Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imefanikiwa kumkamata Danford Mathias, mkazi wa Chalinze, mkoani Pwani, kwa tuhuma za kutengeneza na kuchapisha vitambulisho bandia vya Taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 02, 2025 jijini Dar es Salaam, Msemaji wa NIDA, Geofrey Tengeneza, amesema kuwa kwa miezi kadhaa kumekuwa na ongezeko la vitendo vya udanganyifu ambapo watu hujitangaza kuwa wana uwezo wa kutoa huduma za NIDA na kuwatapeli wananchi.

“Operesheni maalum iliyoendeshwa kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi ilifanikisha kukamatwa kwa mtuhumiwa Aprili 23, mwaka huu, majira ya saa 9:00 Alasiri,” amesema Tengeneza.
Mtuhumiwa huyo alikamatwa katika studio yake inayojulikana kama Bwanga Studio iliyopo Msata, Chalinze, akiwa na vifaa alivyokuwa akitumia kutengenezea vitambulisho feki kwa malipo ya kati ya Shilingi 6,000 hadi 10,000.
Tengeneza ameeleza kuwa mtuhumiwa alikuwa akitumia kitambulisho chake halali cha NIDA kwa kukiscan na kisha kuhariri taarifa ndani ya programu ya Adobe ili kubandika taarifa za wateja.

Aidha, Tengeneza ametoa onyo kali kwa wamiliki wa maduka ya steshenari wasijihusishe kwa namna yoyote na utengenezaji wa vitambulisho bandia, akisisitiza kuwa hilo ni kosa la jinai linalokiuka Sheria ya Usajili na Utambuzi Sura ya 36 ya mwaka 2012 pamoja na Kanuni zake.
“Wananchi wanapaswa kuelewa kuwa vitambulisho halali hutolewa na NIDA pekee, na mara ya kwanza hutolewa bure. Kumiliki au kutengeneza kitambulisho feki ni kosa la jinai,” ameongeza.
Kwa upande mwingine, Tengeneza ametangaza kuwa kuanzia Mei 1, 2025, NIDA imeanza kufungia Namba za Utambulisho wa Taifa (NIN) kwa wale ambao waliarifiwa kuchukua vitambulisho lakini hawakufanya hivyo.

“Hii haimaanishi kuwa kitambulisho kimefutwa. Mtu akifika kuchukua kitambulisho chake, namba yake itahuishwa na kuanza kutumika tena,” amefafanua.
Amewataka wananchi wote, hata wale ambao hawajapokea ujumbe mfupi, kujitokeza kuchukua vitambulisho vyao katika ofisi za NIDA.