KATIKA miaka ya hivi karibuni serikali imefanya miradi mingi ya miundombinu hasa ujenzi wa stendi za mabasi. Kwa sasa mikoa mingi ina stendi mpya kubwa za kisasa ambazo zina uwezo wa kuhudumia mabasi mengi kwa wakati mmoja.
Nyingi ya stendi hizi zimejengwa pembezoni mwa miji kwa sababu ya kuendana na uhitaji wa nafasi kubwa ambazo ni nadra kuipata katikati ya mji. Mpango huu wa ujenzi wa stendi mpya unachukuliwa kama mkakati wa kupanga vema miji mikubwa nchini. Kwa mfano, mkoa wa Dodoma una stendi mpya kubwa ya kisasa, Mwanza nayo inazo stendi mpya kubwa mbili, Tanga hali kadhalika, Mbeya nako ipo, hata mkoa wa Pwani ambao kwa ujumla wake umeathiriwa sana na ukaribu wake na mkoa wa Dar es Salaam, wana stendi mpya pia.
Mkoa wa Dar es Salaam ambao kwa kawaida ndiyo kitovu cha biashara nchini, kihistoria umekuwa ukipokea mabasi mengi kila siku. Wakati huo huo mabasi mengine mengi kila siku yanaanza safari zake katika mji huo kwenda mikoa yote ya Tanzania. Kwa maana hiyo, Dar es Salaam ndiyo mkoa ambao ulihitaji kuwa na stendi kubwa na yenye huduma nyingi muhimu ili kurahisisha huduma kwa wasafiri.
Ni katika mkakati huo baada ya stendi kuu ya Ubungo jijini Dar es Salaam ambayo ilianza mwanzoni mwa miaka ya 2000, ilihamishwa. Stendi ya Ubungo ilianzishwa baada ya kuhamishwa kwa stendi zilizokuwa zimezagaa maeneo mengine ya mji kama Kisutu, Mnazi Mmoja na Msimbazi. Baada ya kuanza kwa ujenzi wa barabara za mabasi ya Mwendokasi, ilionekana eneo la Ubungo lisingeliweza kuendelea kuhimili huduma ya mabasi ya mikoani na huduma hii mpya. Moja ya sababu hizo ni stendi hiyo kupoteza uwezo wa huduma bora, lakini pia ongezeko kubwa la mabasi yanayoingia na kutoka kila siku. Kadhalika, uhitaji wa eneo hilo kwa ajili ya mtandao wa barabara za Mwendokasi ulilazimisha kuhamishwa kwa stendi hii.
Hali hii ililazimisha mpango wa miaka mingi wa kujengwa kwa stendi kubwa ya kisasa eneo la Mbezi Luis kuanza. Stendi hii inayobeba jina la Magufuli, ilijengwa kuanzia Januari 2019 na kukamilika mwishoni mwa mwaka 2020 kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 50.
Kilichofuata baada ya kukamilika kwa stendi hii kubwa kuliko zote nchini, ni kuhamishwa kwa stendi ya Ubungo na stendi nyingine ndogo ndogo (bubu) zilizokuwa zimezagaa maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri wa Ardhini (LATRA) ilitoa angalizo kwa mabasi yote yaliyokuwa yamepewa leseni kwamba ni lazima safari zake zianzie kwenye stendi hii.
Angalizo hili mwanzoni lilizingatiwa na wamiliki wa mabasi yote. Hata hivyo, katika siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la kampuni za mabasi kuhamisha ofisi zao kutoka Magufuli stendi kwenda ‘vichochoroni’ kila mmoja akijijengea kitu kinachofananishwa na stendi, lakini kiuhalisia siyo stendi zenye hadhi inayoweza kutoa huduma bora kwa abiria.
Kwa mfano, eneo la Urafiki jijini Dar es Salaam, zilikojengwa nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) zimezagaa ofisi za kampuni za mabasi, ambazo pia zinatumika kama stendi rasmi za mabasi yao. Ukifika eneo la Urafiki, licha ya kuonekana kama kero na vurugu, kila kampuni ya mabasi yenye ofisi pale anajaribu kulazimisha kuwa ni stendi rasmi, lakini kiuhalisia haina vigezo vya ubora kwa huduma kwa abiria.
Eneo hili, kwanza halikutengwa kwa ajili ya matumizi ya stendi, pili halina nafasi ya kuwezesha huduma hizo kupatikana hapo, lakini la tatu ambalo ni la umuhimu mkubwa, uwepo wa mabasi katika eneo hilo unaongeza msongamano wa magari pasi na sababu yoyote ya msingi. Hali hii ya wenye mabasi kung’ang’ania kurejesha stendi ‘bubu’ mitaani inaibua swali la msingi, ni kwa nini hawataki kutumia stendi kuu ya Magufuli ambayo ina nafasi na imejengwa kwa viwango vya kutoa huduma bora kwa abiria?
Si rahisi kupata jibu la swali hili, mbali tu ya kuelewa kwamba huenda wenye mabasi hawa wanasumbuliwa na kasumba ya kudhani kwamba wanauwezo wa kuendesha stendi zao wenyewe hata kama nafasi na uwezo havipo. Ukiangalia kwa mfano mfumo wa mabasi kuingia eneo la Urafiki na hata miundombinu ya kuwawezesha abiria kufika eneo hilo, utagundua kwamba kinachofanyika ni kuhatarisha siyo tu usalama wa vyombo hivyo vya moto, bali pia na usalama wa abiria.
Mabasi mengi yanayoanzia hizi stendi bubu wala hayajali kupitia stendi ya Magufuli kama yanavyotakiwa na masharti ya leseni zao kutoka LATRA. Kutokufanya hivyo siyo tu ni ukiukaji wa masharti ya leseni, bali pia ni mwendelezo wa kuongeza fujo, vurugu na kufanya juhudi za serikali za kuboresha miundombinu hii kuwa ni kazi bure.
Hali hii haishangazi sana, kwani sasa imekuwa ni kawaida kwa miji yote ya nchi hii kuwapo kwa matumizi mabaya ya miundombinu inayojengwa, lakini walengwa wa huduma hizo wanatoa visingizio vingi vya kukataa kuitumia. Yapo masoko yaliyojengwa maeneo mbalimbali nchini, lakini hayatumiki. Kuna barababara zilizojengwa vizuri na kutengwa maeneo ya watembea kwa miguu, lakini yamevamiwa na kugeuzwa sehemu ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga, na hakuna anayethubutu kuwasogeza.
Hakuna hata mji mmoja katika nchi hii ambako shida hii haijadhihirika. Maeneo mengi ambako barabara mpya zimejengwa au kuboreshwa zimewekewa maeneo ya watembea kwa miguu, lakini kilichopo ni kuvamiwa na wamachinga. Hakuna kiongozi yeyote, siyo wa halmashauri, wilaya, mkoa na hata ngazi ya wizara anayethubutu kuwagusa wamachinga hawa.
Hali hii ya watu kushindwa kwanza kufuata taratibu zilizoko za matumizi sahihi ya miundombinu na pia kushindwa kwa wasimamizi wa maeneo haya kuwashurutisha watu kufuata taratibu zilizoko, ndicho chanzo kikubwa cha miji yetu kuonekana michafu, isiyovutia na hata mara nyingine kuwa chanzo cha uhalifu.
Vurugu na fujo hizi zote vinafanya juhudi za serikali za kuboresha miundombinu hii kuonekana kama ama haina maana kabisa au haijasaidia kuboresha huduma za kijamii, hususan barabara zilizojengwa kwa mabilioni ya fedha.
Ukiwasikia wanasiasa wanapozungumzia hali hii unashindwa kuelewa kama wana nia njema ya kubadili hali duni ya miji yetu kuwa na hali bora zaidi. Kisingizio chao kikubwa ni kwamba wananchi wasibughudhiwe kwa sababu ndiyo wapigakura wao. Aidha, utasikia wakidai kuwa kuwapo kwa stendi bubu ni kuwasogezea wananchi huduma karibu. Katika utetezi huu mwepesi, hutasikia wakilalamikia viwanja vya ndege au bandari, au vituo vya treni kuwa mbali na wananchi. Utetezi huu ni wa kuendekeza uzembe. Ni wakati sasa umefika kwa stendi zilizojengwa kwa gharama ya mabilioni ya fedha za walipa kodi, zitumike ipasavyo ili kuleta tija na kuboresha huduma katika miji yetu.