wa kisheria wa kurasimisha falsafa ya Rais Samia ya R4 – Maridhiano (Reconciliation), Ustahamilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), kwani hadi sasa zilikuwa hazijajengewa msingi wa kisheria nchini.

Kuingizwa kwa falsafa ya R4 kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ni hatua mpya ambayo imepigwa tangu Rais Samia alipoibuka na dhana hizo, na kile ambacho binafsi alipata kukiri kwamba alikabiliwa na upinzani mkubwa ndani ya chama chake.

Kwa hatua hii mpya, kama kulikuwa na uhafidhina dhidi ya R4 ndani ya CCM sasa wenye kuvuta breki katika utekelezaji wa suala hilo, sasa itawalazimu kutafuta pa kutokea, kabla ya kutoshwa.

Wakati wanaCCM wakijipanga kwenda kurudi majiboni kutafuta nafasi za ubunge na madiwani kurejea kwenye kata zao, mtu ambaye hapana shaka amepigwa kikumbo kikubwa ni Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima, ambaye Rais Samia ameonyesha dhahiri kukerwa na hatua yake ya hivi karibuni ya kuitisha mkutano wa waandishi wa habari na ‘kuchafua’ hali ya hewa kutokana na kuzidi kushamiri wa vitendo vya watu kutekwa, kuteswa, kupotezwa na kuuawa.

Katika hotuba yake ya kufunga mkutano mkuu maalum mjini Dodoma baada ya kupitishwa kwa Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya mwaka 2025 – 2030, Rais Samia alitoa tahadhari kwa wajumbe wa akiwakumbusha kujiepusha na tabia ya Kigwajima, akiita Gwajimanisation, kwamba haifai. Alitamka wazi kwamba watu wa namna hiyo wasiruhusiwe kugombea ndani ya chama hicho kwa sababu siyo wenzao.

Kwa kumbora hili, Askofu Gwajima ambaye mwaka 2020 katika kura za maoni jimboni Kawe alikuwa wa tatu, lakini akabebwa kwa nguvu zote na Marehemu Magufuli, kama ana nia ya kuendelea na siasa za kurejea Bungeni baada ya kuvunjwa mwishoni mwa Juni, atalazimika kutafuta fursa hiyo nje ya CCM.

spot_img

Latest articles

Bodi ya wakurugenzi Ewura yatembelea miundombinu ya Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG)

Na Mwandishi Wetu BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati...

Wadau watoa tahadhari kuhusu Haki za Kidijitali kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Na Mwandishi Wetu MASHIRIKA mawili makubwa yanayojihusisha na haki za kidijitali ya Paradigm Initiative...

REA yahamasisha wananchi kutumia Mkaa Mbadala

📌Yasisitiza ni salama, gharama nafuu na ni rafiki wa mazingira 📌Yathibitisha kuendelea kuwawezesha wazalishaji wake WAKALA...

Serikali yasisitiza Dabi iko pale pale Juni 15

Na Mwandishi Wetu Wakati Yanga ikiendelea na kampeni yake ya ‘Hatuchezi’ Serikali imethibitisha rasmi kuwa...

More like this

Bodi ya wakurugenzi Ewura yatembelea miundombinu ya Gesi Asilia iliyoshindiliwa (CNG)

Na Mwandishi Wetu BODI ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati...

Wadau watoa tahadhari kuhusu Haki za Kidijitali kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025

Na Mwandishi Wetu MASHIRIKA mawili makubwa yanayojihusisha na haki za kidijitali ya Paradigm Initiative...

REA yahamasisha wananchi kutumia Mkaa Mbadala

📌Yasisitiza ni salama, gharama nafuu na ni rafiki wa mazingira 📌Yathibitisha kuendelea kuwawezesha wazalishaji wake WAKALA...