WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa ameeleza kwamba sheria ambayo ilitumiwa na serikali kuishurutisha kampuni ya simu ya Vodacom kusajili asilimia 25 ya hisa zake katika Soko la Hisa Dar es Salaam DSE imekuwa na matokeo mabaya.
Slaa ambaye alikuwa akizungumza katika kikao kazi cha serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano kinachoendelea katika jiji la Arusha, alisema njia bora ya kukuza sekta yoyote katika zama za uchumi wa soko huria ni kuacha nguvu ya soko itawale badala ya shuruti.
Akifafanua, Silaa alisema kwa kawaida makampuni hujisajili katika masoko ya hisa kama njia ya kuongeza mitaji, ingawa tofauti na ilivyokuwa mwaka 2017, sheria iliyotungwa iliyalazimisha makampuni kujisajili katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.
“Kwa suala la kujisajili katika soko la hisa, kanuni za kawaida kwa taasisi za kibiashara ungetarajia kwa kampuni inayotaka kuongeza mitaji kujisajili. Lakini mwaka 2017 serikali ilitunga sheria ikizitaka kampuni za simu kujisajili katika soko la hisa. Utekelezaji wake umefanyika kwa vodacom. Napata maswali mengi ni lini wengine watajiunga, lakini kwa maelezo yako wale waliotangulia hali haijawa nzuri,” alieleza Waziri Silaa.
Waziri Silaa aliyekuwa akijibu maswali ya wadau wa mawasiliano alikiri kwamba kitendo cha serikali kulazimisha mambo ya namna hiyo, matokeo yake yanaishia kuwa kama hayo yaliyoipata vodacom tangu mwaka 2017.
“Sisi kama serikali tukianza kutengeneza shuruti katika baadhi ya mambo, matokeo yake sasa ndiyo haya. Ulichokisema sina tathmini sahihi lakini ndicho hiki nilichokisema” alisema waziri Silaa.
Kutokana na hali hiyo alisema anaamini ni wakati sahihi sasa kwa serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo na wadau na kufanya tathmini ya kujua ni kipi hasa cha kufanywa kutokana na kadhia za namna hiyo.
“Nadhani ni wakati mwafaka sasa, sisi kama serikali kurudi kwenye meza ya mazungumzo. Kwa kuwa tuna vikao vingi na wadau tutakaa tuangalie, tulikotoka, maamuzi tuliyofanya, tulipo ili tutengeneze utaratibu mzuri huko tunakokwenda,” alisema Silaa.
Alisema kutokana na uzoefu kuonyesha namna Vodacom ilivyofanya vibaya, upo uwezekano wa Bunge kukaa na kuangalia upya sheria hiyo ili kuondokana na adha za namna hiyo.
“Wabunge wako hapa, Kamati ya Bunge (ya Miundombinu) ipo na sheria siyo msahafu. Tunatunga sheria kupeleka mambo yetu mbele, sheria hazitutungii sisi kutu control kwa nachosema na kwa kuwa nimekisema katika mkutano wa wadau, ni wakati mwafaka sisi kukaa na kuangalia njia bora zaidi ya kampuni hizi kujiendesha,” alisema Silaa.
Katika swali lake kwa waziri Silaa mwanahabari mkongwe aliyehudhuria kongamano hilo, Absalom Kibanda aliitaka serikali kutoa kauli ni hatua gani hasa imezichukua ili kuwasaidia wananchi ambao walishurutishwa na Serikali ya Awamu ya Tano kununua hisa za vodacom ambao hadi leo hawajui hatima ya uwekezaji wao katika hiyo kampuni.
Mbali ya hilo, Kibanda ambaye amepata kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri alihoji iwapo serikali ilikuwa haioni kwamba uamuzi ule wa kuilazimisha vodacom kusajiliwa katika soko la hisa kabla ya kuandaliwa kwa mazingira rafiki ndiko ambako kumesababisha sintofahamu iliyopo.
Kibanda pia aliitaka serikali kueleza ni hatua gani basi, itachukua ili kuwanusuru na hasara kubwa Watanzania walioshawishiwa na serikali kuwekeza katika kampuni ya vodacom kupitia hisa walizonua DSE.
Kumbukumbu zinaonyesha kwamba Machi mwaka jana thamani ya hisa za vodacom ambazo mwaka 2017 zilikuwa zikiuzwa kwa shilingi 850, ziliporomoka thamani na kufikia shilingi 740 kwa hisa, kiwango ambacho ni pungufu kwa shilingi 110.
Awali, Machi mwaka 2021, Bodi ya Wakurugenzi ya kampuni hiyo ya simu ya Vodacom ilitangaza kukosekana kwa gawio kwa wanahisa baada ya kuwapo kwa taarifa za kampuni hiyo kupata hasara
Katika taarifa yake bodi hiyo ilisema, kampuni hiyo ambayo imekuwa ikitanabahisha kuwa kampuni kinara wa mawasiliano ilipata hasara ya shilingi bilioni 30.