Na Mwandishi Wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema katika mchezo wa kesho wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ili kufuzu nusu fainali wanahitaji kushinda matatu lakini kwa mazoezi waliyofanya ni kwa ajili ya kufunga mabao zaidi ya manne.
Wekundu wa Msimbazi hao ambao mchezo wa kwanza ugenini walipoteza kwa kufungwa 2-0, kesho Aprili 9,2025 wanashuka dimbani kurudiana na Al Masry kutoka nchini Misri kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo kuelekea mchezo huo, Fadlu amesema lengo lao ni kupindua meza kwa kuwa Simba ni klabu kubwa Afrika na inataka mafanikio yakiwemo kutinga nusu fainali na ikishindikana atakuwa tayari kuwajibika.
“Tunahitaji mabao matatu ili kufuzu nusu fainali na hii wiki nzima tumefanya mazoezi walau tufunge mabao zaidi ya manne na sio matatu pekee,” amesema Fadlu.
Ameeleza kuwa katika kuhakikisha wanafanikiwa malengo yao katika mchezo huo anaweza kutumia washambuliaji wawili, huku wakiwa makini na wapinzani kuhusu kufanya mashambulizi ya kustukisha.