Wenye vyeti feki vya uandishi wa habari waonywa

Na Mwandishi Wetu, JAB

WAKATI Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) ikiufungua rasmi mfumo wa usajili wa Waandishi wa Habari wa https://taihabari.go.tz ili kuomba kuthibitishwa na kupatiwa Kitambulisho cha Uandishi wa Habari (Press Cards) Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Tido Mhando amewaonya wenye nia ya kutumia vyeti visivyo halali wakati wa kujaza taarifa zao.

Mhando ametoa tahadhali hiyo Mei 19, 2025 wakati akizungumza na Wahariri na Waandishi wa Habari wa vyombo mbalimbali vya Habari katika ofisi za Bodi hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri jijini Dar es Salaam.

“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, Bodi hii itaanza kutoa ithibati kwa waandishi wa habari wote kupitia mtandao na kutoa vitambulisho vya kidijiitali (digital Press Card). Maombi ya ithibati Press Cards yatafanyika kupitia Mfumo unaoitwa TAI-Habari,” amesema.

Mhando alisema mahitaji muhimu wakati wa kujaza taarifa katika mfumo huo kuwa ni pamoja na namba ya simu na barua pepe vinavyofanya kazi, picha ndogo (passport size) iliyoskaniwa barua ya utambulisho kutoka taasisi anayotoka au anakopeleka kazi zake ikiwa ni mwandishi wa kujitegemea (Freelancer), nakala ya Kitambulisho cha Taifa (NIDA) na ada ya ithibati shilingi Elfu Hamsini (50,000).

“Mahitaji mengine ni vyeti vya elimu vilivyoskaniwa kwa mfumo wa PDF na kuthibitishwa na Mamlaka husika (kama chuo kikuu vithibitishwe na TCU na kama ni vyuo vya kati vithibitishwe na NACTVET), na katika hili nisisitize tafadhali sana usiweke cheti ‘feki’ jambo hilo linakiuka siyo tu linakiuka maadili ya taaluma habari, bali pia ni makosa yanatakayodhibitiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi,” amesema Mhando.

Mhando amesema mahitaji hayo ni muhimu ili kukamilisha mchakato wa maombi kwa mafanikio na kwamba ni hatua inayolenga kuboresha huduma, kuimarisha usimamizi wa taaluma ya Uandishi wa Habari na kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho kwa waandishi waliothibitishwa.

Ameomba Wahariri, Waandishi na wadau wote wakiwemo waajiri kutambua umuhimu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari katika kuimarisha weledi, maadili, na uwajibikaji wa taaluma ya uandishi wa habari nchini, na hivyo watoe ushirikiano wa hali ya juu katika kukuza na kuendeleza taaluma hiyo muhimu kwa taifa.

Akijibu maswali ya waandishi wa Habari kuhusu watu walio kwenye tasnia bila kuwa na vyeti vya Elimu ya Uandishi wa Habari, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo Wakili Patrick Kipangula amesema Sheria ilitoa muda wa miaka mitano kwa watu waliokuwa hawana sifa ili wakasome na kutimiza vigezo vya kisheria.

Amesema baada ya muda huo kuisha Waziri aliongeza muda wa mwaka mmoja na kwamba tangu Waziri aongeze mwaka mmoja ni miaka miwili imeshapita na kufanya jumla ya miaka nane na hivyo hakutakuwa na muda wa nyongeza tena.

spot_img

Latest articles

Mkataba wasainiwa kuwezesha gesi kuzalisha mbolea

Na Tatu Mohamed, Media Brain KATIKA juhudi za kukuza uzalishaji wa ndani wa mbolea na...

Mafanikio 10 ya Wizara na Utalii

Na Mwandishi Wetu WIZARA ya Maliasili na Utalii  imebainisha vipaumbele 10 ambavyo wizara na...

Waziri wa Mazingira wa Norway ateta na Waziri Masauni

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mha. Hamad Masauni...

ASKARI JWTZ ASHIKILIWA NA POLISI KWA ULEVI

Na Mwandishi Wetu Jeshi la Polisi mkoani Morogoro  limemkamata Askari wa Jeshi la Wananchi wa...

More like this

Mkataba wasainiwa kuwezesha gesi kuzalisha mbolea

Na Tatu Mohamed, Media Brain KATIKA juhudi za kukuza uzalishaji wa ndani wa mbolea na...

Mafanikio 10 ya Wizara na Utalii

Na Mwandishi Wetu WIZARA ya Maliasili na Utalii  imebainisha vipaumbele 10 ambavyo wizara na...

Waziri wa Mazingira wa Norway ateta na Waziri Masauni

Na Mwandishi Wetu WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Mha. Hamad Masauni...